Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Viongozi wa dini wahimizwa kuhamasisha chanjo

5195c49e113ed755a842f7b9d749b0f6.jpeg Viongozi wa dini wahimizwa kuhamasisha chanjo

Fri, 17 Dec 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

Viongozi wa dini mkoani Tanga wametakiwa kuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha umuhimu wa chanjo ya Covid-19 katika nyumba za ibada na mikusanyiko ya kidini.

Rai hiyo ilitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Hashim Mgandilwa wakati wa kikao cha uhamasishaji na elimu ya umuhimu wa chanjo dhidi ya ugonjwa wa corona kwa viongozi wa dini kilichoandaliwa na Shirika la Amref kupitia Mradi wake wa Afya Kamilifu.

Alisema viongozi hao wana dhamana kubwa ya kunusuru jamii waliyonayo katika kudhibiti maambukizi mapya kwa kufanya uhamasishaji kuhusu chanjo na kuona jambo hilo kama ni sehemu ya wajibu wao kama ilivyo katika kuhubiri neno la Mungu.

“Niwaombe, mkazitumie nyumba za ibada katika kuwaelimisha waumini wenu kuhusu kutumia chanjo ili waweze kujikinga dhidi ya ugonjwa huo lakini na kuisaidia serikali katika vita hii ya Covid-19,” alisema DC Mgwandilwa. Aidha, aliwataka kutumia nafasi zao katika kuwaeleza waumini wao umuhimu wa chanjo hiyo na kuwa sehemu ya mabalozi wa kueleza faida ya chanjo hiyo ili kuondoa dhana potofu juu ya chanjo hiyo iliyopo kwa jamii.

“Wakati mnapofanya mawaidha au kuhubiri neno lazima kuhakikisha mnahamasisha waumini wenu lakini na nyie kuwa sehemu ya mfano kwa kushiriki kupata chanjo kwa hiari kwa kufanya hivyo mtawashawishi jamii yenu lakini na kuisaidia serikali katika jambo hilo,” alisema.

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa, Dk Jonathan Budenu alisema kuwa takwimu zinaonyesha mkoa huo una jumla ya watu milioni 2.5 na lengo la mkoa ni kuhakikisha wanaweza kuwafikia watu milioni 1.5. Alisema kuwa mpaka sasa dozi ya awamu ya pili ambayo ilikuwa ni dozi 46,000 ambazo zililetwa zimebaki dozi 26,000 hivyo kupitia mkutano huo ana imani mpaka ifikapo mwishoni mwa mwaka huu watamaliza kiasi kilichobaki.

“Chanjo kwa sasa inapatikana kwa urahisi kwani tumeweza kuongeza vituo hadi kufikia 362 na inapatikana bila ya gharama yoyote, kinachotakiwa ni kutusaidia kuwahamasisha wananchi hususani wale walio katika umri hatarishi kupata chanjo,” alisema Dk Budenu.

Hata hivyo, Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Amref, Dk Florence Temu alisema kuwa wao kama shirika kupitia Mradi wao wa Afya Kamilifu wanaunga mkono juhudi za serikali za kupambana na Covid-19 kwa kuendelea kuhakikisha jamii inachukuwa tahadhari lakini na kupata chanjo kwa hiari ambazo zipo kwenye vituo mbalimbali vya afya.

Chanzo: www.habarileo.co.tz