Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watoto walia unyanyasaji mbele ya Askofu Ruwaichi

33912 Pic+watoto Tanzania Web Photo

Sat, 29 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Watoto wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam waliokuwa wakiadhimisha kumbukumbu ya watoto mashahidi waliouawa na Mfalme Herode wakati Yesu alipozaliwa, wamepaza sauti wakitaka vitendo vya ukatili dhidi yao vikomeshwe.

Wamesema kuna tatizo hilo hapa nchini kutokana na kuwapo baadhi ya matukio ya unyanyasaji, utekaji na ukatili dhidi yao.

Watoto hao waliitaja Tanzania wakati wakijibu swali kutoka kwa Askofu Mkuu Mwandamizi wa jimbo hilo, Thadei Ruwaichi aliyewauliza kuwa ni nchi gani barani Afrika ina machafuko.

Majibu ya watoto hao yaliwafanya baadhi ya waumini wakiwamo walezi wao kuguna wakionyesha kushangazwa na kauli zao.

Hata hivyo, Askofu Ruwaichi alisema kuwapo kwa habari za matukio ya ukatili dhidi ya watoto kumewafanya waitaje nchi yao, licha ya kuzitaja nchi nyingine kama DRC, Somalia na Sudan.

Ripoti ya Haki za Binadamu ya 2017 iliyotolewa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), inaonyesha matukio 13,457 ya ukatili dhidi ya watoto yaliyoripotiwa nchini huku asilimia 85 yakiwa ni yale ya ubakaji na ulawiti.

Akihubiri katika misa hiyo iliyofanyika Msimbazi Centre jijini Dar es Salaam, Askofu Ruwaichi alisema, “Watoto watatu wameitaja Tanzania, je habari za watoto kunyanyaswa hazipo? Habari za watoto kupotea zipo au hazipo? Watoto wanaopotea wanaliwa na fisi au chui?”

Baada ya kuuliza hivyo waumini waliokuwapo walijibu kuwa wanaofanya vitendo hivyo ni watu.

Askofu Ruwaichi alisema wapo watu wanawaumiza watoto na kwamba ni jukumu la wazazi, walezi, wachungaji na viongozi wengine kuhakikisha kuwa wanasimamia ustawi wa kila mtoto.

“Watoto hawastahili kuteswa, lazima tuache roho mbaya na makandokando ya roho mbaya. Tuombe Mungu ili watoto walindwe, wapendwe, waheshimiwe na wajisikie salama.”

Alisema kiuhalisia hakuna sababu ya watu wazima kutofautiana na watoto kwa sababu utoto wao siyo tishio kwao.

Akitafsiri Biblia, Askofu Ruwaichi alisema Mfalme Herode wakati wa utawala wake aliposikia habari za kuzaliwa kwa Yesu alijua angemsumbua hivyo aliamua kuwaua watoto wote wa kiume waliozaliwa siku hiyo.

“Watoto si tishio, tusiwe kama Mfalme Herode aliyeamua kuwaua watoto kwa sababu alijua kati yao angemuua Yesu ambaye alizaliwa kudumisha amani kati ya watu na Mungu,” alisisitiza.

Alisema kilichosababisha Herode kuwaua watoto hao ni wivu, chuki na roho mbaya.

“Kuna mtoto mwingine amejibu hapa kuwa mtu mwenye roho mbaya hataki maendeleo ya wenzake akisikia mwingine anafanikiwa au anafanya mambo mazuri inamkera, mtu huyu anatafunwa na chuki.”

Baadhi ya walezi wa watoto hao walisema matukio mengi ya kuumizwa kwa watoto yanasababishwa na watu wazima na miongoni mwao ni ndugu wa karibu.

“Mfano matukio ya ubakaji, anayeweza kumfanyia unyama mtoto ni mtu wa karibu anayeshinda naye kila siku. Wazazi tuwe makini,” alisema Anania Jumanne, mmoja wa walezi.

Alisema ni lazima jamii iwe na utamaduni wa kuwalinda watoto dhidi ya matukio ya ukatili na kutoa taarifa juu ya watu wanaowanyanyasa.

Baadhi ya watoto walisema watu wenye roho mbaya ndiyo huwaumiza. Walitoa sifa za mtu mwenye roho mbaya kuwa ni yule aliyejaa chuki, wivu, asiyependa mafanikio ya mwingine, mwongo, mwizi na anayeweza kumuumiza mwenzake bila sababu.



Chanzo: mwananchi.co.tz