Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

AFL pamoto wikiendi hii...

AFL AFL pamoto wikiendi hii...

Sat, 21 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Usiku wa kuamkia leo Afrika na Dunia ilikuwa kwenye Uwanja wa Mkapa kushuhudia Simba ikikiwasha na Al Ahly katika ufunguzi wa michuano ya Africa Football League (AFL).

Mechi ya jana imeacha mitihani kadhaa kwenye michezo ya leo na kesho. Kwanza, nyomi la mashabiki. Pili, kiwango cha soka lililopigwa. Tatu, hamasa na maandalizi yalivyofanikiwa.

PETRO VS MAMELODI

Leo shoo ni moja tu, pale Angola wenyeji, Petro Atletico wanakiwasha na Mamelodi Sundowns. Baada ya Mamelodi kutishia kujitoa kwa wiki kadhaa kutokana na kubanwa na ratiba, leo wako saiti dhidi ya matajiri wenzao kuanza safari ya kusaka 10 bilioni.

Itakuwa mara ya saba kwa wababe hawa kukutana kwenye michuano ya kimataifa, rekodi zinaonyesha hakuna mnyonge kwa mwenzake kati ya Petro de Luanda na Mamelodi Sundowns.

Kila mmoja amemfunga mwenzake mara mbili na kutoka sare mbili na kila mmoja amekuwa akitamba nyumbani kwake.

Mara ya kwanza kukutana ilikuwa 2001 tena katika hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza Mamelodi ikiwa nyumbani iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 lakini ilipokwenda Angola ikatandikwa 2-1 lakini ilitinga hatua ya fainali kwa ushindi wa jumla wa mabao 3-2.

Msimu wa 2019/20, zilipangwa kundi moja (C), zilipokutana Mamelodi ilishinda mchezo wa kwanza ikiwa nyumbani huku mwingine zikitoka sare ya mabao 2-2 na kutinga hatua ya mtoano sambamba na Wydad Casablanca.

Msimu wa 2021/22, katika hatua ya robo fainali, ndipo Mamelodi ilipokutana na wakati mgumu, katika mchezo wa kwanza Petro de Luanda ilikuwa nyumbani ilishinda kwa mabao 2-1 ilipokwenda Afrika Kusini ikatoka sare ya bao 1-1, hivyo ilitinga nusu fainali kwa ushindi wa jumla wa mabao 3-2 na kulipiza kile ambacho kilitokea msimu wa 2001 ambapo zilipokutana kwa mara ya kwanza.

Licha ya kuwa tishio kwenye soka la Afrika, Petro de Luanda bado haijatwaa ubingwa wowote wa kimataifa, mafanikio makubwa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika iliyapata katika misimu ya 2001 na 2021, 22 kwa kufika nusu fainali. Kwenye Shirikisho ilifika hatua ya 16 bora ila ni ilifika fainali Kombe la CAF mwaka 1997.

Mamelodi imeshinda Ligi ya Mabingwa Afrika 2016, 2017 CAF Super Cup na ilichaguliwa kuwa Klabu Bora ya CAF ya 2016, imeingia kwa kujishauri kwenye mashindano haya kutokana na ishu za ratiba.

Ni timu ya kwanza ya Afrika Kusini kuwania Kombe la Dunia la Klabu la Fifa, ambapo ilimaliza katika nafasi ya sita. Itakuwa mechi ya kibabe sana leo ingawa hamasa ya mashabiki inaonekana si kubwa Angola kama ilivyokuwa kwa Simba jana ambapo mashabiki walifunika haswa.

MAZEMBE VS ESPERANCE

Ni kesho Kwa Mkapa. Mchezo huo umehamishiwa uwanjanai hapo baada ya kile kinachoelezwa kutofautiana kati ya mamlaka za DR Congo na CAF.

Mazembe kwa Afrika ni timu tishio kwani imetwaa Ligi ya Mabingwa Afrika mara tano nyuma ya Al Ahly iliyofanya hivyo mara 11, pia imebeba Kombe la Shirikisho Afrika mara mbili mfululizo mwaka 2016 na 2017.

Mazembe imekuwa ikishiriki mara kwa mara kwenye michuano ya CAF na kuwa miongoni mwa timu zenye heshima kubwa katika michuano hiyo.

Mazembe tayari imetinga makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa msimu huu baada ya kuifunga Nyassa Big Bullets ya Malawi. Jopo lake lote chini ya tajiri Moise Katumbi lipo Dar es Salaam na mashabiki wao baadhi.

Wageni wao wametwaa taji la Ligi ya Mabingwa mara nne. Hadi sasa wanaongoza ligi ya Tunis wakiwa wamecheza mechi tano, kushinda nne na kutoa sare moja wakivuna alama 13.

Esperance ipo kwenye makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikiitoa Douanes. Mazembe na Esperance zimekutana mara saba katika michuano tofauti na wakati tofauti na Esperance inaonekana kuwa na rekodi tamu zaidi kwani imeshinda mara tatu na kutoa sare mara mbili huku Mazembe ikishinda mara mbili tu.

Hata hivyo, mwaka 2010 ulikuwa wa timu hizo kufumuana mabao mengi kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, ambapo Esparence ilianza Agosti 28 kwa kushinda 3-0 na Mazembe ikalipiza Oktoba 31 kwa kushinda 5-0. Hii ni mechi nyingine kali ambayo mashabiki wanatakiwa kwenda kuitazama kwa Mkapa kesho Jumapili.

ENYIMBA VS WYADAD

Pale Nigeria kinawaka kesho. Zimekutana mara moja tu kwenye historia ya michuano ya kimataifa nayo ilikuwa Ligi ya Mabingwa mwaka 2011 kwenye hatua ya nusu fainali ambapo mchezo wa kwanza pale Nigeria ulikuwa suluhu mkondo wa pili kule Morocco, Wydad ikashinda bao 1-0 na kutinga fainali ambapo ilipoteza mbele ya Esperance.

Enyimba inanolewa na Finidi Goerge ambaye ni mchezaji wa zamani wa Nigeria pia amewahi kucheza timu kubwa Ulaya kama Ajax na Real Betis. Wydad ina Adil Ramz, raia wa Uholanzi ambaye amewahi kufundisha timu za vijana za PSV.

Ukiondoa ubabe wake kwenye ligi ya ndani, Enyimba msimu huu imetolewa na Al Ahly Benghazi, huko nyuma ilishiriki mara nane kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.

Imechukua ubingwa mara mbili mwaka 2003 ambapo ilicheza fainali dhidi ya Ismailia ya Misri, mchezo wa kwanza pale Enyimba International Stadium iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 na fainali ya pili pale Misri ikafungwa bao 1-0.

Ilichukua tena ubingwa wa pili mfululizo mwaka 2004 na wakati huu ilikutana na Etoile du Sahel ambapo kwenye mchezo wa kwanza pale Nigeria ilishinda mabao 2-1 na marudiano kule Tunisia ikafungwa mabao 2-1. Baada ya hapo ikaenda kuchukua ubingwa kwa penalti ikipata penalti 5-3. Kipindi hiki wamoto kwelikweli.

Mbali ya kuchukua ubingwa Enyimba imetinga hatua ya makundi mara tatu mwaka 2006, 2006 na 2016, pia imecheza nusu fainali mbili mwaka 2008 na 2011.

Kwenye Kombe la Shirikisho imeshiriki mara nne na mafanikio makubwa iliyoyapata huko ni kucheza nusu fainali mara moja mwaka 2018 sambamba na robo fainali mara mbili mwaka 2020 na 2021. Mara moja iliishia hatua ya 16 bora ambayo ni mwaka 2010. Enyimba pia ina makombe mawili ya CAF Super Cup 2004 na 2005.

Lakini Wydad ndio timu inayoongoza kupata mafanikio zaidi ndani ya Morocco ikiwa imechukua jumla ya mataji 22 ya Ligi Kuu. Kimataifa imetwaa Ligi ya Mabingwa mara tatu katika misimu 16 iliyoshiriki.

Pia, imecheza nusu fainali mara tatu, fainali tatu ambazo ilipoteza na imewahi kupoteza robo fainali mara mbili.

Kwenye Kombe la Shirikisho imeshiriki mara nne na mafanikio makubwa iliyopata huko ni kufika hatua ya makundi mwaka 2012, imewahi kuchukua Caf Super Cup mara moja kati ya nne ilizocheza.

Chanzo: Mwanaspoti