Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

150 kuliamsha NBC Waitara Trophy

Kinana Golf 150 kuliamsha NBC Waitara Trophy

Sat, 27 Jan 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Achana na hatua ya 16 Bora ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2023 inayoanza leo usiku kule Ivory Coast, jijini Dar es Salaam kwenye viwanja vya Lugalo kuna uhondo wa mashindano ya mchezo wa Gofu ya NBC Waitara Trophy yatakayoshirikisha zaidi ya washiriki 150.

Unaambiwa milango ya viwanja hivyo itakuwa wazi kuanzia saa 1:00 asubuhi na kitu cha kuzingatia kwa mashabiki ni mchezo huo hautaki kelele, kwa vile kuna aina ya ushangiliaji utakaowapa burudani zaidi, huku wale wanaopenda kujifunza mchezo huo watakutana na bahati na kuifurahia wikiendi yao.

Kwa mashabiki watakaothubutu kwenda kwenye viwanja hivyo vya jeshini, watakutana na bahati kama aliyosema meneja wa Klabu ya Gofu ya Lugalo, Kanali David Erick Mziray aliyesema watatoa mafunzo ya gofu kwa wanaotaka kujifunza.

Mzuka wa Gofu kupitia Mwanaspoti, limefanya mahojiano na Meja Japhet Brown Masai, ambaye ni nahodha wa klabu hiyo ya Lugalo, anazungumzia mashindano hayo na kusema;

“Mashindano hayo yanafanyika kila mwaka tangu yalipoanzishwa 2007, isipokuwa mwaka jana yalishindikana na siwezi kutaja sababu,” alisema Meja Masai na kueleza makadirio yao ni kupata wachezaji 150 na mwisho wa kujiandikisha ilikuwa juzi Alhamisi saa 12:00 jioni kwa ada ya ushiriki ikiwa Sh20,000.

“Tumetoa mwaliko kwa klabu za ndani na nje, pia mwaka huu tumeboresha watashiriki na wanawake na junior, zawadi zipo tayari ila hatuwezi kutaja ni nini wataziona pale pale,” alisema Meja Masaio na kuongeza’

“Mashindano hayo yatafanyika siku moja, zawadi itatolewa kwa mshindi wa jumla wa neti.”

Ushindi wa neti unatokana na jumla ya mikwaju ya makosa ya mchezaji anatoa na handcup zake.

Alisema kutokana na mvua zilizonyesha hivi karibuni, zinazosababisha baadhi ya sehemu za viwanja kuhitaji kufanya ukarabati, hilo wameishalifanyia kazi na kila kitu kipo sawa, “Kama nyasi zimeishakatwa, sehemu za maji yanatolewa na mashine, kilichobaki ni wachezaji kuingia uwanjani.”

BRIGEDIA JENERALI LUWONGO

Brigedia Jenerali mstaafu, Michael Luwongo, ambaye ni Mwenyekiti wa klabu ya Gofu ya Lugalo, alisema mchezo huo huo hauna umri anaweza akacheza mtu yoyote hadi mzee aliye na miaka 100.

“Kwa wiki nakuja kucheza mara tatu, kuna siku nacheza viwanja tisa wakati mwingine 18 ni mchezo unaonifanya nitembee kwa muda mrefu zaidi ya saa tatu, tofauti na mtu akiniambia nitembee nusu saa mtaani kwa ukweli siwezi,” alisema Brigedia Jenerali Luwongoanasema na kuongeza;

“Nawashauri wazee wenzangu waje wajifunze mchezo huo, utawasaidia kuwaweka fiti, kama ninavyojisikia mimi, nikicheza nakuwa vizuri zaidi. Kuna mashindano niliyaona mtandaoni yamechezwa Ulaya, mzee wa miaka 100 alifanya vizuri na huwezi kuamini kama ana umri huo, ilinifurahisha sana.”

Akizungumzia maandalizi ya mashindano ya NBC Waitara Trophy, anasema amejiandaa, ingawa Jumatano alifanya mazoezi kwa kucheza viwanja tisa, kutokana na kusumbuliwa na mguu.

“Nitaangalia siku mbili naamkaje, nikiwa sawa nitashiriki mashindano hayo, kwani ni mazuri na yanatukutanisha watu tofauti. Lakini amewapa ujumbe mzito vijana nchini, kutoogopa kuzungumza na mtu yeyote, pia wajaribu kufanya kazi zaidi ya moja, kuhakikisha wanajijenga kiuchumi.

“Vijana wana safari ndefu sana, wanahitaji kupambana sana, utafutaji wao usiwe wa njia moja, inapofeli wanakuwa wanatoka nje ya mstari, jambo la msingi zaidi wasiogope kumuuliza mtu yoyote wanayeona anastahili kuwapa jibu la maswali yao,” alisema Brigegia Jenerali Luwongo na kuongeza;

“Kupitia gofu, nimegundua akili kubwa ya vijana wengi tofauti na mwonekano, kubwa zaidi huku kuna upendo na mshikamano.”

Kwa upande wa bingwa mtetezi, Isihaka Daud alisema; “Division A zimetofautiana, wapo wanaoshinda kwa neti ambazo unatoa na handcup na wanaoshinda kwa grosi ambao unashinda kulingana na mipigo yako. Nitashiriki kwa kujifurahisha ila kategori yangu haipo, ila ni mazuri naona yanawapa nafasi sana watu wazima, hilo ni jambo linalowapa faraja zaidi.”

Kwa upande wa Kanali David Erick Mziray, alisema; “Nje na mashindano hayo, klabu ipo tayari kutoa mafunzo ya wanaohitaji kucheza gofu na tutawadhamini miezi miwili, baada ya hapo watajiunga na uanachama wa klabu yetu.

“Jambo lingine la msingi mgeni rasmi kwenye mashindano ya NBC Waitara Trophy ni Jenerali Mstaafu George Waitara ambaye ndiye tunayemuenzi kwenye mashindano hayo, kutokana na mchango wake mkubwa alioufanya Lugalo.”

Mkuu wa Kitengo cha Biashara kutoka NBC, David Raymond alisema; “Ni waumini wa kusapoti michezo ndio maana tunasapoti gofu, hivyo tunahamasisha watu kuja kucheza gofu ni mchezo wenye fursa nyingi.”

Chanzo: Mwanaspoti