Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Viongozi wa dini wasikitishwa na kifo cha Maalim Seif

9c9cd167aace65edb1e2988a6ae0692e Viongozi wa dini wasikitishwa na kifo cha Maalim Seif

Thu, 18 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

VIONGOZI wa dini wameeleza kusikitishwa kwa kifo cha Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad na kumuelezea kuwa ni mtu aliyekuwa mzalendo, aliyeweka pembeni maslahi binafsi na kuridhia kuingia katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Wamewataka Wazanzibari kumuenzi kwa kuhakikisha umoja wa kitaifa hauvunjiki visiwani humo na pia vyama vya siasa kujua umuhimu wa kuungana kujenga nchi.

Katibu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Dk Charles Kitima, alisema taifa limempoteza mtu muhimu katika ujenzi wa demokrasia ya vyama vingi nchini na aliyekuwa tayari kuungana na chama tawala kujenga nchi kwa kuingia katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa huku akivitaka vyama vimuenzi kwa kuhakikisha vinashiriki kuijenga nchi.

Naye Shehe wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum, alisema kifo cha Maalim Seif si msiba kwa Wazanzibari pekee bali ni wa taifa kwani alikuwa kama mkono wa kulia wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Mwinyi katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

“Nawasihi Wazanzibari washike maneno ya mwisho ya Maalim Seif kuhusu Umoja wa Kitaifa Zanzibar, yarudiwe mara kwa mara. Wasiyumbe kwa kuondoka kiongozi huyo bali wajijenge kudumisha umoja wao.

Natoa pole sana kwa chama cha ACTWazalendo pia kwa kuondokewa na kiongozi wao,”alisema Shehe Alhad.

Kwa upande wake, Askofu Msaidizi wa Kanisa Katoliki Jimbo la Bukoba, Method Kilaini, alisema kifo hicho ni majonzi makubwa kwani mara zote Maalim Seif ameonesha uzalendo hata pale alipodai ameonewa lakini aliweka mbele maslahi ya Wazanzibari kuliko yake binafsi.

Alisema ni kifo cha mapema kwani alitegemewa kumsaidia sana Dk Mwinyi katika uongozi wake na aliwataka Wazanzibari wadumishe umoja ili kumuenzi Maalim Seif.

Naye Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Mchungaji Moses Matonya, alisema nchi imepoteza mtu muhimu katika maendeleo ya demokrasia ya vyama vingi na kiungo katika ujenzi wa Zanzibar mpya kupitia Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar.

Maalim Seif alifariki jana katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dar es Salaam, alikokuwa akipatiwa matibabu.

Chanzo: habarileo.co.tz