Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

ANOTHER CHANCE: Mastaa 15 Simba wanaojaribu tena kuivusha robo fainali

Simba Robo Sm ANOTHER CHANCE: Mastaa 15 Simba wanaojaribu tena kuivusha robo fainali

Wed, 6 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Simba kumla swala sio habari, ila swala kumla simba ni habari kubwa na ya kufikirisha. Hivyo ndivyo ilivyo kwa Klabu ya Simba ambapo kwa sasa kutinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika sio jambo gumu, lakini ugumu unakuja linapokuja suala la kuvuka hatua hiyo.

Katika misimu saba mfululizo tangu 2018/2019 hadi 2023/2024, Simba imeingia robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mara nne katika misimu ya 2018/2019, 2020/2021, 2022,2023 na 2023/2024.

Pia msimu wa 2021/2022 iliingia robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika huku misimu miwili ya 2019/2020 na 2021/2022 ikitoka kapa, lakini sio haba kwani katika misimu saba imeingia robo fainali za michuano ya CAF mara tano.

Timu hiyo imeingia maara tatu kwenye Ligi ya Mabingwa na moja kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, lakini imekuwa ikikwama kuvuka hatua hiyo ya robo fainali.

Msimu huu imeingia tena. Je itavuka? Itafahamika baadaye. Hata hivyo katika kikosi cha Simba cha sasa kuna wachezaji waliofika robo fainali mara tatu, mbili na moja na kote wakashindwa kuivusha timu hiyo, hivyo sasa ni nafasi yao tena kujaribu kuipeleka hatua hiyo na kuweka rekodi. Wasome hapo chini.

MARA TATU

Aishi Manula, Shomari Kapombe, Mzamiru Yassin, John Bocco na Clatous Chama walikuwa kwenye vikosi vya Simba katika misimu mitatu ambayo timu hiyo ilifika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Wakali hao ambao bado wapo kwenye kikosi hicho hii ni mara ya nne kwao kufika robo fainali na wakati wao kujaribu tena kuivusha Simba kwani mara tatu walizofika hapo walishindwa kuvuka.

Msimu wa kwanza 2018/2019 waliondolewa na TP Mazembe kwa jumla ya mabao 4-1 baada ya kutoa suluhu kwenye mchezo wa nyumbani Uwanja wa Benjamin Mkapa na walipokwenda ugenini DR Congo wakachapwa 4-1 na Simba kuondolewa. Bao la kufutia machozi kwa Simba lilifungwa na Emmanuel Okwi.

Msimu wa pili, 2020/2021, waliondolewa na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini kwa ushindi wa jumla 4-3, ambapo Simba ilianzia ugenini na kupigwa mabao 4-0 na mchezo wa marudiano kwa Mkapa, Mnyama alishinda 3-0 na safari ikaishia hapo.

Mabao ya Simba kwenye mechi hiyo yalifungwa na Bocco aliyecheka na nyavu mara mbili na Chama bao moja. Msimu huo Kaizer ilifika fainali, lakini ikapoteza kwa kuchapwa na Al Ahly mabao 3-0.

Msimu wa tatu ni 2022/2023 walioondolewa na Wydad Casablanca kwa mikwaju ya penalti 4-3 baada ya matokeo ya jumla kuwa 1-1.

Hapo Simba ilianzia kwa Mkapa ikashinda bao 1-0 lililofungwa na Jean Baleke na kwenda ugenini Morocco ambako ilichapwa 1-0 na kupigwa mikwaju ya penalti ambapo ilifunga kupitia Erasto Nyoni, Saidi Ntibanzokiza na Moses Phiri huku Kapombe na Chama wakikosa na safari kuishia hapo.

MARA MBILI

Ally Salim na Kennedy Juma wameshindwa mara mbili kuivusha Simba kwenda nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa na sasa ni msimu wao wa tatu kufika hapo wakiwa na nafasi ya kujaribu kuipeleka hatua inayofuata.

Wawili hao walikuwepo kwenye vikosi vya Simba vilivyofika na kukwamia robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa msimu wa 2020/2021 ambapo Simba iliondoshwa kwa jumla ya mabao 4-3 na Kaizer Chief na uliopita ilipoondolewa na Wydad kwa matuta.

Salim na Kennedy msimu huu wamepata nafasi ya kujaribu kuivusha Simba, hivyo mashabiki wanasubiri kuona watafanya nini kama watapewa nafasi.

MARA MOJA

Ahmed Feruzi, David Kameta, Israel Mwenda, Henock Inonga, Luis Miquisson, Saido Ntibanzokiza, Kibu Denis na Sadio kanoute kila mmoja akiwa na jezi ya Simba amefika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kuishia hapo.

Huu ni wakati wao kufanya maajabu ya kuvuka hatua hiyo. Kwa sasa wanasubiri kujua nani watapangiwa kati ya Al Ahly kutoka Misri, Petro De Luanda ya Angola na Mamelodi Sundowns kutoka Afrika Kusini katika droo itakayochezeshwa Machi 12, 2024.

Simba itaanzia nyumbani mechi ya kwanza ambayo itapigwa mwishoni mwa mwezi huu.

Chanzo: Mwanaspoti