Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Acha wajee...

Maxi Avic Town Acha wajee...

Thu, 3 Aug 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kuanzia Mei mwishoni hadi Julai mwishoni kimekuwa ni kipindi kibaya kwa wapenzi wa soka kwa kuwa hawakuwa na kitu cha kuwafanya kuwa bize.

Ni kawaida kwa kipindi kama hiki kutokea mara moja kwa mwaka kwa wapenda soka kuwa na kipindi cha upweke kama hiki.

Wakati mwingine mashindano mkubwa kama Kombe la Dunia, Michuano ya Euro na mingine mingi hufanyika kwenye kipindi hiki ili kuwapa nafasi mashabiki ya kuendelea kufurahia soka, lakini kwa msimu huu mambo yalikuwa tofauti kabisa kulikuwa hakuna ubize wowote.

Leo ni Agosti 3, mwezi ambao wana soka wanaanza kula bata na ubishi wa nani anakuwa bingwa, nani atakuwa mfungaji bora wa ligi flani utaanza kuonekana hapa.

Kwa hapa nchini mambo yaanza mapema baada ya timu kuanza kurejea kutoka sehemu mbalimbali zilipokuwa zimekwenda kuweka kambi ya maandalizi, Azam na Simba, ni kati ya zile kubwa ambazo zilikuwa nje ya nchi na sasa zinarudi kumalizia maandalizi.

Chini ni mashindano makubwa ambayo yanaanza mwezi huu kwenye viwanja mbalimbali, na pia matukio ambayo mashabiki wanayasubiri:

SIMBA DAY

Maadhimisho ya Tamasha kubwa la Simba Day yanatarajiwa kufanyika Agosti 6 kwenye Uwanja wa Mkapa, ukiwa ni muendelezo baada Yanga kufanya lao la Wiki ya Mwananchi mwishoni mwa mwezi uliopita.

Hili lilikuwa tamasha la kwanza kuwahi kufanywa na klabu hapa nchini la kuwatangaza wachezaji wake wapya ambapo ndiyo litaanza kuonyesha timu hiyo ina mastaa gani kwa msimu huu na itakuwa mara yao ya kwanza kuwaona wachezaji kama Willy Onana, Fabrice Ngoma na kipa wao mpya atakayetangazwa hivi karibuni baada ya kuachana na Mbrazili.

NGAO YA JAMII

Kwa mara ya kwanza Tanzania Ngao ya Jamii itakuwa ikichezwa kwa mfumo wa mtoano, hii ni tofauti na ilivyokuwa kwenye misimu mingine iliyopita jambo ambalo linawafanya mashabiki kuwa makini sana kuona nini kitatokea.

Ngao ya Jamii itafanyika mkoani Tanga kwenye Uwanja wa Mkwakwani kuanzia Agosti 8-13, ambapo Yanga itavaana na Azam FC na Simba itaanza kwa kuvaana na Singida Fountain Gate, ambapo wawili kati yao watacheza mchezo wa fainali Agosti 13, kwenye uwanja huohuo.

Haya yatakuwa mashindano ya kwanza kuwaleta mashabiki pamoja ambapo wataanza kuwatazama kwa uzuri mastaa wao ambao wamesajiliwa kwenye dirisha usajili.

RATIBA YA LIGI KUU BARA

Pamoja kwamba Ligi Kuu Bara inafahamika kuwa itaanza Agosti 15, bado kiu ya mashabiki kwa sasa ni kufahamu ratiba kamili ya ligi hiyo itakavyokuwa.

Hadi sasa hakuna timu inayotambua itaanza na nani, lakini kwenye ratiba hiyo ambayo itatoka siku chache zijazo, inasubiriwa kujua timu za Simba na Yanga zitavaana tarehe ngani na mwezi gani, ili mashabiki waanze kuona makali ya timu zao na nani atakuwa mbabe wa mwenzake kwenye ligi msimu huu.

Lakini pia inaaminika kuwa ratiba italazimika kutoka mapema ili kila timu zifahamu zinaanzaje kujipanga kwa ajili ya michezo ya mwanzoni kwa kuwa nyingi zitakuwa na safari ya kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine.

Pamoja na kuzitazama timu lakini bado mashabiki watakuwa na nafasi ya kuwatazama baadhi ya mastaa ambao wamekuwa gumzo kwenye usajili uliopita akiwamo, Yanick Bangala, Feisal Salum ambao wametoka Yanga na kutimkia Azam FC.

NGAO YA JAMII ENGLAND)

Ngao ya Jamii ya Ligi Kuu England (Premier League), ambayo inasubiriwa kwa hamu kuwa na mashabiki wa soka hapa nchini itapigwa Agosti 6 kwenye Dimba la Wembley.

Huu ni mchezo mkubwa kwa mashabiki wa Arsenal ambao msimu uliopita walimaliza nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu England na mabingwa watetezi wa Ligi Kuu England, Manchester City.

Kwa Arsenal watataka kuona kama timu yao itaweza kuonyesha umwamba wao kwa City, lakini kwa wale wa City itakuwa nafasi kwao kuona kama wanaweza kuendeleza moto wao kwa wapinzani wao ambao wamekuwa wakiwanyanyasa mara kwa mara.

EPL HII HAPA

Pamoja na ligi nyingine kuwa za moto, lakini ni sahihi kusema kuwa mashabiki wa soka la Tanzania wamekuwa wakiisubiri Ligi Kuu ya England hii kwa hamu zaidi kutokana na umaarufu wake hapa nchini.

Mashabiki wanasubiri ligi hiyo ambayo itaanza Agosti 11, kwa mchezo mmoja kati ya wageni kwenye ligi hiyo, Burnley ambao watawakaribisha mabingwa watetezi Manchester City.

Baada ya hapo, Jumamosi ya Agosti 12 ndiyo timu nyingine nyingi zitaingia uwanjani ikiwamo Arsenal, Manchester United, Liverpool na hata Chelsea kwa ajili ya kuanza kasi ya kuwania ubingwa huo hadi Mei mwakani.

LIGI YA MABINGWA AFRIKA

Hii ni hatua nyingine muhimu kwa mashabiki wa soka kusubiri kuona maajabu ya michuano hii mikubwa Afrika wakati ambapo zitachezwa mechi za hatua ya awali.

Agosti 26, mashabiki watakuwa macho muda wote kusubiri mechi kali ya hatua hivyo kati ya Yanga na Asas ya Djibout, endapo Yanga itafuzu hapa basi itakwenda hatua ya kwanza ya michuano hii ili kuanza safari ya kuwania ubingwa wa michuano hiyo mikubwa Afrika.

Mbali na Yanga hatua hii pia baadhi ya timu nyingine kama KMKM, Power Dynamos, Vipers, Medeame, Orlando Pirates, Enyimba Cotton Sports zitakuwa uwanjani siku hiyo kwa ajili ya kuanza safari rasmi ya mafanikio makubwa kwenye soka Afrika.

Pia Kombe la Shirikisho Afrika litaanza mwezi huu, huku kuna vigogo kama Azam, FAR Rabat na wengine wengi wakitafuta njia ya kutinga fainali.

MACHO KWA MAKOCHA WAPYA

Wakati mwezi huu mashabiki wanaanza kuwatazama mastaa wao, siyo ajabu kengele ya hatari kwa makocha wapya kwenye timu na wa zamani ikaanza kulia kutokana na kupewa imani kubwa sana.

Ngao ya Jamii inaweza kuanza kwa manung’uniko kwa mashabiki kama timu zao zitafanya vibaya kwa kuwa nyingi makocha wake wamepewa kila kitu wanachotaka.

Presha kubwa itakuwa na timu zinazoshiriki michuano ya kimataifa, Simba, Yanga, Azam na Singida ambazo makocha wake wamepewa mikwanja mirefu kwa ajili ya kufanya usajili mzuri.

Mbali na kuwatazama hawa, bado mashabiki watakuwa wanatupa macho yao kwa makocha walioondoka nchini akiwamo, Nasreddine Nabi aliyejiunga na FA Rabat akitokea Yanga.

MIPIRA MIPYA YA LIGI

Kwa Tanzania, Ligi Kuu Bara kumekuwa na mipira mipya ambayo hutolewa na wadhamini kwa ajili ya ligi hiyo, hivyo hivyo kwa michuano mingine Ulaya, pamoja na mashabiki kusubiri kuona mwaka huu itatumika mipira ya aina gani, pia mastaa uwanjani nao huwa na hali hiyohiyo.

Mipira hii mara nyingine makipa na washambuliaji ndiyo huwa wanaisubiri kuona kama itakuwa na faida kwao au itakuwa shubiri, mara nyingi makipa huchukia kama itakuja mipira inayoteleza, kwa washambuliaji wamekuwa wakitaka mipira inayokwenda kwa kasi zaidi.

USAJILI WA MWISHO MWISHO

Bahati mbaya au nzuri ni kwamba kwa msimu huu ligi inaanza wakati ambapo bado dirisha la usajili halijafungwa hivyo bado kuna nafasi ya makocha kuona kama kuna mchezaji hawafai basi wanaweza kuachana naye kabla dirisha halijafungwa, au wakiona kuna sehemu ya kuongeza basi hiyo itakuwa upande wao.

Tunachosubiri ni kuona nini ambacho kitatokea kabla dirisha la usajili Bara halijafungwa mwishoni mwa mwezi huu.

LIGI NYINGINE KUBWA

Ligi nyingine kubwa ambazo zinafuatiliwa sana na mashabiki ni pamoja na Ligue 1 ya Ufaransa ambayo ina mastaa kama Kylian Mbappe na Neymar JR itaanza Agosti 12.

Kwa upande wa Ligi Kuu ya Hispania, La Liga ambayo kwao mastaa ni jambo la kawaida, wakiwamo Vinicius Junior wa Real Madrid inaanza Agosti Agosti 11.

Ligi Kuu ya Italia, ambayo timu zake msimu uliopita zilifanya vyema kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, pamoja na Europa Cup, hii itaanza Agosti 20, huku Bundesliga ikitarajiwa kuanza Agosti 18.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: