Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Viongozi wa dini wakemea wanaopanga maandamano

D0e7b5c57e3f323bba095c82a8636b0e Viongozi wa dini wakemea wanaopanga maandamano

Mon, 2 Nov 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

VIONGOZI wa madhehebu ya dini mkoa wa Dodoma wamewataka viongozi wakuu wa vyama vya siasa vya Chadema, CUF na ACT Wazalendo waende kwenye vyombo vya kisheria, kupinga matokeo siyo kuwataka wananchi kuandamana na kutoa kauli za uchochezi zinazoashiria uvunjifu wa amani.

Aidha viongozi hao wa dini wameviomba pia vyombo vya dola kuhakikisha vinadhibiti wanasiasa na wafuasi wanaochochea vurugu na kuharibu amani ya nchi, kwa kutaka kuandamana kutokana na kutoridhishwa na matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika wiki iliyopita.

Kauli hizo zilitolewa na viongozi hao wa madhehebu ya dini walipokuwa wakizungumza na waandishi wa habari mkoani hapa jana.

Askofu Mkuu wa kanisa la Philadelphia Gospel Assembly Tanzania na nchi za Ulaya na bara la Afrika, Dk Yohana Masinga alisema viongozi hao wa vyama wa siasa ambao hawajaridhika wanatakiwa kutafuta haki yao kwa kutumia vyombo vya sheria na siyo kwa kutaka kuingia barabarani kuandamana.

Alisema haki yoyote inapatikana kwa kutumia njia za kisheria husika ikiwemo mahakama na siyo kwa kuvuruga amani na utulivu uliopo. Pia wakumbuke kuwa kwenye ushindani lazima mmoja wapo ashinde na mwingine kushindwa.

Naye Shehe wa Mkoa wa Dodoma, Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Mustaph Rajabu alisema haki yoyote inapatikana kwa kutumia vyombo vya mahakama na siyo kwa kususia na kuleta chokochoko inayoashiria uvunjivu wa amani na kuhamasisha maandamano ya mitaani.

Shehe huyo alisema vyombo vya kisheria vipo na vimewekwa ili kutafuta haki, hivyo malalamiko yao wanapaswa kupeleka huko, si vinginevyo.

Aidha kwa upande wa Watanzania amewataka kujiepusha na kauli hizo zilizotolewa na viongozi hao kwani zinaweza kuhatarisha maisha yao, kinachotakiwa hivi sasa kufanya kazi kwa bidii ili kuiletea nchi maendeleo zaidi.

Kwa upande wake Askofu Mkuu wa kanisa la Pentekoste, Maombezi Tanzania, Living Mwambapa alisema kususia na kuandamana siyo dawa ya kufanyika tena kwa uchaguzi huo ambao uliofanyika kwa uwazi, haki na huru.

Alisema vyama hivyo vinatakiwa kujipanga tena kwa miaka mitano ijayo, kama wanahitaji kutaka nafasi hiyo ya ngazi ya urais na zinginezo za ubunge na udiwani, badala kuendelea kutoa malalamiko yao ambayo yaliyo mengine hayana tija kwa watanzania walio wengi wanaohitaji amani na utulivu kwa hivi sasa.

Askofu mstaafu wa kanisa la EAGT Ipagala, Evance Chande alisema Watanzania wanachohitaji ni kuwapata viongozi waliowachagua kwa masilahi ya maendeleo, hivyo walioshindwa wanatakiwa kutoa ushirikiano kwa walioshinda ili kuweza kuijenga nchi kwa pamoja badala ya kuchukiana.

Chanzo: habarileo.co.tz