Dar es Salaam. Kama ni mfuatiliaji wa mitandao ya kijamii nchini Tanzania lazima utakuwa umekumbana na neno ‘upepo wa kisulisuli’.
Neno hilo limekuwa maarufu na sasa umekuwa kama utani, kwani wapo wanahusisha mambo yao kwenda sawa kama kasi ya upepo wa kisulusuli.
Neno hilo limekuwa maarufu baada ya video iliyosambaa mitandaoni kumuonyesha mchungaji kiongozi wa kanisa la Mlima wa Moto, Dk Getrude Rwakatare akiwaita madhabahuni wanawake na wasichana ambao hawajaolewa ili awafanyie maombi na watawapata wenza wao kwa “upepo wa kisulisuli.”
Neno Kisulisuli lipo katika Biblia takatifu katika kitabu cha Hesabu likiwa na maana ya muujiza.
Maana hiyo ndiyo iliyomfanya mchungaji Rwakatare kulitumia kuwaombea wanaohitaji kupata wenza.
“Nimefurahi maana nimeona ujumbe umefika kwenye jamii na umewagusa wanawake na wanaume kwa kuwa tatizo hilo lipo na pande zote zina uhitaji.”