Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: Maaskofu wanena

Video Archive
Sat, 28 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar/mikoani. Amani, haki na maridhiano ni miongoni mwa salamu zilizotolewa na viongozi wa dini katika sikukuu ya Krismasi wakisihi waumini na jamii wazingatie hayo pasipo kujali vyeo au madaraka ili kudumisha umoja ndani ya Taifa.

Viongozi hao wa kiroho walitumia ibada za mikesha na ile ya jana asubuhi kwenye sikukuu ya Krismasi kukemea binadamu kutesa wenzao, matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii yanayoweza kuliangamiza Taifa, kusamehe watu wengine pamoja na kufanya kila linalowezekana kwa ajili ya kutenda haki.

Ujumbe mwingine ambao waliutoa viongozi hao unahusu uchaguzi mkuu mwakani, ambapo waliliombea Taifa kuvuka salama pamoja na kuwasisitiza wananchi kujitokeza kujiandikisha kwa wingi katika daftari la wapiga kura.

Nasaha za viongozi hao wamezitoa kipindi ambacho kumekuwa na mjadala wa uwapo wa maridhiano ya kitaifa. Mjadala huo ulikolezwa zaidi katika sherehe za miaka 58 ya Uhuru wa Tanganyika zilizofanyika Desemba 9 jijini Mwanza.

Katika sherehe hizo, wenyeviti wa Chadema na CUF, Freeman Mbowe na Profesa Ibrahim Lipumba walitumia muda mfupi waliopewa na Rais John Magufuli kutoa salamu wakisema, kiongozi huyo mkuu nchi ana wajibu wa kujenga demokrasia.

Mbowe alimuomba Rais Magufuli kutumia nafasi na dhamana yake kulinda demokrasia, haki na usawa kwa wote ili kuondoa hisia ya kuwapo kundi linalofurahi na jingine linalolalamika.

Viongozi wa dini, wasomi na wachambuzi wa masuala ya kisiasa na kijamii, waliunga mkono hoja ya kuwapo kwa maridhiano ya kitaifa miongoni mwa wanasiasa na makundi yote ya kijamii kama njia ya kulinda, kudumisha, kuendeleza na kuenzi amani, mshikamano na undugu miongoni mwa wananchi.

Jana, Askofu wa Jimbo la Kanisa Katoliki Mbinga mkoani Ruvuma, John Ndimbo akihubiri kwenye misa ya Kitaifa ya Krismasi iliyofanyika Kanisa Kuu la Mtakatifu, Kiliani Mbinga alisema ili kuwa wakala wa amani, upatanisho na utulivu ni lazima kusamehe watu wengine na kufanya kila linalowezekana kwa ajili ya kutenda haki.

“Tunasali siku zote Mungu utusamehe makosa yetu kama tunavyowasamehe wenzetu waliotukosea, tungetegemea kwa sala hii pasiwe na maovu na ukorofi,” alisema Askofu Ndimbo.

Alisema jamii inayosameheana inakuwa na utulivu tofauti na wasiosameheana inakuwa na mitafaruku na vurugu.

Katika siku hii ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo, Askofu Ndimbo alisema Mungu amempa kila binadamu utu ambao hautakiwi uharibiwe na lolote litakalofanywa kinyume na utu ni chukizo kwa Mungu.

“Tutakuwa wakala wa vyombo vya amani pale tunapouishi ukweli huo kwamba amani ni tunda la haki. Tutakapojali haki ya kuishi katika kila mmoja wetu tutaishi kwa utulivu, tutakuwa katika amani, tutaishi kwa matumaini,” alisema Askofu Ndimbo.

Alisema endapo haki ya kuishi ikiingiliwa mara zote huwa ndio chanzo cha vurugu, hivyo ametaka kusaidiwa kwa wasiojiweza na kuhakikisha kila mmoja anapata haki stahiki ya afya na elimu.

“Popote pale patakapofumbiwa macho suala la afya na elimu tunatengeneza matatizo. Jamii isiyoelimika ni tatizo kwa jamii, jamii isiyo na afya ni tatizo pia,” alisema Askofu Ndimbo.

Askofu Ndimbo alisema mawaziri wameonekana kwenye vyombo vya habari wakilalamikia watendaji wasio waaminifu katika matumizi ya fedha, wanafanya ubadhirifu wa fedha zinazoelekezwa kwenye miradi na amefafanua wanayofanya vitendo hivyo wanajitendea haki binafsi.

“Lakini najiuliza hao ambao wanalalamikiwa kwamba wabadhirifu ndiyo hao tunaosali nao pamoja? Tunakuta ndio hao wanaoharibu miradi na wanaenda makanisani,” amesema Ndimbo.

Naye Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi Mashariki Ziwa Victoria, Andrew Gulle aliwataka wananchi kutumia sikukuu hiyo kama sehemu ya kurejesha mtangamano amani, haki, faraja na upendo vilivyopotea kwenye jamii.

Akihubiri kwenye Ibada ya Sikukuu ya Krismasi, usharika wa Imani Kanisa Kuu jijini Mwanza, Askofu Gulle alisema ujumbe wa kuzaliwa Yesu Kristo unataka watu wapendane bila chuki.

Alisema kwa sasa manung’uniko, kuumizana na dhuluma vimekuwa vingi hivyo hakuna budi kurejesha furaha iliyopotea.

Askofu Gulle alisema kwa sasa chuki kati ya wanasiasa inapanda, jamii, mtu na mtu na wengi wamekosa haki kwa ajili ya manyanyaso hivyo watumie wakati huu kurejesha amani katika familia na taifa kwa ujumla.

“Wakati huu, thamani ya utu inapungua, Yesu anakemea hali hiyo akisema haki itande kati yetu,” aliongeza.

Askofu Gulle amewataka watu wenye mamlaka kutenda haki, “watu wamekandamizwa, wamekosa thamani na kuumizwa, Yesu anapokuja anataka kukaa ndani mwetu tuwe na amani na upendo, ujumbe wake ni kuwapenda wengine.”

Majaji, mahakimu waonywa

Katika hatua nyingine, Mkuu wa KKKT, Askofu Frederick Shoo amewageukia polisi wanaopeleleza kesi, mahakimu na majaji, akiwataka kusimamia ukweli na haki katika majukumu yao.

Askofu Shoo ambaye pia ni Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa hilo alienda mbali na kuwataka watu wenye mali na vyeo katika jamii kuacha kiburi na majivuno.

Akitoa mahubiri jana katika Kanisa Kuu lililopo Usharika wa Moshi mjini, Manispaa ya Moshi alisema, “mtu ambaye umempokea Yesu unapaswa kuuchukia uovu, unahitaji kukemea dhambi, unahitaji kukataa uovu wa aina yoyote. Krismasi hii ikawa nafasi ya kwangu na kwako kutubu.”

“Na hapa kipekee napenda kutoa ujumbe kwa wenzangu wanaohusika katika kupeleleza kesi za watu, mahakimu na majaji. Simamieni ukweli, simamieni haki,” aliomba.

Askofu Shoo alisema kuna vilio vya watu wanaobambikiziwa kesi, vilio vya familia zao na wako ambao wamehukumiwa pasipo kweli kutenda kosa.

“Vilio hivi Mungu anavisikia kama alivyosikia kilio cha wana wa Israel,” alisema.

Kiongozi huyo amewataka wenye mamlaka wafahamu wajibu wao ni kusimamia haki, kusimamia ukweli kwani maandiko matakatifu yanasema watawajibika kwa Mungu pale wakiupindisha ukweli na kutoa hukumu zisizo za haki.

“Mungu awasaidie sana ndugu zangu hawa (polisi, mahakimu na majaji). Ninatambua katika jamii yenye changamoto nyingi kwa wengi inaweza kuwa majaribu lakini tunahitaji msaada wa Mungu,” aliongeza Askofu Shoo.

Akinukuu Zaburi ya 131, Askofu Shoo alisema mtunga zaburi alitambua binadamu anaishi kwa neema ya Mungu hivyo moyo wake hautakiwi kuwa na kiburi wala kujivuna na kuwa na kiburi.

“Kwa watu ambao mmempokea huyu Yesu, hakuna sababu ya kuwa na kiburi, hakuna sababu ya kujivuna. Mali na nafasi katika jamii, cheo vinaweza kukufanya ukajisifu ukawa na kiburi,” alionya.

Onyo mitandao ya kijamii

Askofu wa Kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la Kusini Magharibi, Alinikisa Cheyo alionya wale wote wanaotumia mitandao ya kijamii kuandika mambo machafu na kutukana wengine wanahatarisha amani ya nchi.

Askofu Cheyo alisema hayo jana wakati akitoa salamu za Krismasi ibada ya Kanisa la Moravian Vwawa mjini wilayani Mbozi mkoani Songwe, alisema amani na umoja wa nchi unapaswa kulindwa na kila mmoja ili watu waweze kufanya kazi ya kujiletea maendeleo yao na ya nchi kwa ujumla.

“Wapo wenzetu ambao wanatumia vibaya elimu na uhuru wa habari kuharibu amani yetu, aidha kwa kutumika na watu wasioitakia mema nchi yetu na hao nawaambia nchi hii ndiyo tuliyopewa na Mungu tunapaswa kuilinda,” alisema Askofu Cheyo.

Askofu Cheyo alitumia pia nafasi hiyo kutuma salamu za kumtakia heri Rais wa Tanzania, John Magufuli kwa kazi njema ya kuliongoza Taifa hili.

Kiongozi huyo wa kiroho aliwataka wananchi kuthubutu kufanya kazi za kuwaletea maendeleo badala ya kuendelea kulialia kuhusu hali ngumu ya maisha.

“Watanzania wakati mwingine wanaogopa kuthubutu kuwekeza ili wazalishe, hata Yesu alisema mbegu ikianguka chini ikafa haiwezi kuzaa, msije mkaondoka hapa duniani bila kuacha alama ya ukumbusho, nalisema hili hasa kwa vijana ambao wengi wao wanapenda kulala bila kufanya kazi, hii si hali nzuri,” alisema Cheyo.

...Wajitathmini, kusaidiana

Askofu Mkuu Thadeus Ruwa’ichi wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam alishauri kila mwananchi na Taifa kwa ujumla kujitathmini maisha aliyoyaishi mwaka 2019 kabla ya kuingia mwaka mpya 2020.

Askofu Ruwa’ichi aliyeongoza misa ya mkesha na ya asubuhi jana Kanisa la Mtakatifu Joseph, Dar es Salaam alisema, “tunapoelekea kuhitimisha mwaka huu na kuanza mwaka ujao 2020, itakuwa ni fursa ya kujitathmini tulivyoenenda 2019 na kujitahidi kupambanua malengo, mipango na vipaumbele vyetu ili tupige hatua katika maisha yetu.”

“Niwaalike Watanzania na waumini wote kuzingatia hitaji la umoja, mshikamano, bidii na uwajibikaji katika majukumu ya kila siku, pia ni muhimu kujiwekea malengo yaliyo mema,” alisema huku akioongeza, “Tutambuane na kubebana katika safari ya maisha yetu.”

Naye Mchungaji wa usharika wa Kihonda wa KKKT mkoani Morogoro, Isaya Kairanga alisema sasa ni wakati wa wananchi kujitafakari kwa mienendo yao katika kipindi cha kusherehekea sikukuu ya Krismasi.

Akihubiri ibada ya mkesha juzi usiku, alisema ni jambo la kushangaza kuona watu wakifanya mikesha katika sehemu za starehe na kusahau kumwabudu Mungu aliyewawezesha kufikia walipo.

Mchungaji huyo aliwataka wazazi na walezi kutochoka kutoa malezi mema kwa watoto wao hasa kipindi hiki cha utandawazi kwani vijana wengi wameonekana kukengeuka kimaadili.

Naye Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Morogoro, Telesphory Mkude aliwataka waumini wa dini ya kikristo kusherehekea kwa amani na upendo na kuwakumbuka watu wenye ulemavu na wengine wenye mahitaji maalumu.

Alisema wakati waumini wakisherekea kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo lazima waadhimishe amani ya nchi kwa kuwa hata Yesu Kristo alisisitiza uwapo wa amani.

Mmoja wa waumini waliohudhuria ibada hiyo, Nuruel Mapunda alimshukuru Rais Magufuli pamoja na viongozi wengine wakuu wa nchi kwa kusimamia amani na maendeleo ya nchi.

Mwaka wa uchaguzi

Viongozi hao wa kiroho walizungumzia pia uchaguzi mkuu mwakani wakiwaomba wananchi kujitokeza kujiandikisha katika daftari la wapiga kura.

Msimamizi wa Jimbo la Kanisa Katoliki Moshi mkoani Kilimanjaro, Padre Deogratius Matika akihubiri kwenye misa ya mkesha alisema, “katika kuadhimisha sikukuu ya kuzaliwa kwake Yesu Kristo, tunaelekea mwaka wa uchaguzi, tunaomba katika sala tuiombee nchi yetu tupate viongozi wema na wenye upendo na kuleta utulivu na ushirikiano.”

Naye Askofu wa Anglikana Dayosisi ya Dar es Salaam, Jackson Sosthenes aliwahamasisha wananchi kujiandikisha kwenye daftari la wapiga kura akisema mwaka 2020 ni muhimu kwa Taifa kwa kuwa linakwenda kwenye uchaguzi mkuu.

Askofu Sosthenes alitoa kauli hiyo jana wakati akitoa salamu na ujumbe wa sikukuu ya Krismasi wakati akiendesha ibada katika Kanisa la Anglikana la St Alban’s lililopo Posta, Dar es Salaam.

Aliwaambia waumini wa kanisa hilo na wananchi kuwa mwaka 2020 kutakuwa na uchaguzi wa kuwachagua viongozi kuanzia ngazi ya udiwani, ubunge na urais, ni vyema wakajiandikisha na kupata fursa kuchagua viongozi makini na wenye sifa kwenye mchakato huo.

“Kanisa la Anglikana Dar es Salaam linahamasisha watu kujiandikisha na tunawatia moyo wagombea nafasi mbalimbali kwenye uchaguzi huo. Ni vyema pia wananchi wakawachagua viongozi bora wenye hekima na walio na utayari wa kuwatumikia.

“Kinachomfanya mtu aitwe kiongozi ni namna anavyowaongoza watu wake. Kiongozi imara si yule anayetoa hotuba nzuri na kupendwa bali anayetekeleza matarajio ya wananchi wake,” alisema Askofu Sosthenes.

Uchu wa madaraka, uonevu

Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Shinyanga, Liberatus Sangu yeye aliwataka wananchi kuliombea Taifa liondokane na tatizo la uchu wa madaraka, uonevu na tamaa ya kujilimbikizia mali na utajiri aliyosema ni miongoni mwa sababu zinazochochea machafuko na mauaji katika nchi mbalimbali duniani.

Askofu Sangu akitoa mahubiri wakati wa misa ya mkesha wa Krismasi, alisema mifarakano ya uchu wa madaraka katika jamii husababisha machafuko na adha kwa wananchi wasio na hatia ikiwa ni matokeo ya watu wengi kukengeuka na kuacha mafundisho mema ya imani zao za dini.

“Vitendo hivi ni matokeo ya kumruhusu shetani kutawala maisha ya mwanadamu. Watu wanaiba, wanashiriki vitendo vya rushwa, wanauana na kudhulumu kwa sababu ya tamaa ya madaraka, mali na utajiri. Lazima tutumie kuzaliwa kwa Kristo Yesu kukataa dhambi hizi,” alisema.

Alisema amani imepungua kuanzia ngazi ya familia na jumuiya ambako kunashuhudiwa mifarakano mingi, kuna unyanyasaji wa wanawake na watoto, kudhulumu wajane na watoto yatima, mambo aliyosema hayaakisi upendo, mshikamano na undugu wa Kikristo ambao pia unafundishwa katika imani zote za dini.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti baada ya mahubiri hayo, waumini Paulina Mihayo na Julius Maziku waliwaomba wananchi; kila mmoja kwa nafasi na eneo lake kushiriki kupiga vita viashiria vyote vya uonevu, ubaguzi na dhuluma ya haki na mali kwa sababu vitendo hivyo vikishamiri huondoa amani na utulivu katika jamii.

Unyanyasaji wa wanawake

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma, Mhashamu Beatus Kinyaiya aliwataka wanandoa na jamii kuacha tabia ya kuwanyanyasa wanawake, kwani kufanya hivyo ni kukiuka haki za binadamu.

Kinyaiya aliyasema hayo katika ibada ya mkesha wa iliyofanyika katika Kanisa Kuu Katoliki la Paulo wa Msalaba lililopo jijini Dodoma na kusema matukio ya unyanyasaji wa wanawake yamekuwa yakitokea katika jamii kila mara.

Alisema inasikitisha kuona mwanaume anamnyanyasa mkewe licha ya kuwa aliahidi mbele ya madhabahu kuwa ataishi naye kwenye shida na raha, akiwataka kukumbuka viapo vyao vya ndoa.

“Tumekuwa tukisikia malalamiko mengi juu ya unyanyasaji wa wanawake katika ndoa jambo hilo si zuri kwa mnaofanya hivyo mnapaswa kuacha kwani halileti picha nzuri mbele ya jamii inayotuzunguka. Nawaomba wenye tabia hiyo mtumie sikukuu hii kufanya mabadiliko ndani ya mioyo yenu,” alisema Askofu Kinyaiya.

Hata hivyo, alisema sikukuu hii itumike kuwabadilisha wanafamilia ili kuendana na maadili yaliyo mema, hususani kufuata sheria na taratibu zilizowekwa hapa nchini ikiwemo kupinga unyanyasaji wa kijinsia.

Alisema hakuna sababu ya kwenda kinyume na maadili, hivyo kinachopaswa ni kutenda matendo mema ya kumpendeza Mwenyezi Mungu kila inapoitwa leo.

Kwa upande wake, Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Central Tanganyika (DCT), Dk Dickson Chilingani aliwataka wananchi kuitumia sikukuu hii ya kuzaliwa Yesu Kristo kama siku ya kutenda mema badala ya kugeuza kuwa siku ya kufanya vurugu.

Askofu Chilingani alitoa kauli hiyo jana wakati akihubiri kwenye Kanisa Kuu la Roho Mtakatifu jijini Dodoma ambapo alisema ibada njema ni ya watu wanayoishi kwa mema ambayo Yesu Kristo aliagiza.

Alisema amani ni sehemu ya maandiko ambayo Yesu Kristo mwenyewe aliagiza hivyo watu wakiitunza watakuwa wanamuenzi.

Imeandikwa na Kelvin Matandiko, Bakari Kiango, Muyonga Jumanne, Elizabeth Edward (Dar), Stephano Simbeye (Mbozi), Jesse Mikofu (Mwanza), Stella Ibengwe (Shinyanga), Daniel Mjema na Florah Temba Janeth Joseph (Moshi), Nazael Mkiramweni, Habel Chidawali (Dodoma), Lilian Lucas na Hamida Shariff (Morogoro).

Chanzo: mwananchi.co.tz