Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waziri Mkuu asisitiza kumuabudu Mungu si wakati wa Ramadhani pekee

9331 PM+PIC TZW

Sat, 16 Jun 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemuwakilisha Rais John  Magufuli kwenye Baraza la Idd el Fitri lililofanyika katika viwanja vya Mnazi mmoja jijini Dar es Salaam.

 Akizungumza kwa niaba ya Rais Magufuli leo Juni 15, Waziri Majaliwa amewaasa Waislamu na Watanzania wote kwa ujumla kuendelea kutenda mema baada ya kuwa wamejisahihisha na kutubu makosa yao ndani ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Waziri Mkuu amesema viongozi wanaendelea kuwasihi Waislamu wote na Watanzania kwa ujumla kuonyesha upendo, umoja na kuvumiliana  hasa baada ya kumalizika kwa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.

 “Huruma, ukarimu na ucha Mungu ulionyeshwa katika kipindi cha mfungo wa Ramadhani, uendelee na uwe sehemu ya maisha ya kila siku na kamwe usiwe umeisha baada ya mwandamo wa mwezi wa mfungo mosi,’’ amesema.

 

Waziri Mkuu ameongeza kuwa upendo, umoja, utulivu, mshikamano na subra ulioonyeshwa kipindi chote cha mfungo wa Ramadhani ni vyema ukaendelezwa kwa sababu ucha Mungu si katika mwezi huo pekee.

Magufuli ameniagiza kwa kusema : "Waislamu ni kielelezo cha taasisi za dini zinazozingatia maadili mema, hivyo wachache wasijipenyeze na kuharibu taswira yao. Ninawahakikishia kuwa Serikali iko tayari kushirikiana na taasisi yoyote ya dini ambayo itakuwa tayari kuzingatia matakwa ya Katiba, Sheria na taratibu tulizojiwekea nchini’’amesema

 

Awali, Sheikh Mkuu na Mufti wa Tanzania Sheikh Abubakar Zubeir alitoa wito kwa masheikh wa mikoa na wilaya zote nchini wahakikishe kila wanapofanya mikutano yao mada ya amani na kudumisha uzalendo zisikose kwa kuwa ni vitu muhimu.

 ”Kama mtu huna uzalendo hata dini inapungua, tujenge uzalendo kwa ajili ya kuienzi nchi na kuifanya iendelee kuwa kisiwa cha utulivu. Tuendelee kujenga umoja na mshikamano tusiliache suala hili kwa sababu ndilo liloijenga jamii yetu,’’ amesema.

Pia, Mufti Zubeir amesema ni vizuri kwa Waislamu kuunga mkono juhudi mbalimbali zinazofanywa na Serikali kwa ajili ya maendeleo ya Taifa na waache kuishi kwa mazoea.

 

 

Chanzo: mwananchi.co.tz