Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waziri Jafo awataka viongozi wa dini, Serikali kuwa waadilifu

28017 PIC+JAFO TanzaniaWeb

Tue, 20 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam.  Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- Tamisemi, Selemani Jafo amewataka viongozi wa dini na Serikali kuwa waadilifu ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi.

Mbali na uadilifu Jafo amewataka viongozi hao kudumisha amani ili kuepuka machafuko yanayosababishwa na kukosekana kwa amani.

Jafo alisema hayo leo wakati akihutubia mamia ya wananchi waliohudhuria Baraza la Maulid ikiwa ni kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (S.A.W) lililofanyika kitaifa Korogwe mkoani Tanga.

Waziri huyo aliyemwakilisha Rais John Magufuli alisema kingozi bila uadilifu hawezi kufanya kazi kwa ufanisi na atakuwa amekiuka taratibu na sheria za nchi.

“Lakini pia niwakumbushe tu kuwa kudumisha amani ambayo ndiyo msingi katika nchi yetu ni muhimu sana, tuangalie mataifa ya wenzetu ambayo hayana amani jinsi wanavyopata tabu, tujivunie na tuilinde amani tuliyonayo.”

“Leo hii tusingekutana hapa kama hakuna amani, watu wanadhalilika kwa kukosa haki zao kwa sababu ya ukosefu wa amani, tuidumishe amani tuliyonayo,” alisema.

Jafo aliwataka viongozi wa dini kuepuka migogoro katika nyumba za ibada na badala yake wawe na mshikamano katika kuuendeleza ummakatika maadili mema na kumcha Mungu ilikutengeneza taifa zuri lenye uchumi imara.

Kuhusu mmomonyoka wa maadili, Jafo alisema yapo baadhi ya mambo yanafanyika ambayo ni kinyume cha maadili na yakiendelea kuachwa yanaweza kuangamiza taifa.

“Tusiruhusu mambo machafu ili hizi neema tulizo nazo hapa nchini zisipotee tuhubiri amani, ucha Mungu, maadili mema na kuepusha malumbano kwani hayana tija,” alisema.

Kwa upande wake, Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir aliwataka masheik wa mikoa yote nchini kutumia nyadhifa zao kujenga uwezo wa kujitegemea kuanzia uchumi wa mtu mmojammoja kwani bila kufanya hivyo maendeleo hayataweza kupatikana.

Alisema hata katika vitabu vya dini zipo aya ambazo zinasisitiza uchumi hivyo aliwataka kuhubiri masuala ya uchumi mara kwa mara.

“Tunapoelekea katika kutekeleza kauli mbiu yetu ya jitambue, badilika na acha mazoea tunatakiwa kusisitiza uchumi kwani hata ndani Qur-an kuna aya zinaelezea umuhimu wa uchumi,” alisema.

Aidha, aliwataka masheikh hao kuwa na umoja na mshikamano na kuacha Istighafu ambayo inaweza kuwagawa Waislamu vipande vipande na kudhoofisha dini na taifa.

“Kama tunataka kupata maendeleo basi mshikamano ni muhimu, fanyeni kazi kwa uaminifu na uadilifu, tuache istighafu ambayo ndiyo sababu ya mgawanyiko wa uislamu hapa nchini,” alisema.



Chanzo: mwananchi.co.tz