Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Viongozi wa dini wamshukuru Mungu, wampongeza Magufuli

6ed5cfdbdfde78c83d827c5418265392 Viongozi wa dini wamshukuru Mungu, wampongeza Magufuli

Sun, 1 Nov 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

VIONGOZI mbalimbali wa dini nchini wamemshukuru Mungu kwa kujibu maombi yao kuhusu uchaguzi kumalizika kwa amani na wamempongeza mgombea urais wa CCM, John Magufuli kuchaguliwa tena kuwa Rais wa nchi.

Aidha, wameonya watu wanaotaka wananchi waingie barabarani kupinga matokeo ya uchaguzi, wakiwataka wafuate utaratibu wa kwenda kwenye vyombo vya sheria kama hawakubaliani na matokeo hayo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na HabariLeo, viongozi hao wa dini walisema walimuomba Mungu uchaguzi uwe wa amani na amejibu maombi yao, hivyo wataendelea kutoa dua za kumshukuru katika nyumba za ibada.

“Tunamshukuru sana mwenyezi Mungu, ameendelea kupokea maombi yetu na mimi kama kiongozi wa dini sikuwa na wasiwasi pamoja na kwamba wapo baadhi wanafikiria kufanya wanayotaka kuyafanya, lakini watashindwa na hawataweza,” alisema Shehe wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhadi Mussa Salum.

Alisisitiza, “Huu ndio ushindi wa Tanzania na itazidi kuushangaza ulimwengu, ulinzi wa Mungu utaendelea kutufunika siku zote.”

Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kusini Magharibi, Dk Abednego Keshomshahara, alisema Mungu amesikia maombi ya Watanzania kwani amani imekuwepo na utulivu kwa kiwango kikubwa.

“Watu wanajua kuna maendeleo baada ya uchaguzi, tusijibanze kwenye uchaguzi tukabaki huko, hapana, mpaka sasa amani inaendelea, watu wanaendelea na kazi, kilimo, biashara, afya, elimu. Mpaka sasa amani ipo na tunaendelea kuomba amani na utulivu uendelee kuwepo.

Akizungumzia waliotangaza kupinga matokeo, Askofu Keshomshahara alisema, “Cha msingi ni kukubali matokeo na kama kuna mtu mwenye malalamiko, kuna namna ya kuyafikisha kwenye sheria, mfumo wa kisheria ufuatwe. Njia nyingine inaweza kuleta madhara. ”

Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Method Kilaini, alisema anamshukuru Mungu kwa namna alivyosimamia uchaguzi kwani kampeni zimefanyika vizuri, watu wamepiga kura kwa amani. Alishauri maisha mengine yaendelee.

Alisema amekuwa akifuatilia mauala ya uchaguzi nchini tangu mwaka 1965 hata katika nchi za Ulaya dosari zipo lakini akashauri walioshindwa wakubali matokeo kwa kuwa hakuna mshindi pasi na aliyeshindwa.

“Tulimuomba Mungu na amesikia sala zetu, uchaguzi umefanyika kwa amani na utulivu. Ushauri wangu sasa uchaguzi umeisha twende mbele, kwa wanaoona shida, waende mahakamani ili haki itendeke, lakini kwa ujumla uchaguzi tumemaliza twende mbele,” alisisitiza Kilaini.

Aliendelea, “Anayetaka watu waende barabarani yeye ndio aanze mstari wa mbele. Nawakumbusha vijana mahubiri yangu wakati wote nimekuwa nikiwaasa wasikubali kutumika, wataolewa macho, kuvunjwa miguu huko wakati anayelalamika yupo pembeni, nawasihi wanaolalamika waende mahakamani si barabarani.”

Chanzo: habarileo.co.tz