Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

A-Z Yanga walivyowazidi TP Mazembe kwa Musonda

Musonda Yanga Mdf.jpeg A-Z Yanga walivyowazidi TP Mazembe kwa Musonda

Tue, 17 Jan 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Yanga juzi usiku ilimtambulisha rasmi mshambuliaji mpya kutoka Zambia, Kennedy Musonda, lakini mwenyewe amefungua dili lake lilivyokuwa, huku akiwaahidi mashabiki wa klabu hiyo kwamba amekuja kupiga kazi na kuwataka wasubiri waone mambo uwanjani.

Akizungumza Musonda alifichua aliruhusiwa kuja kumalizana na Yanga kabla ya kutambulishwa na aliporudi Zambia alikutana na taarifa za kutakiwa kwenda Mazembe na kuchomoa kwani alishamalizana na Yanga ikiwamo utambulisho.

“Nilipomaliza kazi hiyo ya kupigwa picha nilirudi kesho yake Zambia, lakini nilikutana na kelele nyingi kumbe Mazembe walikuwa wameleta ofa kubwa zaidi ile ya Yanga wakitaka kunisajili,” alisimulia zaidi Musonda na kuongeza;

“Kama isingekuwa akili ya Rais nadhani mambo yangekuwa tofauti kwa sababu tayari tulishamaliza kila kitu, niliwamabia viongozi wa Dynamos hakuna kitakachobadilisha tena nimechagua kucheza Yanga hao Mazembe wawaambie nawashukuru tu. Mazembe walikuwa wameweka mezani kiasi cha dola 120000 (Sh 279.2 milioni) kuweza kununua mkataba wa mshambuliaji huyo aliyewaahidi wana Yanga mambo matamu zaidi atakapoanza kuitumikia timu hiyo.

“Nimefurahi kujiunga na Yanga lakini nimshukuru zaidi Rais wa Yanga kwa jinsi alivyonipa heshima kwa kunifuata na hata jinsi alivyopambana kuhakikisha usajili huu unakamilika, sasa naangalia mbele kupata mafanikio zaidi nikiwa na Yanga,” alisema Musonda aliyeondoka Dynamos akiwa kinara wa mabao wa Ligi Kuu Zambia, akifunga mabao 11.

Dili kama filamu

Yanga ambayo mwezi ujao itakutana na Mazembe katika mechi za makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, walijua mawindo ya Wakongomani hao juu ya Musonda na haraka hesabu zikaanza.

Dili hilo lilianzia katika mtandao wa kijamii wa Instagram ambapo mshambuliaji huyo wakati Yanga inamsaka kumbe aliwahi kumtumia ujumbe wa kuvutiwa na Yanga kwenye akaunti ya Rais wa Yanga Injinia Hersi Said.

Wakati Hersi akimfuata Musonda kuongea naye kuangalia utayari wake, alikutana na wepesi kufuatia mchezaji huyo kumwambia anamjua na anaijua vyema Yanga.

Hatua hiyo ilimpa wakati mzuri Hersi kufikia makubaliano na mshambuliaji huyo aliyekuwa kinara wa mabao katika ligi ya Zambia akifunga mabao 11 kabla ya kutua Jangwani.

Hersi baada ya kumaliza kazi kwa Musonda aliomba nafasi ya kuonana na uongozi wa Power Dynamos katika kujua uwezekano wa kumuachia mchezaji huyo kujiunga na wananchi.

Licha ya Dynamos kuweka ngumu katika kumuachia Musonda wakieleza kuwa mshambuliaji huyo ndiye staa wao wanayemtegemea katika kumaliza ukame wa mataji wakiutaka ubingwa wa Zambia msimu huu.

Hata hivyo Hersi aliwashika pabaya mabosi wa Dynamos baada ya kuafikiana kuvunja mkataba wa mchezaji huyo kufuatia kifungu kilichopo kwenye mkataba wa mchezaji huyo kisha kuruhusiwa kuzungumza na mchezaji huyo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live