Historia inazichonganisha Simba na Azam FC wakati zitakapokutana leo Jumapili kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara katika mchezo wa hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC), kuanzia saa 9:30 alasiri.
Kumbukumbu ya mechi mbili za Ligi Kuu baina yao msimu huu na ile ya mchezo ambao zilikutana nusu fainali ya ASFC msimu wa 2020/2021, zinafanya kila timu iwe na hamu ya kuibuka na ushindi katika mchezo huo, sio tu kwa ajili ya kutinga hatua ya fainali pekee bali pia kulipa kisasi kwa nyingine kutokana na historia isiyovutia katika mechi zilizowakutanisha kwenye ligi na ASFC.
Simba wao wana hamu ya kulipa kisasi cha unyonge wao mbele ya Azam kwenye Ligi Kuu msimu huu ambapo katika mechi mbili walizokutana, walipoteza moja na mchezo mwingine mmoja ukamalizika kwa sare ya bao 1-1.
Kwa upande wa Azam wao wanakumbuka mechi ya nusu fainali ya ASFC dhidi ya Simba, msimu wa 2020/2021 iliyochezwa Uwanja wa Majimaji huko Ruvuma ambao walipoteza bao 1-0 na kutupwa nje katika mashindano hayo.
VITA YA WANAUME
Timu hizo zimekuwa na mwenendo wa kibabe kwenye mashindano hayo msimu huu na uthibitisho wa hilo ni mechi za raundi nne zilizopita kwa kila upande ambapo zimeonekana kuwa tishio katika kufumania nyavu huku zikionyesha kuwa na ukuta imara.
Katika mechi nne zilizopita za mashindano ya ASFC, Simba imeibuka na ushindi katika dakika 90 mara zote nne ikifunga mabao 18 sawa na wastani wa mabao 4.5 kwa mechi huku ikifungwa bao moja tu wakati huo Azam FC yenyewe imeshinda mechi zote zilizopita kwa muda wa kawaida wa mchezo, ikifunga mabao 17 sawa na wastani wa mabao 4.3 kwa mechi na imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara moja tu.
HUKU MKOSI, KULE BAHATI
Mechi za nusu fainali ya ASFC zimekuwa na upepo usioeleweka kwa Azam FC kwani katika mara nne ilizowahi kutinga hatua hiyo, ilipoteza mara mbili na kupata ushindi mara mbili tofauti na Simba ambayo angalau imekuwa na bahati ya nusu fainali.
Simba imeingia hatua ya nusu fainali ya mashindano ya ASFC mara nne na katika awamu hizo, mara tatu ilipata ushindi huku ikipoteza mechi moja. Mbali na hilo, timu hizo zimekutana mara mbili tofauti katika mashindano ya ASFC na mara hizo zote, Simba waliibuka na ushindi.
REKODI KUSAKWA
Kiu ya kuibuka na ushindi katika mchezo huo inachagizwa kwa kiasi kikubwa na hamu ya kutwaa ubingwa ya mashindano hayo kwa kila timu ili iweke mpya ama ifikie rekodi ambayo imewahi kuwekwa hapo nyuma.
Ushindi kwa Simba utaiweka katika mazingira mazuri ya kuzidi kuimarisha rekodi yake ya kuwa timu iliyotwaa taji hilo mara nyingi zaidi ambapo hadi sasa inaongoza ikiwa imeshachukua mara tatu ikifuatiwa na Yanga iliyotwaa mara mbili. Kwa Azam FC yenyewe inapambania kufikia rekodi ya Yanga ya kutwaa ubingwa wa mashindano hayo mara mbili.
Mara ya mwisho Azam FC kutwaa ubingwa wa mashindano hayo ilikuwa ni msimu wa 2018/2019, ambapo iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Lipuli wakati Simba ilitwaa ubingwa wa mashindano hayo kwa mara ya mwisho katika msimu wa 2020/2021, ilipoibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Yanga.
MIAMBA HII HAPA
Mfungaji bora wa mashindano hayo msimu uliopita, Abdul Selemani 'Sopu' ndio kinara wa ufungaji katika kikosi cha Azam FC kwenye mashindano ya ASFC msimu huu, akipachika mabao matatu huku Kipre Junior na Cyprian Kachwele kila mmoja akipachika mabao mawili.
Kwa upande wa Simba, vinara wa kufumania nyavu katika mashindano hayo ni Jean Baleke na Moses Phiri ambao kila mmoja amepachika mabao manne.
MAKOCHA
Akizungumzia maandalizi ya mchezo huo Kocha Mkuu wa Azam, Kally Ongala alisema; "Kila mmoja wetu anajua umuhimu wa mchezo huo na jambo jema ni kuona wachezaji wote wameonyesha mazoezini ni kwa jinsi gani wanauhitaji, morali kwao ni kubwa kitu ambacho hata sisi benchi la ufundi kinatupa imani."
"Ukiangalia wote tunakutana tukihitaji hili taji baada ya kutokuwa na msimu mzuri katika mashindano mengine sasa hii ni picha halisi ya kukuonyesha ni mchezo mgumu kwa kiasi gani hasa ukichagizwa pia kwa sababu ni wa mtoano."