Mabingwa wa Soka nchini Italia AC Milan wanaripotiwa kumfuatilia beki wa kulia wa Mabingwa wa Soka nchini England Manchester City, Kyle Walker ili wamsajili wakati wa usajili wa majira ya kiangani (Mwishoni mwa msimu huu).
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 32, amebakiza mwaka mmoja kwenye mkataba wake Etihad na hadi sasa hakuna dalili zozote kwamba atasaini mkataba mpya wa kusalia klabuni hapo.
Miamba wa Serie A, Milan ambao wanaweza kukabiliana na City katika fainali ya Ligi ya Mabingwa mwezi Juni, watajaribu kumshawishi Walker kuhamia Italia.
Walker ametokea katika mechi 19 za ligi baada ya kuathiriwa na majeraha na kiwango duni msimu huu, huku meneja Pep Guardiola akidai kuwa hawezi kucheza nafasi anayodai.
Guardiola alifichua mapema mwezi huu kwamba Walker hawezi kufuata maelekezo ya kimbinu yanayohitajika ili kuchukua nafasi ya sasa ya John Stones.
Walker alijiunga na City kwa Pauni milioni 54 mwaka 2017 akitokea Spurs na amekuwa na mchango mkubwa katika mafanikio ya klabu hiyo tangu wakati huo, akicheza mechi 241 na kushinda mataji mengi yakiwemo mataji manne ya ligi kuu, mataji manne ya Kombe la Ligi na Kombe la FA.
Lakini hivi karibuni muda wake wa kucheza umekuwa mdogo hivi karibuni huku akitupwa benchi kwenye ushindi dhidi ya Liverpool mapema mwezi huu, aidha aliingia kama mchezaji wa akiba kwenye ushindi dhidi ya Crystal Palace wiki iliyopita.