Mlinda Lango chaguo la Pili wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans Abutwaleeb Mshery, anatarajiwa kwenda nchini Tunisia kwa ajili ya matibabu.
Mlinda Lango huyo kwa muda mrefu amekua nje ya kikosi cha Young Africans akiuguza majeraha ya goti, ambayo yalipelekea klabu hiyo kumsajili kwa mkopo Metacha Mnata kupitia Dirisha Dogo.
Taarifa zinaeleza kuwa Msheri ataongoza na kikosi cha Young Africans kuelekea Tunis-Tunisia kwa ajili ya mchezo wa Mzunguuko wa Kwanza Hatua ya Makundi Kombe la Shirikisho Barani Afrika, lakini atabaki huko kwa ajili ya kufanyiwa matibabu.
Msheri atapelekwa kwenye Hospitali iliyowatibu Kibwana Shomary na Yacouba Songne ambapo Matibabu waliyoyapata kwenye Hospitali hiyo inayosifika kwa kutoa tiba nzuri iliwasaidia kurejea Uwanjani mapema.
Kikosi cha Young Africans kinatarajiwa kuondoka jijini Dar es salaam Jumanne (Februari 07), tayari kwa mchezo wa Kundi D, Kombe la Shirikisho Barani Afrika utakaowakutanaisha dhdi ya US Monastir, Jumapili (Februari 12).