Hisia zilikuwa mkanganyiko wakati mashabiki wa Simba walipoondoka Uwanja wa Chamazi juzi. Ni kama wale waliokuwa katika baa na vibanda umiza wakitakazama mechi hii dhidi ya Power Dynamos ya Zambia. Walikuwa wamepita kwenda katika hatua ya makundi. Halikuwa jambo la ajabu sana.
Wamezoea kupita kuingia katika hatua hii. Tatizo ni wamepitaje kwenda katika hatua hii? Jina la kocha anayeitwa Robertinho likageuka maarufu katika midomo ya mashabiki wa Simba. Halikutajwa sana kwa mazuri.
Katika mechi ambayo Simba ilihitaji sare ya mabao machache au suluhu au ushindi wa namna yoyote ile, Power Dynamo ikajikuta ikifunga mabao yote mawili ya mechi. Moja ilifunga kwa ajili yao na jingine ikaifungia Simba.
Haikuwafurahisha mashabiki wa Simba. Waliitaka Simba inayochezwa kwa swaga, kwa maringo. Inayocheza kiasi shabiki anatamani mpira usiishe. Inayocheza katika namna ambayo shabiki anatamani kiingilio kiongezwe. Sio Simba hii.
Kutia chumvi katika kidonda, mpira huu kwa sasa unachezwa na watani zao, Yanga. Hiki ndicho kitu ambacho kinatia hasira zaidi. Kwamba miaka michache iliyopita Simba ilikuwa inatawala mechi dhidi ya AS Vita, Al Ahly na wengineo. Leo inacheza kawaida dhidi ya Wazambia.
Iko wapi Simba ya Larry Bwalya, Clatous Chotta Chama, Jose Lous Miquissone, John Bocco, Meddie Kagere na Hassan Dilunga? Simba inayocheza kwa swaga. Hapa ndipo mashabiki wanaposhindwa kumuelewa Robertinho.
Watu wa karibu na Robertinho wanapaswa kumwambia kitu mapema. Watu wake wa karibu ambao ni Watanzania. Wamwambie kitu. kazi yake ipo shakani. Haijalishi na matokeo ambayo ameyapata.
Ameshinda mechi zote za Ligi kuu na timu imekwenda katika makundi. Ameshinda pia Ngao ya Jamii pale Tanga. Hata hivyo, anaishi katika nchi ambayo yote hayo hayatoshi na ukweli ni kwamba anaishi katika nchi ngumu kuliko anavyodhani.
Yote haya hayatoshi kwa sababu amewekewa kipimo kingine katika matokeo yake. Yaje huku wakiwa wanacheza kama Yanga. Kama Yanga wangekuwa wanacheza kama wakati ule wakiwa na akina Abdulaziz Makame basi mashabiki wasingelalamika. Lakini Yanga inacheza mpira wa kuvutia zaidi na hii inawatesa Simba.
Nilichokiona katika mechi ya juzi ni kwamba Simba haiko fiti sana. Haipigi pasi kwa haraka. Haifungui nafasi kwa haraka zaidi. haikabi kwa haraka zaidi. Inaitwa pressing. Haifanyi mambo mengi kwa haraka.
Mpira wa kisasa unataka wachezaji wafanye mambo mengi kwa haraka zaidi. Baada ya hapo ukiunganisha na vipaji vya wachezaji waliopo ni wazi kwamba utatawala mechi ya soka. Inawezekana Robertinho kuna kitu anakitengeneza lakini kinaathiriwa na kocha wake wa viungo.
Inawezekana kocha wa viungo kuna kitu anakifanya lakini mbinu za Robertinho hazifanyi kazi kwa wachezaji wake. Mwisho wa siku atakayeondoka ni Robertinho. Kwa namna ninavyoona mashabiki wameanza kupoteza imani naye.
Makocha wengi wanaondolewa na mashabiki. Wachezaji wengi wanawekwa benchi na mashabiki. Kinachotokea ni mashabiki kupiga presha kwa viongozi kuachana na kocha. Lakini katika kundi la viongozi unakutana na baadhi yao wanaunga mkono mawazo ya mashabiki.
Kadiri siku zinavyokwenda ndivyo ambavyo Robertinho anajipeleka huku. Usijali sana kuhusu kile kinachoitwa mafanikio au kufikia malengo lakini mashabiki wa siku hizi nao wanafahamu soka. Wanajua kwa mfano Tanga walichukua Ngao ya Jamii lakini Yanga ilitawala mechi kwa dakika 90.
Wanajua Simba imekwenda katika hatua ya makundi kama ilivyo kwa Yanga lakini watani wao wanakwenda wakiwa na timu ya kushindana zaidi kuliko wao. Wanataka timu yao ibadilike kwa sababu wanaifahamu timu yao.
Timu yao ambayo iliongoza kundi kwa pointi 13 dhidi ya Al Ahly na AS Vita sio hii hapa. Ni kweli kuna takwimu za hapa na pale za kujiliwaza lakini wakati mwingine kama hauchezi vizuri sana basi unakaribia matokeo mabovu. Linakuwa ni suala la muda tu.
Labda jambo hili ndio ambalo linambeba Robertinho mpaka sasa lakini tajiri wa timu Bwana Mohamed Dewji anapokwenda katika mtandao wake wa Twitter na kuandika kwamba timu inakaribia kumuua kwa presha kwa namna inavyocheza basi ujue kocha anaanza kukalia kuti kavu.
Na sasa Simba na Yanga zote zimekwenda makundi. Ijumaa tutawajua wababe wao. Timu za Tanzania kwa sasa zipo tayari kushindana na yoyote yule. Na unapokwenda katika hatua ya makundi ya michuano hii tegemea kucheza na timu zenye ubavu zaidi.
Kitu kinachovutia kwa mara ya kwanza wote wamekwenda makundi katika michuano hii. siku hizi za karibuni wamehamishia upinzani wao katika mechi za kimataifa. Zamani walikuwa wanabishana zaidi kuhusu nani amemfunga mwenzake mara nyingi au nani amechukua ubingwa mara nyingi.
Sasa wamehamishia katika mafanikio ya michuano ya CAF. Simba ilikuwa inaicheka zaidi Yanga kwa kufanya vibaya katika michuano hii.
Na sasa kuchekana kwao ndio kusukumana kwao kuelekea katika mafanikio. Nani ataishia makundi? Nani atasonga mbele? kwa ninavyowafahamu ni kwamba nafuu pekee ni pale wote wakitolewa makundi au wote wakienda robo fainali. Vinginevyo nchi itasimama kumkebehi mmoja.
Robertinho abadili upepo uliopo. Hatua anayokwenda ni ngumu zaidi ni ni vigumu kupata matokeo kwa kubahatisha. Ukitolewa jasho na Power Dynamo basi bado haujapata nguvu za kupambana na Mamelodi.