Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Viongozi wa dini waja na matano 2022

085c3ff24f4e7393ac4fb8e46bebe6de.jpeg Viongozi wa dini waja na matano 2022

Sun, 2 Jan 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Viongozi wa dini jana katika ibada mbali mbali za kukaribisha mwaka 2022 wametaja mambo matano makubwa yanayostahili kufanyiwa kazi na Watanzania ili waweze kustawi na nchi kupaa kiuchumi.

Katika mahubiri yao walipeleka salamu za za kutaka fedha za mkopo miradi ya kimkakati ziombewe; Waumini kuliombea taifa, viongozi na amani; wananchi kuchukua hatua za kusamehe, kuondoa uchungu ili kuleta mshikamano wa kitaifa; kutoingia hofu ya kifo kwa magonjwa yaliyopo wakitambua kwamba maradhi yanapita na kutambua kwamba mwaka huu ni wa neena kinachopaswa watu ni kuwajibika katika nafasi zao.

Pia viongozi hao walisema kwamba mwaka huu ni wa neema tele kwa watu binafsi na taifa.

Sambamba na matumaini hayo, viongozi hao wamewataka waumini wao kufanya ibada kuombea taifa pamoja na fedha ambazo serikali inakopa kukamilisha miradi mikubwa ya kitaifa ili malengo hayo yatimie.

Katika mahubiri hayo pia ujumbe uliotawala ni kuwataka waumini kusamehe, kuachilia uchungu na badala yake wamshukuru Mungu kwa kuwavusha salama mwaka ulioisha na kuanza salama mwaka mpya.

Aidha waumini hao wamepaswa kuondoa hofu ya maradhi yanayoibuka kwani yamewafanya waishi kwa hofu ya kifo wakati uhalisia kuugua sio kufa na kuwataka wawe na tumaini jipya kwa sababu hata huo ugonjwa utapita na maisha yataendelea.

Katika mahubiri yaliyotolewa jana na Msaidizi wa Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania(KKKT)- Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Kanisa la Azania Front,Dar es Salaam, Chediel Lwiza alisema ni siku mpya inayopaswa kumshukuru Mungu na kuanza naye mwaka mpya.

Lwiza alisema mwaka huu waumini wanapaswa kuanza upya na kuondoa hofu ya maradhi yanayoibuka ambayo yanawafanya wananchi wawe na hofu ya kifo muda mwingi na kusema hiyo ni mbinu ya shetani kuwatoa kwenye tumaini la Mungu na kusema kuendelea kuishi mwaka huu ni Neema ya Mungu.

“Waumini tunapaswa kuondoa hofu ya vitu mbalimbali tunavyovihofia, yakiwemo maradhi haya ambayo mtu anaugua anawaza kifo, wakati kuugua sio kufa, tuwe na tumaini jipya Yesu alishinda na sisi tutashinda, tumepewa neema ya kuona mwaka mpya tumshukuru Mungu,”alisema.

Akihubiri kwenye Ibada ya Mwaka Mpya jana katika Kanisa ya KKKT-Usharika wa Kimara, Dar es Salaam, Mchungaji Kiongozi wa kanisa hilo, Wilbroad Mastai alisema mwaka huu mpya ni vyema waumini wakaachilia uchungu na kusamehe ili kuendelea mbele.

Alisema pamoja na kuomba Mungu kuachilia msamaha ni vyema pia waumini wakaanza kwa kumshukuru Mungu kuwavusha salama na kuomba mwaka huu uwe wa baraka na mafanikio zaidi.

“Kila mmoja ana mahitaji yake rohoni, lakini tuombe Mungu mwaka huu mpya tusamehe na kuachilia uchungu kwa sababu tunapoendelea kuwa na uchungu tunalalamika wakati wa kuomba badala ya kusali,”alisema Mchungaji Mastai.

Akihuburi katika Kanisa la Umoja CCT-Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika Ibada ya shukurani ya Mwaka Mpya, kasisi wa kanisa hilo, Mchungaji James Lubadanja alisema anatamani mwaka mpya kuona watu wanaoishi kwa tumaini na sio kuishi maisha ya mazoea.

Alisema katika mwaka uliopita kama kuna waumini waliishi kwa mazoea basi wabadilike na mwaka huu mpya waanze kuishi maisha ya matumaini yenye malengo huku wakimtanguliza Mungu.

Naye Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la KKKT-Usharika wa Magogoni ,Kigamboni Dar es Salaam,Prosper Kahangwa aliongoza waumini kumshukuru Mungu kuwavusha salama mwaka uliopita na kuomba aendelee kulivusha kanisa na taifa kwa viwango vingine mwaka huu.

“Mungu ametuvusha salama mwaka ulioisha, tunapaswa kumshukuru na tumuombe aeendelee kutuvusha kanisa na taifa mwama huu mkono wake ukaendelee kuwa nasi,”alisema Mchungaji Kahangwa.

Kutoka Dodoma, Watanzania wametakiwa kuombea fedha ambazo nchi inakopa kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo ili zitumike ilivyokusudiwa kwa maslahi ya taifa.

Askofu Mstaafu wa Kanisa la Evangelist Assemblies of God Tanzania (EAGT) Ipagala mkoa wa Dodoma, Evance Chande alisema hayo wakati akihuburi wakati wa mkesha wa kuukaribisha mwaka mpya 2022.

Aliwataka Watanzania kuombea fedha zinazokopwa na serikali kwa ajili ya kutekeleza miradi ya

maendeleo ikiwemo ujenzi wa miundombinu mbalimbali ili zitumike kama ilivyokusudiwa kwa maslahi ya taifa ili kusiwe na ubadhirifu wowote kwenye matumizi ya fedha hizo.

Askofu huyo mstaafu ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya maridhiano Mkoa wa Dodoma aliwataka Watanzania kuendelea kuombea amani ya nchi ili iendelee kudumu.

“Pia tuwaombee viongozi wa serikali, viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini ili watekeleze majukumu yao na kudumisha amani na utulivu uliopo nchini,”alisema.

Aidha aliwataka vijana kuacha tabia ya kukaa vijiweni huku wakilalamikia maisha magumu na badala yake wajishughulishe na shughuli za kiuchumi.

Chande alisema vijana hao wamekuwa wakikaa vijiweni huku wakiilamu serikali kutokana na kukosa ajira wakati suala la ajira lipo mikononi mwao hasa katika kilimo.

Alisema kitendo cha kuacha kujishughulisha na kuendelea kuilamu serikali haitawasaidia vijana ambao wanatakiwa kuchukua maamuzi ya msingi ya kuwaondoa katika umaskini.

“Inasikitisha kuona karibu vijana wengi wanaojihusisha na ulevi wa viroba(konyagi), wakati serikali inahimiza suala la kujiajiri ili kujipatia kipato,”alisema.

Aliwataka wazazi na walezi kuendelea kutoa elimu ya kuwafanya watoto kuwa na hofu na Mungu na kuacha kujiingiza katika matendo machafu.

Kwa upande wake, Mchungaji wa Kanisa la Ukombozi kwa Mataifa yote, James Singu aliwataka Watanzania kuendelea kuombea nchi ili iendelee kuwa na amani.

Akihuburi wakati wa

mkesha wa mwaka mpya uliofanyika katika kanisa hilo lililopo Ipagala alisema Watanzania waendelee kujiombea nchi Ili iwe na amani.

Naye Askofu Mkuu Mwandamizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Yuda Thaddeus Ruwa’ichi wakati wa Misa ya Mkesha wa mwaka mpya iliyofanyika katika Kanisa la Mtakatifu Joseph, aliwataka waumini kuvuna mwaka 2022 wenye neema na usio na huzuni.

Askofu Ruwa’ichi alisema kwa kuwa mwaka wa 2021 nchi ilikumbwa na changamoto kuu mbili ambazo ni ugonjwa wa Covid-19 kama ilivyokuwa kwa mataifa mengine lakini pia kifo cha Rais John Magufuli, matukio ambayo alisema kama mwaka wa 2022 wananchi wakiomba nchi inaweza kuvuka bila ya kukumbwa na janga lolote.

Alisema: “Wananchi wanapaswa kuishi kwa kumuomba Mungu na hii siyo kwa wakristo peke yake bali ni hata kwa wenye imani nyingine yani tunapaswa kuliombea taifa amani”.

“Taifa liwe huru dhidi ya majanga, huru dhidi ya magonjwa na tuiombee serikali kwa kila hali ili serikali ivuke na kuiendeleza jamii ya watanzania vema kwa mwaka wa 2022 na miaka ijayo.”

Amewataka watanzania kuombana msamaha kwa mabaya ambayo wamefanyiana mwaka 2021 na kumuomba Mungu neema zaidi kwa mwaka wa 2022 huku wakimshukuru kwa namna alivyobariki mambo mazuri kwa nchi na kwa mtu mmoja mmoja.

Alisema baraka za Mungu peke yake ndiyo zinaweza kulivusha taifa na watu wake na kuwa bila ya kuomba baraka za Mungu mengine yote ambayo wananchi watayafanya

yatakuwa hayana faida.

Alisema hata katika kazi na shughuli zozote za maendeleo ya mtu mmoja mmoja au taifa ni lazima kuomba Mungu kuwaepusha katika mazingira magumu na kuweka mazingira rahisi na rafiki ya kupata maendeleo.

“Wananchi msisahau kuwa mafanikio mnayopata au mliyopata au hata mnayotarajia kupata kwa mwaka wa 2022 ni bure na wala siyo lolote kama hakuna baraka za Mungu, ni yeye peke yake ndiyo anayefanikisha mafanikio haya hivyo ni lazima kumshukuru na kuzidi kumuomba,”alisema Askofu Ruwa’ichi.

HabariLEO pia baada ya misa hiyo ilitembelea sehemu mbalimbali za Dar es Salaam na kushuhudia hali ya utulivu huku wananchi wakisherehekea kwa amani.

Katika eneo la Tabata Bima katika baa kadhaa idadi ya wananchi ilikuwa kubwa ambapo walikuwa wakiburudika na muziki, katika eneo la Kariakoo na Upanga zilizisikika baruti hasa Upanga mtaa wa Mazengo na maeneo jirani, wananchi walikuwa wakisherehekea katika mitaa huku wengine wakiwa kwenye sehemu za kumbi za starehe.

Katika fukwe ya Dynast iliyopo Ununio nje kidogo ya Dar es Salaam wananchi walijumuika na kusherehekea muziki na fataki zilizokuwa zikirushwa eneo hilo ambapo kulikuwa hakuna kiingilio.

Pia katika hoteli ya Sea Cliff- Masaki wapenzi wa burudani pia walijumuika kwenye kumbi ya starehe ndani ya hoteli wa Mansion na kupata burudani kutoka kwa wachezesha muziki, Dj, mbalimbali.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live