Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wazazi wanaowashinikiza watoto wao kutofanya vyema mitihani waonywa

Wed, 9 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mtwara. Mkuu wa wilaya ya Nanyumbu, Moses Machali amesema atawachukulia hatua wazazi wote waliohusika kuwaagiza watoto wao kufeli mitihani makusudi katika mitihani ya kuhitimu darasa la saba mwaka 2018.

Inaelezwa kuwa wanafunzi katika shule nane za wilaya hiyo wamefeli wote licha ya kuwa baadhi yao walikuwa na uwezo darasani na walijiandaa vyema kufanya mtihani huo.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatatu Januari 7, 2019 Machali amesema watawasaka wazazi na kuzungumza nao ili kuwaonyesha kuwa tabia hiyo si nzuri.

“Tumeshaanza kufanya mikutano mbalimbali kuelimisha wananchi kuthamini elimu. Tukishawaelimisha umuhimu wa elimu hili tatizo litakwisha,” amesema Machali.

“Kama ni kuwafunga hatuwezi kuwafunga wote lakini wale ambao watakaidi maelekezo ya Serikali kutoona umuhimu wa watoto wao kufaulu hatutawaonea aibu tutahakikisha wanakaa sawasawa.”

Mbunge wa Nanyumbu, Dua Nkurua amesema tabia ya wazazi kuagiza watoto wao kujifelisha ni mchezo wa miaka mingi na kwamba mwaka 2018 imepungua kidogo baada ya kuwakanya.

Mmoja wa wazazi, Maulid Salum amesema baadhi ya wazazi wamekuwa wakishangaa kuona watoto wao wanafaulu licha ya kutojua kusoma na kuandika na hivyo kuwapa hofu ikiwa watafaulu.

“Mtoto kama hajui kusoma na kuandika halafu anafaulu unajua inasikitisha sana, anafaulu vipi? Ndio maana inafikia wakati mzazi anamwambia asifanye vizuri katika mitihani yake akiamini  kwamba huko shuleni kuna kitu kinafanyika,” amesema Salum.



Chanzo: mwananchi.co.tz