Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Viongozi wa dini waomba Samia apewe ushirikiano

1200eee0067e273f7ccbc5ea5c2b7223.jpeg Viongozi wa dini waomba Samia apewe ushirikiano

Mon, 22 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

VIONGOZI wa dini mkoani Morogoro wamewataka Watanzania kuungana na kutoa ushirikiano kwa Rais Samia Suluhu Hassan hasa katika kipindi hiki taifa likuwa limegubikwa na majonzi ya kuondokewa na kipenzi chao aliyekuwa Rais wa Tanzania, John Magufuli.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti mjini Morogoro jana, Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Morogoro, Jacob Mameo Ole Paulo alisema huu ni wakati wa Watanzania kushikama kama taifa na kumshukuru Mungu badala ya kuendelea kusikitika kutokana na kifo cha Magufuli.

“Kipindi hiki kila Mtanzania anapaswa kumshukuru Mungu kwa sababu imempendeza kutuletea Mama mchapakazi ambaye ataendeleza mazuri ya mtangulizi wake.”

“Sisi Watanzania tunachotakiwa kufanya kwa sasa ni kuungana na kumpa ushirikiano Rais wetu mpya (Samia) kwa sababu naamini licha ya kupokea nchi katika kipindi kigumu lakini ana uzoefu mkubwa katika uongozi, anachohitaji ni faraja ya Watanzania na kumuamini Mungu,” alisema Askofu Mameo.

Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Morogoro, Godfrey Sehaba alimuelezea Magufuli kuwa alikuwa mstari wa mbele katika kuyaishi maono ya Baba wa Taifa, Mwalimu Juius Nyerere hasa katika kukabiliana na madui watatu yaani ujinga maradhi na umaskini.

Alisema katika mapambano hayo, Magufuli alijitahidi kwa kiasi kikubwa kuimarisha sekta ya afya kwa kujenga vituo vya afya na hospitali za wilaya nchi nzima.

Kuhusu sekta ya elimu, Askofu Sehaba alisema Magufuli aliimarisha miundombinu ya sekta hiyo na ameacha alama kubwa ya elimu bure kuanzia shule za awali hadi sekondari na kutoa ongezeko la fedha za mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu.

Katibu wa Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata) mkoa wa Morogoro, Shehe Ahmed Said alisema ana amini kuwa nchi itaendelea kuwa salama na kukua kiuchumi kutokana na busara za Rais Samia na hiyo inatokana uwezo aliouonesha wakati akiwa kwenye nafasi ya Makamu wa Rais.

“Akiwa katika nafasi hiyo alimsaidia kwa kiasi kikubwa Rais Magufuli kutekeleza majukumu yake na hata kumuwakilisha vyema kimataifa pale alipokuwa akimuagiza.”

“Tuna imani naye kubwa kwani ana uzoefu mkubwa katika kuliongoza taifa tofauti na angaekuwa ndio mara yake ya kwanza kuongoza Watanzania," alisema Shehe Ahmed.

Katika hatua nyingine, aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Morogoro, Stephen Mashishanga amewataka Watanzania kumuenzi Magufuli kwa kuchapa kazi na kumtanguliza Mungu katika kazi zote watakazokuwa wanazifanya.

Alisema hayo baada ya kusaini kitabu cha maombolezo katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro jana cha kifo cha Rais Magufuli aliyefariki dunia Machi 17, mwaka huu.

Alitoa pia rai kwa viongozi wa serikali kumpa ushirikiano Rais Samia Suluhu Hassan na kuendeleza mazuri ambayo Magufuli wakati wa urais wake aliyafanya.

Chanzo: www.habarileo.co.tz