Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Walimu waliohama Mtwara wawekwa kikaangoni

Sat, 29 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mtwara. Kiama cha walimu wa shule za Serikali waliohama pasipo maombi yao ya uhamisho kupitishwa na wakurugenzi wa halmashauri husika kinakuja baada ya kuibua mjadala.

Tuhuma hizo zimeibuliwa jana katika kikao cha Kamati ya Ushauri cha Mkoa wa Mtwara (RCC) baada ya baadhi ya wakurugenzi wa halmashauri kulalamikia barua wanazozipokea kutaka wawapitishe wahame maeneo yao ya kazi.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara, Omari Kipanga alisema amewahi kupokea barua kutaka apitishe walimu huku mkurugenzi wa halmashauri ya Nanyumbu, Hamis Dambaya akisema barua alizopokea wengi wanataka kuhamia katika maeneo wanayotokea.

Mbunge wa Mtwara Vijijini (CCM), Hawa Ghasia alisema kanuni zinataka mtumishi kuhamishwa baada ya kumaliza muda wake wa majaribio lakini wakati mwingine inakuwa tofauti hasa mtumishi anapopata namba ya hundi ya malipo.

Alisema pamoja na kwamba kuhama ni haki ya mtumishi, lakini usawa uangaliwe hasa katika mikoa ya pembezoni ambayo haina uwiano wa mwalimu na wanafunzi.

“Tuwaombe Utumishi na Tamisemi suala la kuhamisha watumishi mikoa ya pembezoni ili kuhakikisha kuna uwiano sawa, wale wanaokuja kwa ajira wakae walau miaka mitatu  na kama wakimuhamisha mtu basi wahakikishe wanaleta mwingine wa kuziba ile nafasi,” alisema Ghasia.

Mkuu wa mkoa huo, Gelasius Byakanwa amlishauri Wizara ya Utumishi kama inaweza kutengeneza waraka kupima haki ya mtumishi kuajiriwa, haki ya anayehama pamoja na haki ya mtu anayetakiwa kupewa huduma ili  kuwe na usawa.

“Lazima kuwe na usawa, mtumishi anayo haki ya kuhama vipi kuhusu haki ya hawa wenye haki ya kupewa huduma kama ni elimu, afya au maji niwaombe Utumishi waje na waraka kupima haki zote tatu na kama basi mtu akihamishwa walete mtu mwingine kujaza ile nafasi,” amlisema Byakanwa.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, George Mkuchika ambaye ni mjumbe wa kikao hicho, alisema kanuni za Serikali zinasema ni haki ya mtumishi kuhama lakini hajihamishi mwenyewe.

Alisema waraka uliotolewa na Serikali unasema ni marufuku mkurugenzi au mtu yeyote anayeongoza ofisi yoyote kukataa kupitisha barua ya mtu anayetaka kuhama kwani kufanya hivyo kunamnyima haki kuwasiliana na mwajiri wake.

“Barua inapoandikwa kupitia ‘kwa’ ni fursa ya wewe kutoa maoni yako unasema nina uhaba wa watumishi sipendekezi uhamisho huu labda kama nitaletewa mbadala ndio maana ya kupitia kwako.”

“Kwa hiyo ukiipitisha barua haina maana kwamba mtu ameshahama, ulichofanya ni wewe ambaye unafanya naye kazi utupe maoni yako,” alisema Mkuchika.

Aidha alisema katika utumishi wa umma kuna sababu za kiubinadamu ambazo pia zinapelekea mtu kuomba uhamisho.

“Mtu yuko Kigoma baba yake ana miaka 95, mama amefariki na huyu ndio mtoto wa kwanza ndio huyohuyo wanayemtegemea, kwa hiyo haiwezekani watu wasihame, lazima ieleweke hiyo kupitia kwa maana yake ni wewe kutoa maoni yako na katibu mkuu anaangalia anakofanya kazi wanasemaje,” alisema.

 Mkuchika alimuagiza Katibu Tawala Mkoa wa Mtwara (RAS), Dk Jilly Maleko kuwasiliana na wakurugenzi wake kupata majina ya waliohama pasipo wakurugenzi kuwapendekeza ili kuwashughulikia waliowahamisha bila kufuata utaratibu.

“RAS uwasiliane na wakurugenzi wako kwa zile halmashauri ambazo walimu wake wamehamishwa kwa kisingizio kufuatia barua yako ya tarehe hiyo nimekuhamisha tupate majina yao, wale ambao hamjawapendekeza nao tupate majina yao, tuleteeni pia na majina ya watu ambao wamekuja kuripoti hajamaliza muda wa majaribio akahamishwa,” alisema.



Chanzo: mwananchi.co.tz