Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Viongozi wa dini wazungumzia uchaguzi

Wed, 2 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar/mikoani. Viongozi wa dini nchini wamewataka Watanzania kufunga na kusali ili kudumisha amani na utulivu katika kipindi cha chaguzi zijazo za Serikali za Mitaa mwaka huu na Uchaguzi Mkuu wa 2020.

Walisema hayo katika ibada za mkesha wa mwaka mpya zilizofanyika juzi usiku na jana asubuhi.

Kiongozi wa Kanisa la Evangilical Assembles of God (EAG), Mwanjelwa, Mbeya, Isaya Kayayo alisema Watanzania wanapaswa kuendelea kudumisha amani na utulivu katika kuelekea chaguzi hizo.

Muumini wa kanisa hilo, Vincent Asumwisye alisema Taifa ili lisonge mbele ni lazima kila mwananchi atambue wajibu wake wa kufanya kazi kwa bidii na kulipa kodi kwa mujibu wa sheria kwani ndiyo inayoendesha nchi.

Askofu Dayosisi ya Kaskazini Kati ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Solomon Masangwa aliwataka Watanzania bila kujali tofauti zao za kisiasa kushirikiana kimaendeleo ili kuinua uchumi wa Taifa.

Mchungaji Kiongozi wa Usharika wa KKKT Moshi Pasua, Manase Ndimbirwe akihubiri katika Mtaa wa Kalimani jana, aliwataka waumini kudumisha umoja, upendo na mshikamano kwa kuwa ndio msingi wa mafanikio.

Katika Kanisa Katoliki, Parokia ya Mtakatifu Petro, Oysterbay, Dar es Salaam, paroko msaidizi, Padri Barthlomeo Bachoo alisema, “Tunapoadhimisha siku kama hii, tuendelee kuiombea amani nchi yetu, tuwaombee viongozi wetu akiwamo Rais John Magufuli na baraza lake la mawaziri, wagonjwa, watu wenye mahitaji, lakini pia tusisahau kuwaombea vijana wetu wajiepushe na vitendo vya uvunjifu wa amani.”

Paroko msaidizi wa Kanisa Katoliki la St Joseph, Ernest Boyo alisema, “Tusipokuwa wanyenyekevu itakuwa vigumu kusikia habari za Mungu wala kupokea baraka zake, tunapoanza mwaka huu mpya kila mtu aimarishe amani ya familia yake na taifa kwa ujumla.”

Askofu Mwandamizi wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam, Yuda Thadeus Ruwa’ich alisema kazi mojawapo ya amani ni kuwa na uhusiano uliotengamaa na jirani yako.

Katika kanisa la Anglikana la Mtakatifu Albano, Dar es Salaam, Padri Meshack Malilo aliwataka Wakristo kutokata tamaa wakati wakikabikiana na changamoto za maisha, “Hata kama umepitia changamoto ngumu kiasi gani, neno la Mungu likupe nguvu ya kuendelea mbele na kupata amani na mafanikio makubwa.”

Paroko msaidizi wa kanisa Katoliki la mtakatifu Petro, Aziz Haule alisema, “Maisha tuliyonayo hapa duniani ni matayarisho ya maisha mengine, tunapofanya kazi tufanye kwa bidii na kwa malengo tukiutunza muda.”

Msaidizi wa Askofu wa KKKT Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Mchungaji Chediel Lwiza alisema kuhangaikia maisha pasipo kumtafuta Mungu hakuna baraka na ni maisha yasiyo na maana.

Mtume wa Kanisa la Inuka Uangaze, Boniface Mwamposa ‘Bulldozer’ aliwataka wazazi kuwa makini katika malezi ya watoto wao hasa wanapokuwa shuleni kwa kuwaandaa kiroho ili waweze kuwa na maadili mazuri.

Mchungaji wa Kanisa la Waadventista wa Sabato (SDA), Mtaa wa Kizota Dodoma, Stephano Bomani aliwataka viongozi nchini kuwa na moyo wa kujitolea na kufanya kazi kwa kuwajali wanyonge ili kupata baraka za Mungu.

“Ndugu zangu viongozi wa Tanzania, napenda kuwatia moyo msikate tama kuwatumikia Watanzania, pamoja na changamoto nyingi zinazojitokeza msikate tamaa. Mwaka 2019 tambueni Mungu yupo upande wenu na sisi viongozi wa dini hatutachoka kuwaombea,” alisema.

Imeandikwa Hadija Jumanne, Fortune Francis, Elizabeth Edward, Bakari Kiongo, Cledo Michael, Pamela Chilongola, Tumaini Msowoya, Peter Elias, Pamela Chilongola (Dar), Godfrey Kahango (Mbeya), Florah Temba (Moshi), Musa Juma (Arusha), Habel Chidawali (Dodoma), Sanjito Msafiri (Pwani).



Chanzo: mwananchi.co.tz