Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Viongozi wa dini washauri uundwe mwongozo wa maadili

Bbbf61a2187199327a1956c4914852e0.jpeg Viongozi wa dini washauri uundwe mwongozo wa maadili

Sun, 16 May 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

KUKENGEUKA miongoni mwa wazazi wa sasa wa kupokea bila kuchuja desturi za kimagharibi,kumetajwa kuwa chanzo cha mmomonyoko wa maadili katika familia jambo ambalo imeshauriwa uwepo mwongozo wa kitaifa wa maadili kurejesha jamii katika misingi ya utamaduni wa Kitanzania.

Viongozi wa dini, wanasaikolojia kadhaa waliozungumza na gazeti hili wakishauri kuwapo mwongozo wa kitaifa wa maadili, wameunga mkono ushauri uliotolewa hivi karibuni na Rais Samia Suluhu Hassan la kutaka nyumba za ibada kurejesha mafundisho ya maadili kwa waumini.

Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Nuhu Mruma, alisema suala la maadili si la serikali au viongozi wa dini pekee, bali la jamii nzima.

“Tumewapa maelekezo ngazi za chini wote, vipindi vya swala za Ijumaa na kwenye madrasa tumewataka kuongeza vipindi maalumu kwa ajili ya maadili. Hili ni tatizo la jamii nzima si wana dini pekee, dini ni ‘forum’ (jukwaa) moja wapo na ikitumika vizuri inasaidia zaidi, huu ni mmomonyoko wa maadili ambao ni tatizo la jamii nzima,” alisema Mruma.

Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Padri Charles Kitima, alisema kanisa Katoliki linatamani kuwepo na mwongozo wa kitaifa wa maadili utakaotoa dira katika eneo hilo.

“Lazima kuje na programu ya kitaifa, kurejesha uadilifu kwa kizazi na mali ya umma, haya yatafanikiwa tukipitisha mwongozo wa pamoja utakaoanzia katika masomo ya shule za msingi na sekondari. Rais Samia amefungua mlango mzuri tunashukuru. Tumeomba na alisema atatuita, akitupa fursa ya kuonana naye viongozi wa dini zote, tutaongelea hili,” alisema Dk Kitima.

Alisema Kanisa Katoliki kupitia Jumuiya ndogo ndogo, wanatoa mafundisho kwa ngazi ya familia kuhusu malezi na maadili. Lakini alisema familia au kanisa pekee halitoshi kwa kuwa watoto wanapokutana shuleni, wanabadilishana tabia na huko ndiko mabadiliko ya tabia hujengwa.

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Mchungaji Moses Matonya, aliunga mkono hoja ya kuwapo kwa mwongozo wa kitaifa kuhusu maadili na kueleza kuwa hata kabla ya Rais Samia kusema, wanafundisha hayo katika makanisa yao kwa kuwa yapo kwenye maandiko hivyo kauli ya Samia imechochea zaidi.

“Mtazamo wangu, mashuleni huko msisitizo uongezwe, tulivamie hili kutokea kwenye ‘angle’ (njia) zote, majukwaa ya kisiasa, dini, wakuu wa wilaya, vijijini mpaka shule zetu kutoka chini mpaka vyuo vikuu”.

Alipendekeza kuwepo na mwongozo wa pamoja wa kitaifa wa maadili ili kurejesha nidhamu na heshima katika jamii.

Mwanasaikolojia, John Ambrose alisema wakati umefika kuwa na mwongozo wa kitaifa wa maadili utakaozingatia misingi ya makuzi na malezi kuanzia utoto, ujana, utu uzima na uzee.

“Watu wanapaswa kukuzwa na mila na desturi zao, makuzi ni mila na desturi zilizokubalika katika jamii husika. Rais alisema hulka zetu na tamaduni zetu hatujengi nyumba kuwatunza wazee bali tunaishi nao katika familia zetu lakini hulka hii inapotea hivi sasa,” alisema Ambrose.

Akieleza sababu za mmomonyoko wa maadili, Ambrose alisema watu wanaowajibika kuwakuza vijana katika utamaduni, desturi na itikadi njema wamekengeuka na kurudi nyuma kutokana na muingiliano wa desturi na utamaduni mwingine.

Kuhusu nini kifanyike, alishauri Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na wadau nchini, kuandaa mwongozo wa kitaifa wa maadili na kurejesha mafunzo ya stadi za maisha zenye kubeba utamaduni na kuzifundisha kwa kundi lililo katika hatari zaidi ambalo ni kundi la rika ya balehe kwa vijana.

Katika kutekeleza hayo, wanawake wakatoliki (Wawata) katika Kanda ya Mtakatifu Dominiko ya Parokia ya Peter Claver, Mbezi Luis wameweka mkazo wa mafundisho ya maadili kwa watoto kwa kuwatambua watoto zaidi ya 80 wenye umri kati ya miaka mitatu hadi 14 na kuwapa mafunzo ya kiimani.

Alipozungumza na wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam Mei 7 mwaka huu, Rais Samia alihimiza umuhimu wa kurejesha mafundisho ya maadili misikitini na makanisani.

Chanzo: www.habarileo.co.tz