Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanafunzi 212 wabebeshwa mimba ndani ya miezi 11

34101 Mimba+pic Tanzania Web Photo

Mon, 31 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mtwara. Wanafunzi 212 wa shule za msingi na sekondari mkoani Mtwara na Kilosa mkoani Morogoro, wamekatishwa masomo baada ya kupata ujauzito kati ya Januari na Novemba, mwaka huu.

Mkoani Mtwara, takwimu zilizowasilishwa juzi katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) na Katibu Tawala wa Mkoa, Dk Jilly Maleko zinaonyesha kuwa kati ya wanafunzi hao, 150 ni wa sekondari na 38 msingi.

Dk Maleko alisema Wilaya ya Tandahimba inaongoza kwa kuwa na wanafunzi 48 waliopata mimba, sekondari wakiwa 20 na msingi 28.

Aliitaja wilaya inayofuata kuwa ni Masasi yenye mimba 36 za wanafunzi, kati yao sita ni wa shule ya msingi na 30 sekondari. Nanyumbu (25) msingi zikiwa tatu na sekondari 22, Manispaa ya Mtwara Mikindani (25), msingi mimba moja na sekondari 24.

“Halmashauri ya Wilaya ya Newala mimba ziko 18, mbili shule ya msingi na 16 sekondari, Mtwara kuna mimba 12, tatu shule za msingi na tisa shule za sekondari, Masasi Mji ziko 10 zote za sekondari.

“Newala Mji zipo tisa, moja ya shule ya msingi na nane za sekondari na Nanyamba Mji zipo tano, mbili za msingi na tatu sekondari,” alisema Maleko.

Akichangia hoja katika kikao hicho, Mbunge wa Nanyamba, Abdallah Chikota alishauri kuandaliwa kwa mpango maalumu wa kukabiliana na janga hilo.

Mbunge wa Ndanda, Cecil Mwambe alisema suala la mimba kwa wanafunzi linachangiwa na malezi, huku akisema kuwa baadhi ya wanafunzi waliopata ujauzito wanaishi mijini na wako karibu na wazazi wao tofauti na wale wanaoishi kwenye nyumba za kupanga hususan wa sekondari.

“Mtwara Mikindani sekondari kuna mimba 24 na hapa ni mjini kwa maana watoto wanaamka kwao wanakwenda shule, kwa hiyo hizi mimba wamezipatia nyumbani tukiachana na hii watoto wanakaa mbali na nyumbani kwao,” alisema Mwambe.

“Kuna suala la utamaduni na namna watu wanavyojali, ili tulikomeshe lazima tufuatilie kesi zilizopo kwa sababu ni za jinai,” alisema.

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa alisema; “Sisi tunakimbilia mahakamani wanafunzi na wazazi wanakimbilia kuharibu ushahidi, mimi nimewahi kushauri sheria ibadilishwe imuwajibishe na mtoto wa kike.”

Kilosa

Wakati hali ikiwa hivyo katika mkoa wa Mtwara, wanafunzi 24 wa shule za sekondari katika Wilaya ya Kilosa wamekatisha masomo yao kati ya Januari na Septemba mwaka huu kwa sababu ya mimba.

Ofisa Elimu Sekondari wa wilaya hiyo, Paula Nkane alisema jana kwamba tatizo la mimba ni miongoni mwa changamoto zinazoikabili sekta ya elimu.

“Tuna wanafunzi wa kike 7,617 na waliopata mimba ni idadi hiyo niliyoitaja. Serikali inawashughulikia wanaume waliohusika kwa mujibu wa sheria na mkakati wetu ni kusiwe na mwanafunzi hata mmoja atakayeacha shule eti kwa sababu ya mimba,” alisema.

Aliwataka wazazi na walezi kujenga tabia ya kuzungumza na watoto wao kuhusu miili yao na namna ilivyo hatari kujiingiza kwenye uhusiano wakati wakiwa na umri mdogo.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Mazinyungu Ngamba Manegese alisema katika kudhibiti tatizo la mimba, wamekuwa wakiwapima wanafunzi mara kwa mara.

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Zombe wilayani Kilosa, Ismail Kindaile alisema kitakachosaidia kukomesha tatizo hilo ni elimu kwa watoto kuhusu afya ya uzazi.



Chanzo: mwananchi.co.tz