Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

AFRICAN FOOTBALL LEAGUE: Ukimwaga ugali huku wanamwaga mboga

Kikosi Ahly.jpeg AFRICAN FOOTBALL LEAGUE: Ukimwaga ugali huku wanamwaga mboga

Fri, 20 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Simba wanaliamsha dhidi ya Al Ahly katika mechi ya ufunguzi wa michuano mipya ya African Football League leo, lakini unaambiwa utamu hauishii hapa, kuna kitimtim kingine huko Angola ambako kesho Jumamosi wenyeji Petro Atletico de Luanda watawaalika wababe wa Afrika Kusini, Mamelodi Sundowns kupigania nafasi ya kutinga hatua ya nusu fainali.

Mbabe wa jumla katika mchezo huo ambao utaenda kumaliziwa kule Kwa Madiba Afrika Kusini, atakutana na mshindi wa jumla kati ya Simba na Al Ahly ambazo zinafungua pazia la michuano hiyo mipya leo pale kwa Kwa Mkapa.

Hii itakuwa mara ya saba kwa wababe hawa kukutana kwenye michuano ya kimataifa huku kila ubande ukivimbia ubora wa kikosi chake, rekodi zinaonyesha hakuna mnyonge kwa mwenzake kati ya Petro de Luanda na Mamelodi Sundowns.

Kwanini? Petro de Luanda na Mamelodi Sundowns wamekutana mara sita kwenye michuano ya kimataifa ambayo ni Ligi ya Mabingwa Afrika kila mmoja amemfunga mwenzake mara mbili na kutoka sare mbili na kila mmoja amekuwa akitamba nyumbani.

Mara yao ya kwanza kukutana ilikuwa 2001 tena katika hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza Mamelodi ikiwa nyumbani iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 lakini ilipoenda Angola ikatandikwa kwa mabao 2-1 lakini ilitinga hatua ya fainali kwa ushindi wa jumla wa mabao 3-2.

Msimu wa 2019/20 walipangwa kundi moja la C na walipokutana Mamelodi Sundowns ilishinda mchezo wa kwanza ikiwa nyumbani huku mwingine wakitoka sare ya mabao 2-2 na kutinga hatua ya mtoano sambamba na Wydad Casablanca.

Awamu ambayo walikutana tena ni msimu wa 2021/22 katika hatua ya robo fainali, ndipo Mamelodi ilipokutana na wakati mgumu, katika mchezo wa kwanza Petro de Luanda ilikuwa nyumbani ilishinda kwa mabao 2-1 na zilipoenda Afrika Kusini zikatoka sare ya bao 1-1 hivyo Atletico ilitinga nusu fainali kwa ushindi wa jumla wa mabao 3-2 na kulipiza kile ambacho kilitokea msimu wa 2001 ambapo walikutana kwa mara ya kwanza.

Nani ataandika rekodi mpya ya kutoa mwenzake kwenye African Footaball League na kutinga hatua ya nusu fainali? Ni jambo la kusubiri na kushuhudia lakini hizi ni dondoo muhimu kuhusu klabu hizi mbili ambazo zimekuwa tishio kuanzia kwenye ligi zao za ndani hadi upande wa Kombe la Shirikisho na Ligi ya Mabingwa Afrika.

PETRO ATLETICO LUANDA

Hii ni klabu ya soka kutoka Luanda, Angola, iliyoanzishwa mwaka wa 1980. Klabu hii ilishinda taji lake la kwanza, Ligi ya Angola 1982 na ndio timu yenye mafanikio zaidi nchini humo.

Katika siku zake za awali, klabu hiyo ilijulikana kama Petroclube.

Wachezaji wanne kutoka Petro Atletico waliiwakilisha Angola katika Kombe lao la kwanza la Dunia mwaka 2006 ambao ni Lebo Lebo, Lama, Ze Kalanga na Delgado.

Klabu hiyo pia ina timu ya mpira wa kikapu. Wachezaji wengi wa mpira wa kikapu wa timu hiyo, walishiriki na timu ya taifa ya mpira wa kikapu ya Angola katika Olimpiki ya 2008.

Licha ya kuwa tishio kwenye soka la Afrika, Petro de Luanda bado haijatwaa ubingwa wowote wa kimataifa, mafanikio yao makubwa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika waliyapata katika misimu ya 2001 na 2021-22 kwa kufika katika hatua ya nusu fainali.

Upande wa Kombe la Shirikisho mafanikio yao makubwa ni kufika hatua ya 16 bora ila wababe hao wa Luanda ni wanafainali wa Kombe la CAF mwaka 1997.

MAMELODI SUNDOWNS

Klabu ya soka ya Mamelodi Sundowns (inayojulikana kwa urahisi kama Sundowns) makao yake makuu ni Pretoria katika jimbo la Gauteng. Ilianzishwa katika miaka ya 1970, timu hiyo inacheza michezo yake ya nyumbani katika Uwanja wa Loftus Versfeld.

Sundowns wameshinda taji la Ligi Kuu Afrika Kusini mara 13 tangu kuanzishwa kwake 1996. Kwa sasa ndiyo klabu yenye mafanikio makubwa zaidi katika historia ya ligi ya Afrika Kusini. Walishinda Ligi ya Mabingwa Afrika 2016, CAF Super Cup 2017 na walichaguliwa kuwa Klabu Bora ya CAF ya 2016.

Katika ligi yao ya ndani, pia wameshinda Kombe la Nedbank mara sita, MTN 8 mara nne na Telkom Knockout mara nne. Ni timu ya kwanza ya Afrika Kusini kushindana katika Kombe la Dunia la Klabu la FIFA, ambapo walimaliza katika nafasi ya sita.

Sundowns inamilikiwa na mfanyabiashara mkubwa wa Afrika Kusini, Patrice Motsepe ambaye pia ni Rais wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), na ni mojawapo ya klabu zenye thamani zaidi barani Afrika.

Klabu hiyo inajivunia mtindo wake wa kipekee wa uchezaji wa kushambulia, unaojulikana kama “Shoe Shine & Piano” ambao unajumuisha mchanganyiko wa pasi za haraka na fupi za chini na hii inafananishwa na tiki-taka ya Uhispania.

Kwa miaka mingi, mtindo huu wa uchezaji umeonyeshwa katika timu zake za vijana na timu ya mpira wa miguu ya wanawake. Mwaka 2021, Sundowns ilikuwa klabu ya kwanza barani Afrika kushinda mataji ya Ligi ya Mabingwa ya CAF na Ligi ya Mabingwa ya Wanawake ya CAF.

Chanzo: Mwanaspoti