Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wapentekoste wajitenga na makanisa yanayohubiri mafuta, maji kanisani

Mafuta Upako.jpeg Wapentekoste wajitenga na makanisa yanayohubiri mafuta, maji kanisani

Sat, 20 Jul 2024 Chanzo: Mwananchi

Baraza la Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (CPCT) limetoa tamko la kutowatambua viongozi wa dini wanaotumia visaidizi vya maombi kama mafuta, maji, keki, leso, chumvi na au udongo.

CPCT inayoundwa na mkanisa 12 imesema wanaofanya hivyo na vinginevyo si wanachama wao bali wanachafua Upentecoste ulioenea ulimwenguni.

Baraza hilo limetoa tamko hilo jana Ijumaa Julai 19, 2024 mbele ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliyekuwa mgeni rasmi kwenye Kilele cha Mkutano wa Baraza la Maaskofu wa CPCT, uliofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Biblia Miyuji jijini Dodoma.

Tamko hilo wanalitoa takribani wiki moja imepita tangu Mwananchi lililoripoti mfululizo wa habari ya uchunguzi juu ya makasani yanayotumia visaidizi hivyo.

Katika habari hiyo, iliangazia baadhi ya viongozi wa makanisa hayo ‘manabii na mitume’ wanavyonufaika na biashara ya kuuza maji, mafuta na ua chumvi. Shuhuda za waumini wao jinsi baadhi walivyonufaika navyo na wale ‘waliopigwa’ kwa kutokupata yale waliyokusudia.

Jana Ijumaa, katika semina hiyo ya viongozi wa CPCT, Katibu Mkuu wa baraza hilo, Dk Baraka Kihoza ametoa tamko la baraza linalojitenga na kinachoendeleaviongozi wa dini wanaotumia visaidizi hivyo.

Dk Kihoza amesema miaka ya hivi karibuni kumezuka kundi la viongozi wa dini wanaojiita wapentekoste na wanatumia visaidizi vya maombi kama maji ya upako, mafuta ya upako, udongo, chumvi, leso, keki za upako na vingine vingi kwa kuwatoza waumini gharama za visaidizi hivyo kinyume na Neno la Mungu.

"Watanzania watambue viongozi hao wa dini siyo wanachama wetu na wala siyo wapentekoste kwa sababu wanapingana na misingi ya Kipentekoste ambayo inaamini katika Jina la Yesu Kristo na si katika visaidizi vya maombi," amesema Dk Kihoza.

Amesema viongozi hao wa dini (bila kuwataja majina yao) wanatumia vibaya baadhi ya vifungu vya maandiko kwenye Biblia Takatifu kufanyia biashara kwani vitu hivyo kama maji, mafuta leso na udongo vilitumika kwa kazi maalum ambayo haikujirudia tena kwenye utendaji wao wa kazi na siyo kwamba vitatumika miaka yote katika kutenda ishara zile zile.

Amesema viongozi hao wa dini wamegeuza miujiza iliyofanywa kwenye Biblia kwa kutumia vitu hivyo kama biashara na kwenda kinyume na Neno la Mungu linalosema wamepata bure watoe bure.

Wamesema misingi ya Upentekoste imesimama kwenye Neno la Mungu na inaamini uponyaji na miujiza katika Jina la Yesu na si vinginevyo kwani kwa kufanya hivyo wanataka kuwaaminisha watu kuamini miujiza katika vitu na si katika Jina la Yesu ambaye ndiye mtenda miujiza.

Amesema CPCT haikubaliani na mafundisho yanayohimiza matumizi ya visaidizi. Aidha kwa kutolewa bure au kwa malipo ili visaidizi hivyo viwasaidie watu katika matatizo yao kwa sababu hakuna mahali popote kwenye Biblia ambapo mitume walaifanya maombezi kwa malipo ya fedha.

"CPCT inatambua inawezekana kabisa Roho Mtakatifu kumpa mtumishi wa Mungu maelekezo ya namna ya kutimiza huduma ya kiuponyaji lakini haitakuwa hivyo siku zote na kwamba maelekezo hayo maalum hayawezi kutumika kutengeneza fundisho," amesema Dk Kihoza.

Dk Kihoza amesema Imani ya kipentekoste asilia haihusiani kwa vyovyote vile na uuzwaji wa manunuzi ya huduma za kiroho bali wanaamini Jina la Yesu limejitosheleza na wala halihitaji msaada wa ziada wa chumvi, mafuta, sabuni na vitu vinavyofanana na hivyo.

Naye Mwenyekiti wa baraza hilo, Dk Barnabas Mtokambali amesema mojawapo ya kazi za baraza hilo ni kukemea maovu yanayojitokeza kwenye jamii ikiwemo uchawi, mapenzi ya jinsia moja, kutelekeza familia na kujenga ustawi wa jamii inayomjua Mungu.

Aidha amewataka Watanzania kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura ili wapate nafasi ya kushiriki kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Ameitaka Serikali kuweka mazingira rafiki ya watu kushiriki uchaguzi ili uwe huru na hakina kuepukana na matumizi makubwa ya vyombo vya dola ambavyo huwa vinazua hofu na taharuki kwa wananchi.

Ujumbe wa Majaliwa

Katika hotuba yake, Majaliwa amewahakikishia viongozi hao wa dini uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 utakuwa huru na haki na kuwataka Watanzania kujitokeza kwa wingi kwenye uandikaji na uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura.

Amesema Serikali inatambua mchango mkubwa wa taasisi za kidini katika kutoa huduma za kijamii kama vile elimu, afya na sekta nyingine muhimu hivyo itashirikiana nao katika kuhakikisha kuwa malengo yao yanatimia.

“Tuna kila sababu ya kuyashukuru Makanisa kwa kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali katika kuleta maendeleo ya wananchi kwa ujumla, yamekuwa sehemu ya suluhisho katika changamoto za kijamii kama vile umaskini, elimu duni, na matatizo ya kiafya,” amesema.

Majaliwa amesema:“Nitumie fursa hii kusisitiza taasisi za dini kuendelea kuimarisha ushirikiano na Serikali na kuendelea kuiishi kwa vitendo kaulimbiu yenu ya Palipo na Umoja, Bwana huamuru baraka! Bwana huamuru baraka, palipo na Umoja.”

Chanzo: Mwananchi