Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waislamu na Wakristo endeleeni kudumisha amani, wema na upendo- Shaka

8d4b9ca7c4b22d978a90df6294d5b53f.jpeg Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Shaka Hamidu Shaka

Sat, 6 Nov 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Shaka Hamdu Shaka amewaomba waumini wa dini ya Kikristo na Waislamu kuendelea kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya sita chini Rais Samia Suluhu Hassan kuendelea kuwaletea wananchi maendeleo nchini huku wakidumisha amani na ushirikiano uliopo nchini

Pia amewataka waumino hao, kuendelea kusimamia na kufuata amri zilizoelekezwa na Mungu kwa kutekeleza mafundisho ya kiongozi wa dini ya mtume muhammad (saw) kueneza ujumbe wa amani ulimwenguni.

Hayo ameyasema jana katika mahojiano mafupi yaliofanyika kwenye Maulid ya Mtume muhamad (saw) yaliofanyika katika Madrasat Abbasia katika makutano ya mitaa ya Mafia na Likoma Kariakoo Jijini Dar es Salaam alisema ni vema watanzania wakaendelea kudumisha amani na upendo huku wakifuata mafundisho ya Mungu.

Alisema ni vema watu wakaishi na kuufuata mienendo na mafundisho ya Mungu huku wakikwepa vitendo viovu kama dhulma, kusengenyana na kutoishi kwa kuchukiana."Kila binadamu amuhimize mwenzake katika kutenda haki na kutimiza wajibu ikiwemo kujiweka mbali na matendo maovu ambayo Mungu huchukizwa nayo," alisema na kuongeza

"Mkusanyiko huu mkubwa mnaona unafanyika hapa leo ni kutokana na nchi yetu inaamani hivyo tujue yapo mataifa kadhaa duniani yanatamani watu wake wakusanyike pamoja kama sisi lakini haiwezekani kwa kuwa hakuna amani katika nchi zao," alisisitiza Shaka.

Aidha kutokana na kuwepo kwa matokeo ya mazingira mazuri ya ustawi wa amani na umoja nchini ,watanzania hawana budi kuilinda na kuiendeleza amani waliobarikiwa na Mungu.

"Tuzidi kufanya bidii na kukithirisha ibada zetu misikitini na makanisani kumuomba Mungu aijalie neema na fanaka nchi yetu,azidi kutunza na kudumisha amani iliyopo nchini na endapo kama kuna mwenye shari zake au uchochezi wowote Mungu mkarimu azivunje nia na dhamira zao batili, alisema

Alisema ni vema jamii iendelee kukemea vitendo viovu visivyompendeza Mungu ambavyo kwa aina moja au nyingine vinaweza kuleta machafuko ya amani iliyopo nchini.

Aidha Shaka aliwataka waumino wote wakristo na waislamu kufuata mafundisho na mienendo ya Mitume na Manabii ambao walifikisha duniani ujumbe wa kutambua haki,wajibu na kuwataka watu waishi kwa wema, upendo na kuhurumiana.

Kwa upande wake Mufti wa Tanzania, Mufti Abubakar Zubeir aliwasihi waumini wote wa kiislamu nchini kuendelea kuchanja chajo ya Uviko - 19 ili kuendelea kuongeza kinga katika kupambana na gonjwa hili hatari.

Pamoja na hayo Mufti alisisitiza waumini na watanzania wote kuendelea kudumisha mshikamano na kushirikiana na serikali katika ujenzi wa Taifa.

Chanzo: www.habarileo.co.tz