Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wachungaji 250 watembelea eneo litakalojengwa chuo

Wed, 20 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Hai. Wachungaji 250 wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini, wakiongozwa na Mkuu wa Kanisa hilo, Askofu Fredrick Shoo leo Jumanne Machi 19, 2019 wamekutana katika eneo wanalotarajia kujenga Makao Makuu ya Chuo Kikuu Kishiriki cha Kumbukumbu ya Stefano Moshi (SMMUCO) kufanya maandamano kuzunguka eneo hilo na maombi.

Hatua hiyo imekuja kufuatia madai ya kuwepo kikundi cha watu kilichoandaa vijana kwa ajili ya kuvamia eneo hilo na kufanya shughuli za kilimo.

Eneo hilo la ukubwa wa ekari 50, lililopo Kijiji Cha Nshara Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro lilitolewa na vyama vya ushirika vya Uduru na Nshara kwa kanisa kwa ajili ya ujenzi wa makao makuu ya chuo hicho.

Akizungumza kabla ya kuanza kwa maandamano hayo na maombi, Askofu Shoo amesema baada ya kupewa eneo hilo, walifuata taratibu zote na tayari wamepewa hati miliki ya eneo hilo.

Amesema wakati wakiendelea na taratibu za kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa chuo hicho na ramani, Ijumaa ya Machi 15, 2019 walipata taarifa za uwepo wa kikundi cha watu kilichoandaa vijana kwa ajili ya kuvamia eneo hilo huku wakijua ni la kanisa.

"Kuna kikundi kidogo cha watu, kimeandaa vijana na kuwataka siku ya Alhamisi waje hapa kwa ajili ya kugaiwa eneo hili ili wafanye shughuli za kilimo, hii si sawa, maana eneo hili kwa sasa tuna hatimiliki," amesema Dk Shoo.

Alisema baada kupata taarifa za kuwepo kwa watu wanaotajwa kuvamia eneo hilo, Jumapili ya Machi 17, 2019 alifika usharika wa Nshara na Hosiana na kuzungumza na wananchi ambao ni wanaushirika waliotoa eneo hilo.

"Jumapili nilikutana na wananchi katika usharika wa Nshara na Hosiana na kuzungumza nao na kubaini wanaochochea hili ni kikundi kidogo cha watu, nilionya juu ya hilo kwa kuwa kitu kikishawekwa wakfu kwa kazi ya Mungu, hapapaswi kufanyiwa mchezo," amesema.

Mbali na Askofu Dk Shoo na wachungaji, pia maombi hayo yamehudhuriwa na askofu mstaafu wa Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa hilo, Dk Erasto Kweka, katibu mkuu wa dayosisi hiyo, Arthur Shoo na watumishi wengine wa dayosisi hiyo.

 



Chanzo: mwananchi.co.tz