Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

ABDOUN: Maufundi yake yamdatisha Mturuki

Abdoun Pic Maufundi yake yamdatisha Mturuki

Tue, 13 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Neema yanukia! Kocha wa Boluspor Kulubu inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza Uturuki ‘TFF First League’, Sait Karafirtinalar ametoa mwaliko wa mwezi mmoja kwa kinda la Kitanzania, Abdoul Ibrahim Salum ili kupata zaidi nafasi ya kumtazama baada ya kuvutiwa na uwezo wake siku chache zilizopita.

Maskauti wa chama hilo ambalo limewahi kushiriki Europa Ligi kipindi hicho ikiitwa UEFA Cup msimu wa 1974ñ75, walilipeleka faili la kinda huyo kwa kocha huyo ili kufanya maamuzi ya mwisho baada ya kuvutiwa naye.

Wiki chache nyuma, mwakilishi kutoka Uturuki alikuwa nchini kwa kushirikiana na taasisi ya African Youth Empowerment (AYE) na walifanya ziara ya kutembelea maeneo mbalimbali na kutoa fursa kwa vijana wenye vipaji vya kucheza soka kwa lengo la kuwaendeleza.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Uturuki, Kocha wa Boluspor Kulubu amekunwa na uwezo wa kijana huyo ambaye alirekodiwa video wakati wa mchakato huo na mwakilishi ambaye alikuwa nchini kwa zoezi hilo hivyo ameagiza aletewe amtazame zaidi.

Makamu wa rais wa klabu hiyo, Mr Mahmut Cimender ametuthibitishia hilo kwa kusema Abdoul atakuwa nchini humo kwa mwezi mmoja na kama atamshawishi zaidi kocha wa kikosi chao basi anaweza kusajiliwa moja kwa moja hivyo anatakiwa kuondoka na kila kitu chake kwani anaweza kuingizwa kwenye programu za timu.

Hakuishia hapo, alitutumia barua ya mwaliko huo ambayo imesainiwa naye ikieleza, “Sisi Klabu ya Boluspor nchini Uturuki tunavutiwa na mchezaji bwana ABDOUN IBRAHIM SALUM mwenye hati ya kusafiria ya Tanzania (tumehifadhi) na tunamkaribisha ajiunge na klabu yetu kwa majaribio ya mwezi mmoja.....,”

Ndani ya wiki hii, Abdoun atatakiwa kuwa Uturuki na mara moja kuanza programu za timu hiyo huku akifuatiliwa kwa karibu na kocha huyo. Huyu atakuwa mchezaji wa nne wa kwanza ni Ramadhan Makame (Hatayspor), Athuman na Shaffih Omary ambaye tulikuwa naye kwenye safu hii huku tukiripoti alivyotambulishwa na Tuzlasp.

Akiongelea safari ya Abdoun, Mkurugenzi Mtendaji wa AYE, Muyimba Gerald anasema kila kitu kimekamilika, kilichobaki ni upande tu wa mchezaji kwenda kumshawishi kocha huyo ambaye ameonekana kuvutiwa naye kwao ni faraja kuona mchezaji akaipiga hatua.

“Abdoun amekuwa na subira maana ukiangalia mchakato ulichukua muda lakini kwa sasa hakuna tena kusubiri, anaondoka kwa kwenda Uturuki ambao tunaamini utakuwa mwanzo wake wa safari ya kufika mbali zaidi, uzoefu ambao ataupata hapo utamsaidia baadae kumwona katika klabu nyingine kubwa,” anasema.

“Huu ni mwendelezo kwetu wa kuendelea kupigania ndoto za vijana wa Kitanzania, tunajua changamoto huwa haziwezi kukosekana, kwetu huwa tunazichukulia kama fursa tu na wala haziwezi kuturudisha nyuma.”

“Wapo watu ambao wamekuwa wakitaka kuturudisha nyuma lakini tupo imara na tutaendelea kufanikisha hili kwa masilahi mapana ya vijana na taifa kwa jumla, tumekuwa na ushirikiano wa karibu na Wizara ya Michezo, Shirikisho la Soka nchini na hata wadau mbalimbali ambao tumekuwa karibu nao.”

Wiki iliyopita wakati tukimhoji kuhusu Shaffih, Muyimba alisema kuhusu mchakato mwingine wa kutafuta wachezaji wengine kwa ajili ya kuwapeleka Ulaya, utakuwa mwakani na sehemu watazitangaza hapo baadae lakini itakuwa Bara na Visiwani.

“Hata kama watapatikana vijana 50 au 100 nafasi zipo nyingi maana mtandao wetu Ulaya ni mkubwa tunashirikiana na zaidi ya timu 100 barani humo kikubwa wawe vijana wenye vipaji kwelikweli, hatuna upendeleo kwa yeyote,” anasema.

Hii itakuwa mara ya kwanza kwa Abdoun kupanda ndege hivyo shauku ni kubwa ndani yake kuona vile ambavyo safari itakuwa ya kwenda kupigania ndoto zake nchini humo ambako aliwahi kucheza nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta (Fenerbahce).

“Ninafuraha sana kupata nafasi hii ambayo ilikuwa kwenye ndoto yangu, naamini nitaitumia vizuri ili kutengeneza njia kwa wachezaji wengine,” anasema Abdoun.

Boluspor ni klabu ya soka ya Uturuki inayopatikana katika jiji la Bolu. Imekuwa ikicheza michezo yake ya ushindani ikiwa na jezi nyekundu na nyeupe na inafanya hivyo tangu ilipoanzishwa mwaka wa 1965.

Baadhi ya wachezaji wake mashuhuri walikuwa Lutfu Isigollu, Sinan Alayoglu, Sadullah Acele, Ridvan Dilmen, Sercan Gorgulu, Halil Ibrahim Eren, Recep Cetin, Ali Beykoz, Senol Fidan, Mufit Ikizogit na Faruk Yigitlu.

Ndani ya nchi, klabu hiyo imeshinda Ligi Dara la Kwanza ya TFF mara moja. Mafanikio yao makubwa zaidi katika soka ya daraja la juu yani Ligi Kuu Uturuki yalikuja mwaka wa 1974, walipomaliza katika nafasi ya tatu.

Klabu hiyo imeshiriki machuano mikubwa Ulaya mara moja tu, ikipoteza kwa Dinamo Bucharest, katika Kombe la UEFA 1974-75 ambalo sasa ni Europa Ligi.

Chanzo: Mwanaspoti