Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Unavyoweza kupata kibali cha Mungu ili ufanikiwe

37551 Mahubiri+pc Unavyoweza kupata kibali cha Mungu ili ufanikiwe

Tue, 22 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Bwana Yesu asifiwe. Naitwa Nabii Elisha Muliri kutoka Kanisa la Ebenezer lililopo Kinondoni Studio jijini Dar es Salaam.

Jumapili ya leo napenda kuzungumza nawe msomaji wa gazeti la Mwananchi juu ya jambo moja muhimu sana linaloitwa ‘kitu kikavu’. Kitu kikavu kwenye mahubiri haya ni kile kisicho na msaada wowote kwa sababu kimekauka.

Nitasoma neno la Mungu kutoka katika kitabu cha Ezekiel 37:1. Biblia inasema, “Mkono wa Bwana ulikuwa juu yangu, naye akanichukua nje katika Roho wa Bwana akaniweka chini katika bonde, nalo limejaa mifupa, akanipitisha karibu nayo pande zote natazama palikuwa mifupa mingi katika uwanda, nayo tazama ilikuwa mikavu sana.”

Ezekiel alikuwa nyumbani kwake, Biblia imeandikwa kwamba alichukuliwa na Roho wa Bwana na kupelekwa kwenye bonde la mifupa mikavu.

Kiuhalisia unatakiwa kupenda kuchukuliwa na Roho wa Bwana kwa sababu akikuchukua atakupatia uwezo wa kufanya vitu visivyowezekana kufanywa kikawaida.

Roho wa Bwana akikuchukua anaweza kukutoa mahali ulipo akakuweka kwenye nafasi nyingine kabisa kiasi cha kuwashangaza wanaokuzunguka waliozoea kukuona wa kawaida.

Biblia inasema mifupa mikavu na kila mtu anajua unaposema mifupa mikavu ni au ilikuwa ya wanyama au binadamu.

Mifupa mikavu ni matokeo ya kisa cha mtu au mnyama aliyekuwa hai na sasa amekufa. Kwa lugha nyingine, mifupa mikavu ni ya kiumbe hai kilichokufa ambacho hakina uwezo wa kutembea wala kufanya chochote kwa sababu kimekufa.

Katika maisha ya kawaida ukiwa mkavu huwezi kumiliki mali, huwezi kuwa na pesa na wakati mwingine unakosa marafiki wala chochote cha kujivunia.

Wapo watu wakavu katika ulimwengu wa roho ambao japo wanapendeza machoni, lakini wamepoteza tumaini. Watu hawa wamezungukwa na mambo magumu, wengine wamesoma ila hawana kazi, hawana rafiki wala ndugu anayeweza kusimama nao, pia wamezungukwa na madeni makubwa. Biblia inasema Ezekiel alichukuliwa na Roho wa Bwana akapelekwa kwenye hilo bonde na kuulizwa je mifupa hii inaweza kuishi tena?

Ukweli ni kwamba hakuwa na jibu kamili kama kweli mifupa mikavu inaweza kuishi lakini ilibidi ajibu ukweli, akasema “mimi sijui ila wewe Bwana unajua.”

Mpendwa msomaji ni vizuri wakati unapokuwa hujui jambo useme ukweli kwamba hujui ili uweze kusaidiwa ujue.

Kwa sababu Ezekieli alijibu vile, Mungu akamwambia, “basi ni wewe utatabiri juu ya mifupa hii na mifupa hii inaweza kuishi tena.” Kumbe ukitamka kitu kilichokauka kwenye maisha yako kinaweza kupata uhai tena.

Wacha nikuambie ukweli, kuna vitu usingoje mtu mwingine aongee kuhusu maisha yako. Mungu anataka wewe mwenyewe utamke kwa kinywa chako.

Ndio maana unaona hata mahakamani kuna wakati wakili au shahidi anaongea lakini wakati mwingine wewe mwenyewe mwenye kesi unatakiwa kuongea.

Mtu yeyote anahitaji kuwa na uwezo na uhuru wake wa kujitetea kama mwanadamu. Unaweza ulizwa swali ukataka mtu mwingine akujibie au kwenye kikao linaulizwa swali nawe unasema “kama yule alivyosema”, hapana. Jibu wewe mwenyewe. Mungu alimwambia Ezekiel ni wewe mwenyewe sio mwingine.

Mungu alikuwa anamtafuta mtu mwenye imani kuitabiria mifupa iweze kuishi tena, Ezekiel alionekana. Inawezekana kwenye familia yako kuna mifupa mikavu mfano magonjwa, njaa, dhiki ukawa ni chanzo cha ukombozi. Mungu anataka imani yake ili usimame kwa ajili ya ndugu zako.

Kuna wakati familia inahitaji mtu kama Ezekiel aweze kutamkia mema familia yake. Usiulize utaanzaje? Unaweza kuanza tu kutamkia mema na Mungu akakupatia kibali.

Biblia imeandikwa mtu atakula matendo ya kinywa chake. Wewe tamka mema hata kama wakati mwingine huna pesa wewe tamka tu “mimi ni tajiri.” Hata kama huna mtu wa kukusaidia tamka tu kwamba, Mungu ataniinulia mtu nami nitakuwa salama.

Jambo la msingi unalotakiwa kufanya ni kuwa na imani. Inawezekana umesoma sana ndio, ila huna kazi na umehangaika sana kuipata licha ya sifa ulizonazo kwa sababu hauna connection (muunganiko).

Inawezekana huna pesa kabisa na wallet yako ikawa inajazwa karatasi tu na vocha zilizokwanguliwa kwa sababu umekosa tu mtu wa kukushika mkono. Mishipa kwenye mwili ni muhimu sana sawa na connection, lakini pia unaweza kuwa na hiyo connetion watu wakakukubali lakini ukakosa kibali.

Anayeweza kukupatia kibali ni Mungu. Kibali anachoweza kukupatia Mungu kitakufanya upenye kwenye jambo lolote lile gumu.

Itaendelea wiki ijayo



Chanzo: mwananchi.co.tz