Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Viongozi wa dini waiunga mkono serikali vita ya corona

44d1befa8c3210cf10193fb42bb96f50 Viongozi wa dini waiunga mkono serikali vita ya corona

Fri, 30 Jul 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

VIONGOZI wa dini wamesema wiki hii watatoa waraka rasmi wa kuiunga mkono serikali na kuhimiza waumini wao kuacha mzaha, bali wahakikishe wanazingatia miongozo ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona vinavyosababisha ugonjwa hatari wa covid-19 kama wanavyoelekezwa na wataalamu wa afya.

Wakizungumza na HabariLEO jana Dar es Salaam, Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dk Alex Malasusa alisema wameitikia wito wa serikali katika kuhimiza waumini kujikinga na virusi vya corona na kwamba wameshaanza kutoa maelekezo kwa usharika zake zote kuhakikisha ibada zinakuwa fupi na kuzingatia njia za kujikinga na corona.

"Kwa kweli tunaiunga mkono serikali katika hili la kupambana na corona, tumeshawaagiza wachungaji wetu wote kwenye sharika zetu kufanya ibada fupi na pia tumeahirisha makusanyiko yasiyo ya lazima," alisema Askofu Malasusa.

Alisema katika kudhibiti kusambaa kwa virusi vya corona, tamasha kubwa la uimbaji mwaka huu linaloandaliwa na kanisa hilo limesitishwa, lakini pia wamesambaza waraka kwa kila usharika kuwataka wachungaji wa sharika hizo kuhakikisha wanaepuka kutumia vipaza sauti kwa kushirikiana.

Alisema kesho viongozi wote wa dayosisi hiyo wakiwemo wachungaji watakuwa na warsha inayotolewa na madaktari kuhusu kujikinga na virusi vya corona na endapo watashauri hatua zaidi za kuchukua, kanisa litatii.

"Kesho kutwa (kesho) tuna warsha na madaktari wanakuja kutuelimisha na kutuelekeza kuhusu hatua za kuchukua kukabiliana na corona na endapo watatushauri hatua zaidi ikiwamo hata kusitisha ibada kama hali ni mbaya, tutatii," alisema.

Alisema kwa sasa wameagiza ibada za Jumapili kwa kila usharika ziwe fupi na kama kuna uhitaji wameruhusu ziongezeke kutoka mbili kwa siku hadi tatu au nne kama waumini ni wengi ili kuepusha msongamano kwenye ibada moja.

Aidha, aliwataka wananchi wote bila kujali imani zao kuacha ubishi na kuchukua hatua kwa kuvaa barakoa, kuepuka msongamano na kunawa mikono kwa maji na sabuni na kutumia vitakasa mikono ili kudhibiti kuenea kwa virusi hivyo.

Akizungumzia hatua zinazochukuliwa na Kanisa Katoliki Tanzania, Katibu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Dk Charles Kitima alisema wanaiunga mkono serikali kwa hatua iliyochukua kutangazia umma uwapo wa janga hilo na kuwa kesho watatoa waraka rasmi wa hatua za kuchukua kwa waumini wao na watausambaza kwa makanisa yote nchini.

"Jumanne hii (kesho) tuna kikao cha kujadili masuala ya corona, tukishamaliza kikao hicho cha tathmini tutatoa waraka na kuusambaza makanisa yetu yote ili viongozi wa parokia na waumini wauzingatie, lakini tunachoendelea kusisitiza ni kuzingatia maelekezo yote ya wataalamu wa afya na serikali," alisema Dk Kitima.

Alisema hivi sasa ibada zote wameelekeza zifanywe kwa ufupi huku tahadhari zote zikichukuliwa na kuwa wapo tayari kufuata maelekezo yote ya serikali ikiwa watatakiwa kufanya hivyo.

Kwa upande wake, Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata), limesema walishaanza kutoa hamasa na elimu kwa waumini wa Kiislamu juu ya kujikinga na virusi vya corona na kwamba katika hilo wamehimiza ibada ziwe fupi, huku likiwataka waumini kila mmoja kwenda na mswala wake msikitini.

"Tunahimiza uvaaji wa barakoa kwa waumini wetu wote, tumeelekeza muda wa ibada uwe mfupi na kila muumini aende msikitini na mswala wake, tumepiga marufuku kukumbatiana, corona ipo ni lazima tuchukue tahadhari kama serikali inavyosema," alisema Katibu Mkuu wa Bakwata, Nuhu Mruma.

Alisema leo watatoa waraka rasmi na kuusambaza kwenye misikiti yote nchini ili waumini waweze kuufuata kujikinga na corona na kuwataka waumini wote kuacha kupuuzia corona bali wavae barakoa na kufuata maelekezo yote ya wataalamu wa afya.

Hata hivyo Tanzania imejiunga rasmi na Mpango wa Kukabiliana na Maambukizi ya corona kwa Nchi Masikini (Covax),wa Shirika la Afya duniani WHO ili kukabiliana na janga hilo.

Kwa hatua hiyo, kunaipa nchi fursa ya kuingizwa kwenye mpango wa kupata chanjo za mpango huo mwaka huu na hivi karibuni Marekani imeipa Tanzania chanjo aina ya Johnson&Johnson dozi milioni 1.058,400 .

Balozi wa Marekani nchini Tanzania ,Donald J Wright alisema wanasambaza chanjo hizo ili kuokoa maisha na kuongoza dunia katika harakati za kuangamiza ugonjwa huo.

Wanawake wajasiriamali wadogo nchini walisema serikali itakapoanza kutoa chanjo ya corona, watakuwa wa kwanza kuikimbilia kwani ni mkombozi wa afya zao na familia zao.

“Tunasubiri chanjo ianze, sisi tutachanjwa kwa sababu tunafanya biashara ndogo ndogo kwenye msongamano wa watu, kuambukizwa corona ni rahisi, hivyo ili tujikinge chanjo ikitoka tu, tutakuwa mstari wa mbele kuchanjwa,alisema Maria Modesti mfanyabiashara wa mbogamboga soko la Mabibo,Dar es Salaam.

Julai 25,mwaka huu akitangaza mwongozo mpya wa 17 wa kukabiliana na ugonjwa huo Dar es Salaam Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maende1leo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Profesa Abel Makubi alisema hatua hiyo pamoja na mambo mengine imelenga kukata mnyororo wa maambukizi katika ngazi ya kaya na jamii bila kuathiri shughuli za kiuchumi.

Kuhusu hali ilivyo ya corona nchini Tanzania, Waziri wa Afya, Dk Dorothy Gwajima alisema hadi sasa zaidi ya watu 29 wamefariki kwa ugonjwa huo huku wengine zaidi ya 858 wakiugua na kusisitiza wananchi kuendelea kuchukua tahadhari ikiwemo kupata chanjo ya corona mara itakapozinduliwa.

Chanzo: www.habarileo.co.tz