Wiki kadhaa zilizopita Tanzania ilipata heshima kubwa ya kuwa wafunguzi wa mashindano makubwa na tajiri zaidi ya vilabu bora barani Afrika (AFL) huku mchezo wa ufunguzi ukiwakutanisha miamba ya soka barani Afrika Simba SC and Al Ahly.
Likiwa ni tukio la kihistoria kuwahi kufanyika katika ardhi ya Tanzania na kuhudhuriwa na viongozi wakubwa wa soka Afrika na duniani ikiwamo; Rais wa Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF), Patrice Motsepe, Rais wa Shirikisho la Soka duniani (FIFA), Gianni Infantino, Rais wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Wallace Karia, marais wa mashirikisho mengine, viongozi waandamizi wa FIFA na CAF, Tanzania ilitia fora katika maandalizi yake kutokana na burudani zilizopamba hafla hiyo.
Mamia kwa maelfu ya wapenda soka duniani walifuatilia tukio hilo kwa njia mbalimbali na kujionea namna Tanzania ilivyopiga hatua katika maandalizi ya ufunguzi wa mashindano hayo, ikihitimishwa na soka la viwango vya juu lilionyeshwa na klabu ya Simba, iliyokuwa ikiwakilisha ukanda wa CECAFA, kwa kwenda sare ya 2-2 na mabingwa wa kihistoria wa michuano ya CAF, National Al Ahly.
Lakini nikuambie kuwa hiyo haikuwa historia pekee iliyoandikwa usiku ule. Kutokana na maboresho ya uwanja wa Benjamin Mkapa yaliyofanyika kwa maagizo ya CAF ili kupata kibali cha ufunguzi wa tukio hilo, ambapo miongoni mwa maboresho hayo, kulifungwa mabango ya matangazo ya LED ya kisasa zaidi. Mabango hayo, kwa mara ya kwanza, yalitufundisha namna ya kutoa thamani inayoendana na fedha kwa wadhamini mbalimbali wa mchezo wa soka, jambo ambalo halikuwa likifanyika kwa viwango vinavyotakiwa.
Achilia mbali mabango, uliona kuanzia nje ya uwanja, nembo na michoro ya mashindano na wadhamini wake wakuu walikuwa wakitapakaa katika kuta na sehemu za miundombinu ya uwanja huo. Walipata thamani yao halisi kabla ya mchezo, wakati wa mchezo na baada ya mchezo.
Baada ya AFL kuisha, Ligi Kuu ilirejea na, SportPesa, moja ya mdhamini mkuu wa vilabu vya soka hapa nchini, ilionja ladha ya kuwekwa katika mabango hayo wakati wa mchezo baina ya Yanga na Singida FG. Kila kitu ambacho SportPesa ingetamani kionekane na macho ya wapenda soka, kilitokea kwa ubora na hiyo ndiyo maana ya kuthaminisha wale wanaowekeza katika soka.
Viwanja vyetu vinahitaji usasa kama huu ili wadhamini kama SportPesa waendelee kufurahia uwekezaji wao katika vilabu na ligi yetu ambayo sasa inatazamwa kila kona ya dunia. Hii ndiyo njia mojawapo ya kuendelea kuwabakisha wadhamini katika soka na kuvutia wadhamini wapya kutokana na kile wanachokipata katika udhamini wao.