Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: Askofu Cheyo aonya matumizi ya mitandao ya kijamii, kwaya kuchangisha waumini

Video Archive
Fri, 27 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mbozi. Askofu wa Kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la Kusini Magharibi, Alinikisa Cheyo ameonya wale wote wanaotumia mitandao ya kijamii kuandika mambo machafu na kutukana wengine kuwa wanahatarisha amani ya nchi.

Askofu Cheyo amesema hayo leo Jumatano Desemba 25,2019 wakati akitoa salamu za Krisimasi katika ibaada la Kanisa la Moravian Vwawa mjini wilayani Mbozi mkoani Songwe kuwa amani na umoja wa nchi unapaswa kulindwa na kila mmoja ili watu waweze kufanya kazi ya kujiletea maendeleo yao na ya nchi kwa ujumla.

"Wapo wenzetu ambao wanatumia vibaya elimu na uhuru wa habariĀ  kuharibu amani yetu, aidha kwa kutumika na watu wasioitakia mema nchi yetu na hao nawaambia nchi hii ndiyo tuliyopewa na Mungu tunapaswa kuilinda," amesema Askofu Cheyo.

Askofu Cheyo ametumia pia nafasi hiyo kutuma salamu za kumtakia heri Rais wa Tanzania, John Magufuli kwa kazi njema ya kuliongoza Taifa hili.

Katika salamu hizo, Askofu Cheyo ameviomba vikundi vya uimbaji katika madhehebu ya dini kuwa vikundi vya kiuchumi ili kuvifanya vijitegemee badala ya kutegemea michango ya waumini.

Amesema mtindo uliopo hivi sasa wa vikundi vya kwaya kutaka kununua vyombo vya muziki vyenye thamani kubwa kwa kuchangisha watu halafu vikiharibika wanarudi kuchangisha sio mzuri.

"Ndugu zangu lazima tutumie akili zetu tujiongeze kujiimarisha kiuchumi, ni vizuri vikundi hivi vya kwaya vianze kujigeuza kuwa vya kiuchumi anzisheni kwanza miradi halafu baadaye mnunue vyombo vya muziki muepukane kuwachangisha waumini na hata wengine ni wazee wana hali ngumu lakini wanalazimika kuwachangia" amesema Askofu Cheyo.

Amesema Mungu mwenyewe hapendi watu wake wawe masikini na hivyo amewataka waumini wa kanisa hilo kuamka na kutumia fursa mbalimbali kujiletea uchumi.

Chanzo: mwananchi.co.tz