Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waziri Mkuu akomelea msumari alioupiga Magufuli

9333 Pic+waziri+mkuu TZW

Sat, 16 Jun 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesisitiza kile alichokisema Rais John Magufuli juzi, akiwataka viongozi wa dini wasiwatumie wanasiasa kuwasemea mambo yao.

Waziri Mkuu aliyasema hayo jana alipomwakilisha Rais Magufuli katika Baraza la Idd el Fitri lililofanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.

Mapema wiki hii, Rais Magufuli alitoa wito kwa viongozi wa dini kutowatumia wanasiasa kuwasemea mambo yao alipokuwa akikagua ujenzi wa msikiti unaojengwa makao makuu ya Baraza Kuu la Waislamu (Bakwata), unaofadhiliwa na Mfalme Mohamed VI wa Morocco.

Alichosema Waziri Mkuu

Akizungumza katika bara hilo, Waziri Mkuu, Majaliwa alisema, “Viongozi wa dini mnatakiwa kujadili masuala ya amani badala ya kuwatumia wanasiasa kuwazungumzia baadhi ya mambo yenu.”

“Baraza liangalie na kusimamia rasilimali zake. Nakumbuka wakati mufti anaingia madarakani aliunda kamati ya kuchunguza mali za Waislamu, ni vizuri mjue mali zetu, mjue thamani yake na kuchukua hatua.”

Majaliwa aliwataka viongozi wa dini katika baraza hilo kuangalia na kujadili misingi ya amani kwa sababu ni moja ya tunu ambazo Taifa linajivunia na kuwa mfano kwa mataifa mengine.

Pia alitoa wito kwa baraza hilo kuangalia namna ya kusimamia malezi ya vijana ili kulinda maadili na utamaduni wa Taifa.

Alilitaka baraza hilo kuweka misingi mizuri na Serikali kwa sababu inatambua uhuru wa kuabudu ipo kwa ajili yao.

Kadhalika, alilitaka baraza kujadili na kutoa miongozo katika uwekezaji kwenye miradi ya maendeleo hasa kilimo ambacho hakijapewa nafasi kubwa.

Majaliwa alisema Serikali inatambua mchango mkubwa wa maendeleo unaotolewa na taasisi za dini kwenye sekta za elimu, afya na maji.

“Sisi kama Serikali tunatambua mchango mkubwa ambao mnautoa kwenye maendeleo ya Taifa letu. Mmejenga shule nyingi, mmejenga vyuo vikuu, mnatoa huduma za maji na afya, endeleeni kushirikiana nasi katika shughuli za maendeleo,” alisema.

Waziri Mkuu aliwasihi Waislamu na Watanzania kwa ujumla kuonyesha upendo, umoja na kuvumiliana hasa baada ya kumalizika kwa Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Alisisitiza kuwa upendo, umoja, utulivu, mshikamano na subira vilivyoonyeshwa kipindi chote cha mfungo ni vyema ukaendelezwa kwa sababu ucha Mungu siyo katika mwezi huo pekee.

Bakwata yataka dini zijisimamie

Bakwata waliiomba Serikali iendelee kuacha masuala ya dini yasimamiwe na waumini wenyewe.

Naibu katibu mkuu utawala wa Bakwata, Sheikh Nuhu Jabir aliwasihi wale ambao siyo viongozi wa dini kuacha kusemea mambo ya dini katika vyombo vya kiserikali na kuwataka wanapotaka kuyazungumza ni vyema waende katika taasisi husika za kidini.

Alisema watakapokwenda katika taasisi husika watapata elimu na usahihi wa kile wanachotaka kukizungumzia kuliko kupotosha.

“Viongozi wa dini zote hubirini ucha Mungu, amani, malezi bora kwa vijana, kukemea maovu, mmomonyoko wa maadili na kutokubali kuchotwa fikra na wasiokuwa wana dini,” alisema Sheikh Jabir.

Sheikh Mkuu na Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir alitoa wito kwa masheikh wa mikoa na wilaya zote nchini wahakikishe kila wanapofanya mikutano yao mada ya amani na kudumisha uzalendo zisikosekane.

“Kama mtu huna uzalendo hata dini inapungua, tujenge uzalendo kwa ajili ya kuienzi nchi na kuifanya iendelee kuwa kisiwa cha utulivu. Tuendelee kujenga umoja na mshikamano, tusiliache suala hili kwa sababu ndilo lililoijenga jamii yetu,’’ alisema.

Mufti Zubeir aliwataka Waislamu kuunga mkono juhudi mbalimbali zinazofanywa na Serikali kwa ajili ya maendeleo ya Taifa na waache kuishi kwa mazoea.

Baraza hilo lilihudhuriwa pia na mchungaji Antony Lusekelo, Askofu Charles Gadi na katibu wa Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini ya Mkoa wa Dar es Salaam, Padri John Solomon.

Chanzo: mwananchi.co.tz