Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

AFRICAN FOOTBALL LEAGUE: Wikiendi ya utamu Dar

TP Mazembe Official.jpeg AFRICAN FOOTBALL LEAGUE: Wikiendi ya utamu Dar

Fri, 20 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Baada ya Simba na Al Alhy, kuzindua michuano mipya ya African Football League leo kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam, dimba hilo litachezewa mechi nyingine ya michuano hiyo, keshokutwa Jumapili, kati ya wababe wa DR COngo, TP Mazembe na Esperance Sportive de Tunis ya Tunisia.

Hii ni michuano mipya na huu utakuwa mchezo wa pili baada ya ule wa Simba unaopigwa leo, mashabiki watakuwa macho kwenda kuutazama na kuona muendelezo wa michuano hiyo.

Mchezo huo umehamishiwa Kwa Mkapa baada ya kile kinachoelezwa, Serikali ya DR Congo imegoma kutoa kibali cha kuingiza nchini humo vifaa mbali mbali vya maandalizi ya mchezo huo kutoka CAF.

Mwanzo mechi hiyo ilipangwa kupigwa Oktoba 21 mjini Lubumbashi lakini ikabadilishwa na sasa itachezwa Kwa Mkapa, Dar es Salaam, Oktoba 22 na mechi ya marudiano itakuwa Oktoba 25, Rades, Tunis.

Mwanaspoti kupitia makala hii, linakuletea kwa ufupi historia ya timu hizo mbili kabla ya mechi hiyo inayotarajiwa kuwa na ushindani wa aina yake, huku Mazembe wakiwa na makombe matano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

TP MAZEMBE

Hawa ni wababe wa soka kutoka DR Congo, timu iliyoanzishwa mwaka 1993, ambapo jezi zao ni nyeusi na nyeupe zilizochanganya rangi hizo.

Mazembe kwa Afrika ni timu tishio kwani imetwaa taji la Ligi ya Mabingwa Afrika mara tano nyuma ya Al Ahly iliyofanya hivyo mara 11, pia imebeba Kombe la Shirikisho Afrika mara mbili mfululizo mwaka 2016 na 2017.

Mazembe imekuwa ikishiriki mara kwa mara kwenye michuano ya CAF na kuwa miongoni mwa timu zenye heshima kubwa katika michuano hiyo.

Msimu uliopita Ligi ya DR Congo haikumalizika kutokana na machafuko ya kisiasa na vita lakini msimu huu hadi sasa Mazembe imecheza jumla ya mechi nne za ligi ikishinda zote na kuongoza ikiwa na alama 12.

Mazembe pia tayari imetinga makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa msimu huu baada ya kuifunga Nyassa Big Bullets ya Malawi kwa jumla ya mabao 5-0, na imepangwa kundi A sambamba na Mamelodi Sundowns, FC Nouadhibou na Pyramids.

ESPERANCE

Timu hii ilianzishwa mwaka 1919 na rangi za jezi zake maalumu ni nyekundu na njano, ikiwa nyumbani kwenye mechi zake mara nyingi imekuwa ikitumia Uwanja wa Hammadi Agrebi wenye uwezo wa kuingiza mashabiki 60,000 kama ilivyo kwa Mkapa.

Esperance ni kati ya timu tishio Afrika ikiwa imetwaa taji la Ligi ya Mabingwa mara nne nyuma ya vigogo Ahly iliyofanya hivyo mara 11, ikifuatiwa na Mazembe na Zamalek zilizobeba mara tano kila moja.

Msimu uliopita ilimaliza nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Tunisia nyuma ya Etoile du Sahel lakini ndio mabingwa mara nyingi zaidi wa ligi hiyo ikiwa imetwaa taji hilo mara 32.

Msimu huu hadi sasa inaongoza ligi ikiwa imecheza mechi tano, kushinda nne na kutoa sare moja ikivuna alama 13.

Pia, msimu huu imekata tiketi ya kucheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikiitoa Douanes kwa jumla ya bao 1-0, na ipo Kundi C sambamba na Etoile du Sahel, Petro de Luanda na Al Hilal.

REKODI WALIPOKUTANA

Mazembe na Esperance zimekutana mara saba katika michuano tofauti na wakati tofauti ambapo Esperance inaonekana kuwa na rekodi tamu zaidi kwani imeshinda mara tatu na kutoa sare mara mbili huku Mazembe ikishinda mara mbili tu.

Hata hivyo, mwaka 2010 ulikuwa wa timu hizo kufumuana mabao mengi kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, ambapo Esparence ilianza Agosti 28 kwa kushinda 3-0 na Mazembe ikalipiza Oktoba 31 kwa kushinda 5-0. Hii ni mechi nyingine kali ambayo mashabiki wanatakiwa kwenda kuitazama Kwa Mkapa.

Chanzo: Mwanaspoti