Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: Maombi ya kukesha ni silaha ya kukuokoa na majanga yanayoweza kutokea kesho

VIDEO: Maombi ya kukesha ni silaha ya kukuokoa na majanga yanayoweza kutokea kesho

Mon, 11 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Halleluya Halleluya, Jina la Bwana libarikiwe.

Naitwa Nabii Richard Godwin kutoka kanisa Jehova Mercy, Swaswa jijini Dodoma.

Jumapili ya leo nakuletea neno la Mungu nikikufundisha kuhusu faida za maombi siyo maombi ya kawaida ila maombi ya mkesha.

Napozungumza faida za maombi unaweza tazama harakaharaka, kikawaida hakuna asiyejua faida za maombi kwamba unapoomba unazungumza na Mungu wako kuhusu mambo mbalimbali ikiwemo mahitaji yako unayotaka kusaidiwa naye.

Watu wengi wamekuwa wakienda kanisani kufanya mikesha, lakini hawajui faida zake, hawajui kwa nini wanaenda kukesha na kuomba.

Neema ya Mungu ikufunike unaposoma ujumbe huu ukusaidie kuanza kuomba kwa kukesha. Kumbuka pia tupo katika kipindi cha Kwaresma kuelekea Pasaka yaani kufa na kufufuka kwa Yesu Kristo.

Sasa naomba tusome Biblia katika kitabu cha Marko 14.38 neno la Mungu linasema “Kesheni muombe, msije mkaingia majaribuni kwa kuwa roho i radhi lakini mwili ni dhaifu.”

Kwa hiyo faida ya kukesha na kuomba ni kukusaidia usije ukaingia majaribuni kwa sababu mwili ni dhaifu.

Kwa hiyo maombi ya mkesha yanakusaidia usije kuingia majaribuni kwa sababu unapokesha unapata muda mrefu sana wa kuzungumza na Mungu wako kuhusu mambo yako.

Unapokesha unatumia walau saa nane mpaka 10 ya kuweza kutafakari na kuomba mambo yote muhimu uliyotaka kuzungumza na Mungu. Yesu alipokuwa na wanafunzi wake aliwakumbusha kuhusu maombi ya kukesha kwa sababu alijua wazi miili yao ni dhaifu japo roho zao zipo radhi kupambana na majaribu.

Hii ina maana kama wasingekesha wangeweza kuingia majaribuni.

Tusome pia kitabu cha Matendo ha Mitume 16:24, neno la Mungu linasema “Naye akiisha kupata amri akawatupa katika chumba cha ndani akawafunga kwa mkatale, lakini usiku wa manane Paulo na Sila walikuwa wakimuomba Mungu na kumuimbia nyimbo za kumsifu huku wafungwa wengine wakiangalia.”

Paulo na Sila waliomba usiku wa manane wakimwambia Mungu kuhusu mateso waliyo nayo na hapa walikuwa wanakesha. Wakati walipofanya hivyo ipo faida ambayo waliipata.

Biblia inaendelea kusema kwamba ghafla pakawa na tetemeko kuu la nchi hata misingi ya gereza ikatikisika kisha milango ya gereza ikafunguka nao wakatoka.

Faida nyingine hiyo ya maombi ya mikesha kwamba unapoomba misingi ya gereza ulilofungwa inatikisika.

Inawezekana upo kwenye gereza kubwa la umaskini japo unafanya kazi kwa bidii lakini hufanikiwi.

Inawezekana pia upo magereza mengine mengi kama magonjwa, kukata tamaa, kukataliwa hata na ndugu zako sasa unaweza kufanikiwa kupata muda mrefu wa kuzungumza na Mungu yaani kukesha. Kuna wengine tangu walipokuwa tumboni mwa mama walinenewa mabaya kwamba hawatafanikiwa, hivyo ni muhimu uchukue hatua kwenda kanisani kwako wakati wa mikesha upate muda wa kuzungumza na Mungu.

Misingi ya magereza inapolegezwa hata ajira iliyokuwa ngumu kupatikana utaipata tu kwa sababu umeongea na Mungu.

Msomaji wa Mwananchi kuna wakati biashara zako haziendi, kuomba kwa kukesha ni ufunguo wa mpenyo wa kibiashara. Kwenye maisha ya kawaida kuna maadui wa mafanikio yetu ambao wanatamani kuona upo palepale kimaisha, hicho ni kifungo kikubwa kwa walio wengi na utakivuka tu ukiamua kutenga muda wa kuzungumza na Mungu wako.

Maombi ya mkesha hukusaidia wewe kugeuza silaha za adui zako. Yaani yale mabaya waliyotaka yakutokee huwa yanawageukia wao wenyewe.

Silaha iliyotegwa kukumaliza huwa inaenda kuwamaliza wao wenyewe na wakati wanashangaa imekuwaje, Mungu anakufanikisha.

Napenda kukushauri msomaji wetu kwamba ni wakati wako kutenga walau siku moja kwa mwezi kufanya maombi ya mkesha. Wakati mwingine siyo lazima uwe na majaribu ndipo ukeshe na kuomba hapana, unaweza fanya hivyo kwa ajili ya mambo yako ya baadaye.

Omba ulinzi wa familia yako hasa ulinzi wa watoto kulingana matukio yaliyopo. Mungu wetu ni mwaminifu sana, yeye husikia na kulegeza vifungo vya yale tuyaombayo.

Hapa simaanishi ukiomba muda mfupi hakuna faida, hapana. Naamani sana update muda mrefu wa kukaa karibu na Mungu ukimueleza mambo mbalimbali.

Ndugu yangu msomaji jua jambo lolote baya shetani alilopanga kukufanyia utaweza kulipangua kwa kuomba na kukesha.

Maombi

Baba katika Jina la Yesu Kristo ninaomba kwa ajili ya msomaji wa gazeti la Mwananchi mpe kiu na nguvu ya kuwa muombaji kwenye mikesha.

Ninaomba kwa ajili ya uongozi wa Mwananchi kwa kufungua milango ya watu kujifunza neno la Mungu na kila anayesoma apate baraka, amen.



Chanzo: mwananchi.co.tz