Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waumini KKKT Dar wataka mwaka 2020 uwe wa maridhiano

Waumini KKKT Dar wataka mwaka 2020 uwe wa maridhiano

Thu, 2 Jan 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

 Waumini wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), usharika wa Azania Front Dar es Salaam wamesema wangependa kuona mwaka wa 2020 unakuwa mwaka wa maridhiano baina ya makundi yanayotofautiana katika jamii.

Waumini hao waliyasema hayo jana usiku Jumanne Disemba 31, 2019 wakati wa ibada ya mkesha wa kuupokea mwaka mpya wa 2020.

Mkazi wa Upanga, Francisca Jerome alisema angependa kuona mwaka 2020 Watanzania wote wanakuwa na sauti moja kwa kuondoa tofauti zao kupitia maridhiano.

"Binafsi nafurahi kufika mpaka wakati huu nikiwa na afya lakini kwa mambo ya kitaifa, nadhani tunahitaji zaidi umoja. Tukae chini pamoja kwenye nyumba zetu za ibada, kwenye vyama vyetu au kwenye ofisi zetu tutafute maelewano," alisema.

Kwa upande wake, Ignas Kasoni alisema anamuomba Mungu mwaka 2020 uwe na amani na mafanikio kwa kila mmoja ili maisha yawe ya furaha kwa wote.

"Ukifanikiwa kuwa na afya basi omba mafanikio na yasiwe mafanikio yako tu bali na kwa wengine maana kwenye hata maisha tunategemeana. Hayo yote tutayapata kama kuna amani," alisema Kasoni. Awali, akihubiri wakati wa ibada hiyo, Mchungaji Kiongozi, Charles Mzinga alisisitiza kwamba mwaka mpya ukawe mwanzo wa furaha kwa kila mmoja ukawe mwanzo mpya wa maisha ya ushindi.

"Mungu anaweza kukuandaa kwa miaka minne, mitano au zaidi ili mradi tu siku moja uwe mahala fulani. Wana wa Israel waliandaliwa kwa miaka mingi jangwani...jambo la muhimu ni kutokata tamaa hata kama mwaka uliopita haukuwa mzuri kwako," alisema Mchungaji Mzinga.

Chanzo: mwananchi.co.tz