Kocha Msaidizi wa AS Vita ya DR Congo, Raoul Shungu amewapongeza Yanga baada ya kufanikiwa kutinga fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika lakini amewaonya mastaa wa timu hiyo kwa kuwaambia kama wanataka kombe hilo basi wahakikishe wanajitoa kwa uwezo wao wote.
Shungu ametoa kauli hiyo kufuatia Yanga kufuzu fainali ya michuano hiyo baada ya kuiondosha Marumo Gallants ya Afrika Kusini kwa jumla ya mabao 4-1.
Sasa Yanga itacheza fainali ya michuano hiyo dhidi ya USM Alger ya Algeria ambao wao waliitoa Asec Mimosas ya Ivory Coast kwa jumla ya mabao 2-0. Fainali ya kwanza ya michuano hiyo imepangwa kupigwa Mei 28, mwaka huu katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kabla ya mchezo wa marudiano utakaopigwa Juni 3, nchini Algeria.
Akizungumza na Championi Ijumaa, Shungu alisema kuwa Yanga wana kila sababu ya kujipongeza kwa kuweza kufikia hatua hiyo lakini wanapaswa kutambua kazi kubwa iliyopo mbele yao ni wachezaji wa timu hiyo kuweza kujitoa zaidi ili kufikia malengo ya kuchukua ubingwa huo.
“Binafsi kwanza niwapongeze Yanga kwa hatua kubwa ilipiga kwa kuweza kufika fainali ya Kombe la Shirikisho kwa sababu ni jambo kubwa na imekuwa ni mara ya kwanza upande wao kuweza kufikia hatua hiyo lakini ukiangalia kwa sasa tayari wa ubingwa wa Ligi Kuu tayari na sasa wanaenda kucheza fainali ya Afrika kitu ambacho ni kikubwa kwa kuwa wachezaji wao wamejitoa kwa nafasi kubwa.
“Lakini wanatakiwa kujua kazi iliyokuwa mbele ni kubwa na ngumu zaidi kwa sababu fainali kila timu huwa inakuja na mpango ambao huenda hakuwa umeutarajia na ninachotaka kuwaambia wachezaji wanatakiwa kujua ukubwa wa jukumu la mechi mbili za fainali ya CAF ambayo wanatakiwa kuipigania kwa kujitoa zaidi pamoja na kuongeza nidhamu ya mchezo kutokana na aina ya timu wanayokwenda kucheza nao,” alisema Shungu.