Wakati hatua ya pili ya michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) ikimalizika kwa baadhi ya timu zikivuna zilichopanda, rekodi na historia zimewekwa kwenye mashindano hayo, huku vigogo Simba na Yanga wakisubiriwa.
Mashindano hayo yalishirikisha timu 64 kuwania kutinga 32 bora ya michuano hiyo ambayo Yanga ndiye bingwa mtetezi na haijashuka uwanjani kukutana na Hausung ya mkoani Njombe.
Mbali na Yanga, watani wao Simba nao wanasubiri tarehe rasmi kunyukana na Tembo FC ya mkoani Tabora inayoshiriki Ligi ya Mkoa huo kupata atakayeungana na wapinzani wao waliotangulia mapema.
Katika michuano hiyo ambayo ilihitimishwa juzi Jumapili kwa mechi 30, ilishuhudiwa baadhi ya timu kubwa zikiwamo za Ligi Kuu zikisombwa na upepo kwa kukubali vipigo na kuaga mashindano hayo.
HAT-TRICK
Kama ilivyokuwa msimu uliopita kushuhudiwa wachezaji wakiondoka na mipira yao kwa kufunga mabao matatu na zaidi, msimu huu pia rekodi zimeendelezwa kwa mastaa kufanya kweli.
Wachezaji watano wa timu tofauti hawakufanya makosa kwa kufunga idadi ya mabao matatu (hat-trick) na kuondoka na mpira kila mmoja na kufuzu hatua ya 32 bora.
Wachezaji hao ni Edward Songo aliyetupia matatu wakati JKT Tanzania ikiinyuka Kurugenzi FC 5-0, Paschal Wagana aliyefunga idadi kama hiyo akiisaidia Biashara United ikitakata 4-1 dhidi ya THB na Kelvin Sabato aliyeifungia Namungo mabao matatu wakiibuka na ushindi wa 5-0 dhidi ya Hollywood.
Wengine ni Shaban Seif wa Mbuni aliyetupia matatu kwenye ushindi wa 6-2 dhidi ya Bus Stand FC na Yohana Mkomola wa Tabora United aliyeweka tatu akiipa timu yake ushindi wa 4-1 mbele ya Monduli Coffee.
PRISONS, KEN GOLD HOI
Katika michuano hii, Tanzania Prisons ya Ligi Kuu iliwashangaza wengi kwa kuondoshwa katika michuano hiyo ilipochapwa na TRA ya First League.
Katika mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Sokoine, Prisons ikiwa na mastaa wake wote haikuamini kilichowakuta kwa kukunjwa penalti 6-5 baada ya dakika 90 kuisha kwa suluhu.
Matokeo hayo yaliifanya timu hiyo kuwa ya kwanza Ligi Kuu kuaga michuano hiyo ikiwa ni mara ya kwanza kwa maafande hao kutupwa nje ya mashindano hayo.
Mbali na Prisons huko Championship napo hali ilikuwa tete, kufuatia vinara wa ligi hiyo, Ken Gold kutupwa nje dhidi ya Gunners FC ambao ni bingwa wa Mkoa wa Dodoma waliposhinda bao 1-0.
Pia timu za Cosmopolitan, Ruvu Shooting, Pan African na Copco FC zilijikuta zikiondoshwa kwa aibu mbele ya wapinzani wao wanaocheza ligi za chini ikiwamo ngazi ya mkoa.
Ruvu ilinyolewa kwa bao 1-0 dhidi ya Mkwajuni inayoshiriki ligi ya Mkoa wa Songwe, Copco ikalazwa 2-1 mbele ya Mabao FC ya Shinyanga na Cosmopolitan ikafa 2-1 na Rhino Rangers ya First League.
MVUA YA MABAO
Kama ilivyoshuhudiwa msimu uliopita kwa baadhi ya timu kukumbana na vipigo vizito juzi pia mvua ya mabao ilizikumba baadhi ya timu na kujikuta zikiaga michuano hiyo.
Msimu uliopita Malimao FC ilikula kibano cha mabao 9-0 dhidi ya Azam, Yanga ikiirarua Kurugenzi mabao 8-0, huku Simba nayo ikiiangushia kichapo African Sports cha mabao 4-0.
Msimu huu Sharp Lion ndio ilikumbana na aibu ya kipondo kizito cha 7-2 dhidi ya TMA, Mbuni ikaiburuza 6-2 Bus Stand, Namungo ikaigaragaza 5-0 Hollywood na Geita Gold nayo ikaichakaza 5-0 Singida Cluster.
Pia Tabora United iliikanda 4-1 Monduli Coffee, Green Warriors ikaichapa 4-1 Kilimo FC na Biashara United ikashinda 4-1 dhidi ya THB na kufanikiwa kufuzu hatua ya 32 ya michuano hiyo.
WASIKIE MAKOCHA
Kocha mkuu wa Gunners, Juma Maulid anasema baada ya kufuzu hatua inayofuata kwa sasa wanaenda kujipanga kumkabili yeyote watakayepangwa naye akisema kuwa nia yao ni kufika fainali.
Anasema pamoja na ugumu wa michuano hiyo, lakini kuwafunga Ken Gold timu yenye upinzani mkali na iliyowaacha kwenye soka, si kitu kidogo na inawapa mwanga kufikia ndoto.
“Tunamsubiri yeyote na tuko tayari kupambana kuhakikisha tunafika mbali, iwe Simba, Yanga au Azam tutafurahi kukutana naye kwani itaendelea kutuweka pazuri na kututangaza,” anasema.
Nyota wa TRA, Mohamoud Rashid anasema licha ya kuwa First League lakini kiu yao ni kucheza fainali akitamba kuwa kumfunga Prisons haikuwa kazi rahisi isipokuwa kujituma.
Anasema licha ya mashindano ya First League waliyonayo lakini watahakikisha wanajipanga kufanya vizuri kila eneo ili kupanda championship akiwaomba wenzake kikosini kuendelea kukaza.
“Mashabiki waendelee kutupa sapoti na sisi tutapambana kuhakikisha tunafika mbali kwenye hii michuano na First League, hatuogopi yeyote bali kuheshimu kila timu,” anasema kipa huyo.
Kocha mkuu wa Ken Gold, Jumanne Chale anasema baada ya kuaga michuano hiyo akili na nguvu zote zinaelekezwa kwenye Championship kuhakikisha timu inapanda Ligi Kuu.
Anakiri kuwa vijana wake hawakuwa kwenye ubora katika mchezo wao dhidi ya Gunners na kujikuta wakicheza chini ya kiwango kwa kuonekana kuwadharau wapinzani.
“Ni kama waliwadharau kwa sababu hata kucheza kwao hakukuwa katika ubora nilioutaka wa siku zote, lakini mpira ndio ulivyo, tutaelekeza nguvu sasa kwenye Championship kupandisha timu Ligi Kuu,” anasema Challe.