Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waziri Mkuu mgeni rasmi Baraza la Eid, Sheikh Alhad atoa neno

61098 Pic+majaliwa

Mon, 3 Jun 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wakati Waislamu wakiwa ukingoni mwa mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, imeelezwa baraza la Eid el Fitr litafanyika kwenye hoteli ya Tanga Beach Resort mkoani Tanga ambapo mgeni rasmi atakuwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimuwakilisha Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu Juni 3, 2019, Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam ambaye pia ni katibu wa kamati ya mwandamo wa mwezi taifa, Alhad Salum amesema kabla ya Baraza la Idd, swala ya Idd kitaifa itaswaliwa mkoani humo na itaongozwa na Mufti wa Tanzania, Abubakar Zubeir.

Amesema swala hiyo itaswaliwa kwenye viwanja vya Ngamiani mkoani humo.

"Waumini wajitokeze kwa wingi, wanawake pia kwa sababu swala ya uwanjani itawapa fursa wote kuswali wale waliokuwa na udhuru zao," amesema Alhad Salum.

Salum amefafanua kuwa kwa mkoa wa Dar es Salaam swala hiyo itaongozwa na Alhaj Ally Hassan Mwinyi (Rais wa awamu ya pili) na itaswaliwa kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja.

Salum pia alitumia mkutano huo kutoa nasaha kwa waumini kuadhimisha siku hiyo kwa kufuata maelekezo ya Mtume Muhammad (SAW) na si vinginevyo.

Pia Soma

"Imeelezwa kuwa atakayefanya maasi siku hiyo dhambi zake zitakuwa sawa na  aliyemuasi Mwenyezi Mungu siku ya kiama.”

"Yaani watu wamesimama kwenye viwanja vya hukumu siku ya kiama, halafu wewe unatenda dhambi siku hiyo, ni hasara ya namna gani utakayopata, hivyo tuwe makini katika kuadhimisha siku hii," amesema Salum.

Amewaasa wazazi kuwapeleka watoto wao kwenye maeneo salama ambayo hayatahatarisha maisha yao.

"Wazazi tusiwaruhusu watoto wa kike na wa kiume waliobalehe  kutoka pamoja kwenda fukweni, kwa sababu kinachotokea huko ni laana, uharibifu na ukosefu wa maadili kwa mabinti ikiwamo kuambukizana ukimwi.”

"Nikiwa kama kamishna wa  Tacaids sifurahishwi siku hii njema iliyopewa maelekezo ya namna ya kuifurahia Mtume Muhammad (S.A.W), kutumika watu kuambukizana Ukimwi, naiomba Serikali kupitia Jeshi la Polisi kuzuia magari yaliyobeba mchanganyiko wa wasichana na wavulana  kwenye fukwe zisizokuwa na staha," amesema Salum.

Chanzo: mwananchi.co.tz