Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Viongozi Katoliki Rombo wafunga siku tisa jamii iondokane na ulevi

49311 Viongozipic

Fri, 29 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Rombo. Viongozi wa Kanisa Katoliki wilayani Rombo wameanza kufunga kwa siku tisa kumuomba Mungu aiepushe jamii wilayani humo na tabia ya ulevi uliopindukia hususan kwa vijana.

Kwa mujibu wa viongozi hao, vijana wengi wanashindwa kuoa kutokana na ulevi.

Mkuu wa Vikarieti ya Rombo na paroko wa Usseri, Padri Emmanuel Lyimo alisema wameamua kufunga ili kukisaidia kizazi hicho kiweze kupenda kazi kuliko unywaji pombe.

Alisema Tanzania inapoteza vijana wanaotegemewa kushiriki katika shughuli mbalimbali za ujenzi wa uchumi wa Taifa.

Paroko huyo alisema kukithiri kwa unywaji wa pombe haramu katika wilaya hiyo kunatokana na vijana wengi kutokuwa na kazi za kufanya, badala yake wanaishia kwenye vilabu vya pombe na hatimaye kushiriki katika matukio mbalimbali ya uhalifu.

Kiongozi huyo wa dini aliiomba Serikali kuanzisha vikundi vya ujasiriamali ili kupunguza uzururaji wa vijana pamoja na vitendo vya uhalifu ikiwemo mauaji.

Related Content

“Ni lini Serikali itakomesha unywaji wa pombe haramu pamoja na mauaji yasiyo na hatia Rombo?” alihoji paroko huyo.

“Serikali endapo itaanzisha vikundi vya ujasiriamali, haya matukio ambayo yanaendelea kwa sasa hayatakuwepo, kanisa tupo tayari kupitia jumuiya ndogo ndogo kuwakusanya vijana ili iwe rahisi kuwafikia walengwa.”

Alisema, “yapo makundi mbalimbali ya vijana yameibuka katika wilaya hii, wanavunja na kuchoma nyumba za watu, kupora pamoja na kuua. Hii hali kiukweli inasikitisha.”

Padri Lyimo alisema kutokana na hali hiyo waumini wa kanisa hilo wameamua kufunga na kuomba ili Mungu ainusuru jamii na matukio ya kihalifu yanayotokea.

Kiongozi wa jumuiya ya kanisa hilo, Athanas Joseph alisema wameamua kufunga baada ya kuchoshwa na matukio ya kihalifu yanayosukumwa na ulevi kupindukia miongoni mwa vijana.

“Sasa hivi hakuna vijana wanaooa, wengi wameishia kunywa pombe haramu, vijana wengi unakuta wanakunywa pombe aina ya gongo na mbundimbundi ambazo zinawamaliza nguvu kabisa,” alisema.

“Hapa kuoa hawawezi kabisa na mwisho wake baada ya muda kijana wa miaka 20 utafikiri ni mzee wa miaka 60.”

Aliitaka Serikali kuangalia namna ya kuwanusuru vijana wilayani humo kwa sababu wanaangamia.

“Kizazi kijacho hatutakuwa na vijana imara katika wilaya hii, tunaomba Serikali itusaidie kuwapatia vijana hawa mtaji angalau wajiingize katika shughuli mbalimbali za ujasiriamali,” alisema Joseph.

Kwa mujibu wa wakazi wa wilaya hiyo, kuna zaidi ya aina 52 za pombe za kienyeji zinazonywewa wilayani humo.

Mmoja wa wakazi hao, Alfred Martin aliliambia Mwananchi kuwa kutokana na wingi wa pombe hizo na jamii kutokuwa na mbinu madhubuti za kudhibiti unywaji kupita kiasi, inakuwa rahisi kwa vijana kujiingiza katika tabia hiyo.

“Labda tu itokee kwamba kuna mkakati maalumu, lakini vinginevyo iwe ni maombi na ibada ili Mungu atusaidie,” alisema.



Chanzo: mwananchi.co.tz