Kufuatia taarifa ya Bodi ya Ligi juu ya maboresho ya kanuni ambapo imeweka marufuku kwa mchezaji kuingia mkataba binafsi wa udhamini na mshindani kibiashara wa mdhamini mkuu wa Ligi, Chama cha ACT Wazalendo kimeshangazwa sana kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF) kupitia Bodi ya Ligi kwa kukubali kuingiza masharti haya katika wakati ambao nchi inapambana kuona michezo inaenda kuinua maisha ya vijana wengi kwa kutoa ajira na kukuza maslahi ya wachezaji.
Aidha ACT Wazalendo kupitia kwa Kamati ya Kuisimamia Serikali ya Wasemaji wa Kisekta (Baraza Kivuli la Mawaziri) imesema “tunaungana” na wadau wengine kupinga maboresho hayo ya kanuni kwasababu zifuatazo:-
-Kanuni hii inawanyima wachezaji uhuru na haki binafsi katika kujitafutia kipato. Mchezaji ni raia wa kawaida anayeweza kushiriki kwenye matangazo binafsi na kampuni au taasisi yoyote ambayo haikiuki haki za kipekee (exclusive rights) za Mdhamini Mkuu wa Ligi.
-TFF katika kununi ya 16 (1.4, 5,6) imeweka makatazo na utaratibu wa matangazo yasiyokuwa ya Mdhimini Mkuu ambapo vifungu vyote vimezuia maeneo ya uwanja pamoja na matumizi ya nembo ya mdhamini Mkuu kwenye vifaa vya kuchezea vya timu husika.
Ni wazi kwamba haki zote kwa mdhamini mkuu zimeorodheshwa kuongeza kifungu hiki ni kukandamiza maslahi ya wachezaji.
-Maboresho ya kanuni hayajatoa tafsiri ya shughuli zitakazo chukuliwa kuwa ni kuingiliana na zile za Mdhamini Mkuu wa Ligi Kuu. Hii inaweza kutoa tafsiri tofauti tofauti au inaweza kutumika vibaya kuzuia matangazo kwa wachezaji.
-Kanuni imekuja bila kuchukua uzoefu kutoka maeneo mbalimbali duniani katika kusimamia haki na maslahi ya wachezaji linapoja suala la udhamini.
Uzoefu wa wachezaji wakubwa Duniani wamekuwa wakiingia mikataba binafsi na kampuni tofauti tofauti ambazo zinamgongano wa kimaslahi wa karibu. Mdhamani Mkuu hawezi kupewa haki ya Uhodhi hata kwa maisha ya wachezaji. Hii haikubaliki.
Hivyo basi, ACT Wazalendo kupitia kwa Msemaji wa Sekta ya Utamaduni, Sanaa na Michezo tunaitaka TFF na Bodi ya Ligi kuondoa marekebisho haya mapya ili kulinda maslahi ya wachezaji.
Pili, tunaitaka kuwepo kwa ushirikishaji katika masuala yote ya michezo yanayohusu pande mbalimbali.