Dar es Salaam. Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Zanzibar, Augustino Shao amesema kinachoendelea hivi sasa nchini Tanzania kuhusu tuhuma za uhujumu uchumi kwa watu mbalimbali ni matokeo ya kujilimbikizia mali, kutotumia utajiri wao kuwasaidia wengine.
Amesema ubinafsi wa kutaka mali kumnufaisha mtu mmoja au familia yake ni kikwazo kikubwa katika uchumi hasa wa Taifa linaloendelea kujijenga.
Ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Oktoba 24, 2019 wakati akifungua warsha ya siku mbili inayohusu masuala ya uchumi kwa vijana.
Askofu Shao amesema jambo hilo linapaswa kutafutiwa ufumbuzi, kubainisha kuwa hatua inayochukuliwa sasa na serikali imedhihirisha ni kiasi gani matajiri wanashindwa kutumia fedha zao kusaidia wengine na Taifa.
“Sasa hivi wahujumu uchumi wanakiri na kuomba msamaha na ama haitoshi wanarudisha fedha, hebu tujiulize fedha zile zote zilikuwa wapi.”
“Unawezaje kurundika benki kiasi kikubwa vile cha fedha wakati ungeweza kuzizungusha kwenye uchumi, ukatengeneza ajira na kuokoa maisha ya watu,” amesema.
Pia Soma
- Mchakato wa kampuni 100 bora waanza
- Rugemalira mgonjwa, ashindwa kufika mahakamani
- Wanafunzi wa Chuo Kikuu Makerere wavamia kituo cha polisi