Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Viongozi wa dini walaani kasi ya mauaji

Kisu Damu Viongozi wa dini walaani kasi ya mauaji

Fri, 4 Feb 2022 Chanzo: www.habarileo.co.tz

Viongozi wa dini nchini wamelaani vitendo vya mauaji ya kikatili vinavyoendelea kutokea ambavyo wamedai sababu kubwa ni ukosefu wa maadili, imani za kidini pamoja na umaskini kwa jamii.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya viongozi hao walisema vitendo vya mauaji ambavyo vimeendelea kutokea katika jamii ni ishara kubwa ya ukosefu wa utu na maadili.

Mwenyekiti wa Kamati ya Amani Taifa ambaye pia ni Shehe wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Salum alisema kwa sasa jamii inakabiliwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa imani na kutoshika mafundisho ya dini jambo ambalo ni hatari.

“Kama kiongozi wa dini nalaani vikali matukio ya mauaji ya kikatili yanayoendelea kutokea hapa nchini, mauaji haya ambayo tumeshuhudia yanasababishwa na ukosefu wa hofu ya Mungu, mmomonyoko wa maadili, ukosefu wa utu pamoja na umaskini,” alisema Shehe Alhad.

Alisema ni wajibu wa viongozi wa dini kuhakikisha wanakabiliana na matukio hayo kwa kuelimisha jamii umuhimu wa uzalendo, utu na upendo ikiwamo kuacha tamaa ya mali ambazo zinagharimu maisha ya wengine.

“Wajibu wa kuelimisha jamii ili kukabiliana na mauaji tunao kama viongozi wa dini na wajibu huu hauishii kwetu pia uende kwa vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na serikali kuhakikisha wanawachukulia hatua watu wote ambao watabainika kuleta hali ambayo itavuruga amani,” aliongeza.

Mbali na hilo, aliwataka viongozi kuwa wazendo na wawajibikaji katika kulinda maslahi ya wananchi ikiwemo kukomesha vitendo hivyo vya mauaji kwa kuhimiza Watanzania kuwa wazalendo na kupendana wenyewe kwa wenyewe.

Padri Dk Idan Msafiri wa Jimbo Katoliki Moshi, alisema vitendo vya mauaji hayo ni kutokana na wananchi kukengeuka kwa kutozingatia amri na maagizo ya Mungu jambo ambalo viongozi wa dini wana wajibu mkubwa wa kuandaa mikutano na midahalo itakayokuwa na lengo la kurejesha utu na upendo.

“Kanisa Katoliki linaamini katika kupigania haki za mtu kuishi, tunapaswa kutubu kama taifa juu ya dhambi hii, lakini pia serikali ichukue hatua za wazi kwa watakaobainika na sisi wote tuwe wadau wa kupigania uhai,” alisema Dk Msafiri.

Shehe wa Mkoa wa Kilimanjaro na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mahusiano ya Dini mbalimbali Kanda ya Kaskazini, Shaabani Mlewa alisema ipo haja ya taifa kufanya maombi na dua ili kurejesha utu na upendo kwa jamii ili kukomesha matukio hayo.

Askofu mstaafu wa Kanisa la Assembles of God (TAG) na Rais wa Shirika la New Life foundation, Glorious Shoo alisema uwepo wa matukio hayo unatokana na mambo mbalimbali yaliyotabiriwa katika vitabu vya dini kwamba huenda ni siku za mwisho.

“Matukio tunayoyaona sasa yalishatabiriwa kwamba siku za mwisho kutatokea vitendo vya usaliti, upendo wa wengi kupoa, ndugu kwa ndugu kuchukiana na kuuana hivyo kama viongozi wa dini wajibu wetu ni kuwafundisha watu kurejea katika imani,” alisema Askofu mstaafu Shoo.

Chanzo: www.habarileo.co.tz