Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watetezi haki za binadamu wampa tano Askofu Shoo

33138 Pic+watetezi Tanzania Web Photo

Mon, 24 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Wadau wa Haki za Binadamu nchini, wamepongeza hatua ya Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Shoo kukemea ukatili kwa watoto ukiwamo ubakaji na ulawiti.

Katika salamu zake za Krismasi na Mwaka Mpya, pamoja na mambo mengine, Askofu Shoo alisema jamii inashuhudia vitendo vikubwa vya ukatili kwa wanawake, watoto na vijana.

“Kwa mfano vipo vitendo vya kikatili kama vile ubakaji, ukeketaji, ndoa za utotoni na ukatili wa kila aina,” alisema Askofu Shoo ambaye pia ni Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini ya KKKT na kuongeza;- “Zipo changamoto mbalimbali zinazotokana na umasikini zinazosababisha watu kuwa na manung’uniko na kukosa matumaini. Ujumbe wa Krismas na Mwaka Mpya utukumbushe sote kutokata tamaa.”

Hata hivyo, pamoja na kumpongeza Askofu Shoo, wametaka Taifa lijitafakari na kutafuta kiini cha ongezeko la tatizo hilo licha ya adhabu kwa wabakaji kuwa kali hadi kifungo cha maisha.

Mkurugenzi wa Asasi ya Action for Justice in Society (Ajiso), Virginia Silayo alisema jana kuwa, kauli ya Askofu Shoo akiwa kiongozi wa kiroho, imempa faraja na itaongeza nguvu ya mapambano ya vitendo hivyo.

“Tunamshukuru sana baba Askofu kwa kupaza sauti yake juu ya haya matatizo hasa ya watoto wadogo kubakwa na kulawitiwa. Vyombo vingine vya dini vipaze sauti zao na jamii nayo ipaze sauti,” alisema.

Mwanasheria Harold Sungusia alisema pamoja na kumshukuru Askofu Shoo kwa kukemea mambo hayo, alitaka Taifa lijikite kushughulikia kiini kinachosababisha kuongezeka kwa vitendo hivyo.

“Viongozi wetu wengi wanaangalia tatizo pasipo kuangalia chimbuko. Tuna tatizo kubwa la maadili kama Taifa. Tuanze kwanza kutibu ethics (maadili) na Integrity (uadilifu),” alisema Sungusia.

Alisema muda mwingi hivi sasa, wazazi hawakai na kuzungumza na watoto wao, badala yake wanategemea kazi hiyo ifanywe na walimu au wafanyakazi wa ndani jambo ambalo si sawa.

“Wazazi wenyewe siku hizi nao ni shida. Hawawi mifano kwa watoto. Kila siku kwenye magazeti ya udaku baba kafumaniwa au mtu fulani ni shoga. Watoto nao wanaiga. Jamii ni tatizo,” alisema.

Mwenyekiti wa taasisi ya Maadili Centre, Florentina Senya, mbali na kumpongeza Askofu Shoo, alitaka kanisa liwe na mpango mkakati wa kuwajengea uwezo waumini kupiga vita vitendo hivyo.



Chanzo: mwananchi.co.tz