Wakati fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2023 zitakazofanyikia Ivory Coast zikiwa zimesaliwa na wiki mbili kabla ya kuanza kwake, nyota wanane wa kigeni wanaocheza Ligi Kuu Bara wameitwa kwenye vikosi vya awali vya nchi zao zitakazoshiriki fainali hizo zitakazoanza Januari 13 mwakani ikishirikisha nchi 24.
Shirikisho la Soka Afrika (CAF) liliachia hadharani vikosi vya awali za timu hizo shiriki ikiwamo Tanzania itakayoshiriki kwa mara ya tatu baada ya ya fainali za 1980 na 2019, huku nyota hao wanane wanaokiwasha Bara majina yao yaking'ara kwa kuitwa kwa ajili ya mazoezi kabla ya kupitishwa mchujo wa mwisho.
Nyota hao wanane wa kigeni walioitwa kwenye timu hizo wanatokea vigogo watatu wa Ligi Kuu, Simba, Azam Fc na Yanga iliyotoa watano ikiwa ndio kinara.
Wachezaji hao wa Yanga ni washambuliaji Hafiz Konkoni aliyeitwa na Ghana na Kennedy Musonda (Zambia), viungo washambuliaji Pacome Zouzoua (Ivory Coast) na Stephane Aziz KI (Burkina Faso) pamoja na kipa Djigui Diarra (Mali).
Wengine ni kiungo mshambuliaji wa Simba, Luis Jose Miquissone aliyeitwa timu ya taifa ya Msumbiji na beki Henock Inonga , pia wa Simba aliyejumuishwa Dr Congo pamoja na beki wa Azam, Cheikh Sidibe aliyeitwa timu ya taifa na watetezi wa michuano hiyo ya Afcon, Senegal.
Wenyeji Ivory Coast imetenga viwanja sita tofauti vitakavyotumika kwenye fainali hizo za 34 ambavyo ni Alassane Ouattara, uliopo Abidjan unaobeba mashabiki 60,000, Felix Houphouet-Boigny uliopo Abidjan wenye uwezo wa kubeba mashabiki 33,000.
Uwanja mwingine ni Charles Konan Banny, uliopo mjini wa Yamoussoukro unaobeba mashabiki 20,000,Stade de la Paix, uliopo Bouake unaobeba mashabiki 40,000, Amadou Gon Coulibaly, uliopo Korhogo wenye uwezo wa kuingiza mashabiki 20,000 na ule wa Laurent Pokou, uliopo San Pedro unaingiza pia mashabiki 20,000.