Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: Krismasi ni ukaribu kati ya mwanadamu na Mungu, ni wakati wa kuimarisha imani

Video Archive
Sun, 23 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Naitwa Askofu Jackson Sosthenes Jackson wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dar es Salaam. Kabla ya kuanza mahubiri, tuombe. Mungu mwenye enzi yote tunakushukuru kwa wakati huu na saa hii, mruhusu roho wako mtakatifu awe nasi, atuongoze tunapotafakari pamoja juu ya siku muhimu sana ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo, amen. Katika Injili ya Luka 2:14 mwandishi Luka anasema, “Atukuwe Mungu juu mbinguni na duniani iwe amani kwa watu aliowaridhia.” Wimbo huu ni lugha ya malaika ambao wanaimba kwamba atukuzwe Mungu, utukufu uwe kwa Mungu mbinguni na duniani iwepo amani kwa watu wote ambao Mungu amewaridhia waweze kuwepo.

'

Unaweza kujiuliza kwa nini wazungumze juu ya ujumbe wa amani duniani badala ya kuzungumza utukufu kwa Mungu? Ukisoma maandiko unaona wazi kuwa, Kristo anahusishwa na amani duniani. Mazingira ya wimbo huu yanaweza kurudisha nyuma sana, kwa nini Kristo anapozaliwa inaonekana amani imekuja duniani. Hapo nyuma kabla ya Kristo kuzaliwa nini kiliondoa amani duniani? Tukirudi katika kitabu cha Mwanzo tutaona habari ya uumbaji, maandiko yanasema Mungu akaumba dunia na kila kitu kikawa chema kabisa na katika kukamilisha wema ule akamuumba mwanadamu kwa sura na mfano wake Mungu.

Wanadamu wakafurahia maisha, lakini tunu ya furaha na amani ile ikapotea mara moja baada ya anguko la dhambi. Wazazi wetu wa kwanza Adam na Hawa walipoamua kuasi, dhambi ikaingia duniani, amani ikatoweka. Kwa nini ilitoweka? Kwa sababu dhambi ilipoingia duniani haikumuacha mwanadamu salama. Maandiko yanasema, siku utakapokula tunda utakufa. Japo kimwili ilionekana kuwa hai lakini dhambi ilipoingia duniani yapo mengi yaliyokufa. Kwa sababu hiyo amani haikuwa sehemu ya maisha ya mwanadamu. Jambo la kwanza kwa dhambi ile, uhusiano kati ya Mungu na mwanadamu ulivunjika. Mwanadamu aliyezoea kutembelewa na Mungu katika saa za kupigwa na jua, sasa Mungu anamuuliza Adam uko wapi? Anajibu, niliposikia sauti yako nikaogopa, nikajificha. Hivyo amani ilitoweka.

Jambo la pili, kwa dhambi ile amani kati ya mwanadamu na mwanadamu ilitoweka, Adam ambaye mwanzoni alijivunia Hawa na kumtaja kwa sifa zake, mifupa katika mifupa yangu, nyama kati ya nyama yangu lakini baada ya anguko akiulizwa je umekula tunda nililokukataza usile, anajibu “ni huyu mwanamke ambaye umenipa.” Sio sura tena ya urafiki bali sasa ni sura ya uadui, kwamba ‘huyu ni tatizo’ mwanadamu kumuona mwenzake ni tatizo. Ukisoma katika maandiko yanasema Adam akaambiwa kwa sababu umekula tunda nililokataza usile, ardhi sasa imelaaniwa kwa ajili yako.

Michongoma na miiba itakuzalia, kwa tabu kwa jasho utakula. Ardhi iliyokuwa imeandaliwa kuwa baraka kwa mwadanamu na humo afurahie maisha kwa amani, inabadilika na inafika mahali mpaka mwanadamu aumie sana ndipo aweze kula, kwa jasho.

Kwa hiyo kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo katika (Krismasi) ni siku ya kipekee na muhimu kwa sababu inamrejeshea mwanadamu matumaini yaliyokuwa yamepotea katika bustani ya Eden pale Adam wa kwanza aliposhindwa, sasa Adam wa pili anazaliwa Yesu Kristo.

Huyu ndiye mwenye kurejesha uhusiano kati yetu na Mungu. Yesu anazaliwa na kutusogeza karibu na Mungu, yeye anaitwa Emmanuel yaani Mungu pamoja nasi.

Sikukuu hii ya Krismasi pia inarejesha uhusiano baina yetu sisi na sisi. Unapomuona mwingine ni tatizo Yesu anapozaliwa tunamuona mwingine kwamba ni sehemu ya baraka katika watu tulioumbwa kwa mfano na sura ya Mungu pasipo kujali tofauti zetu.

Jambo la tatu, Yesu Kristo aliye mkombozi tunaona kabisa baraka zetu za ukombozi kwa ulimwengu tuliowekwa kuishi tunazipokea sasa.

Tunapozungumza katika Krismaisi ni kuondoa katika tafsiri iliyozoeleka kwamba ni kipindi cha kufanya sana biashara na kufuta hasara zilizopatikana katika vipindi vingine. Sawa, maisha ya kila mmoja anafanya kwa kipawa alichopewa, lakini Krismasi ni zaidi ya biashara.

Wengine wanatumia vibaya, wengine wachafu na hapa unaweza kujiuliza je tunawezaje kumuenzi msafi kwa machafu? Kama aliyezaliwa ni msafi na mtakatifu lazima tumuenzi kwa usafi.

Yesu azaliwe ndani yetu ili ukristo wetu uwe na thamani. Tukisoma historia ya kanisa la kwanza wenzetu waliitwa Wakristo kwa sababu maisha yao walipoandaliwa walimuona Kristo.

Wapo watu hawana amani na wake zao, waume, familia, sehemu za kazi na hawana amani na watu wote wanaowazunguka. Mungu atusaidie na kutupatia neema ili tunapomaliza mwaka 2018 tuumalize tukiwa na amani na kuupokea mwaka mwingine kwa amani. Kuzaliwa kwa Kristo kutakuwa na maana kubwa sana. Mungu akubariki sana kijana unayenisikiliza, tafakari amani yako na wengine.

Chanzo: mwananchi.co.tz