Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Unaitambua mamlaka aliyokupa Mungu? Ukiitumia utapenya

39807 Pic+mahubiri Unaitambua mamlaka aliyokupa Mungu? Ukiitumia utapenya

Mon, 4 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Naitwa Mchungaji Christosiler Kalata kutoka Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Mbezi Beach, Dayosisi ya Mashariki na Pwani.

Leo tunaongozwa na Neno la Mungu kutoka katika kitabu cha Mathayo 16:18 – 19.

Biblia inaandika; “Nami nakuambia, Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu; wala milango ya kuzimu haitalishinda. Nami nitakupa wewe funguo za ufalme wa mbinguni; na lolote utakalolifunga duniani, litakuwa limefungwa mbinguni; na lolote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni.”

Maneno haya ya Yesu Kristo yanatuonyesha mamlaka ambayo Mungu amelipatia kanisa lake kuwa lina nguvu kubwa na mamlaka kuliko shetani.

Kanisa ni mwili wa Yesu mwenyewe na wakristo wameokolewa kwa damu ya Yesu wakati alipowambwa msalabani kwa ajili ya ondoleo la dhambi zetu.

Wakristo tuliookolewa ni wana wa ufalme. Yesu Kristo anapotamka maneno haya kuwa atalijenga kanisa lake wala milango ya kuzimu haitalishinda, maana yake ni kwamba, kila mkristo aliye katika dunia hii amepewa mamlaka, uwezo na nguvu na anajengwa kiroho awe na uwezo wa kumshinda shetani.

Kupitia neno hilo, hakuna mlango wa kuzimu utakaomshinda kwa sababu Neno la Mungu limemuahidi hivyo.

Wewe Mkristo unatakiwa kufahamu jambo hili kwamba Yesu Kristo hawezi kutuambia au kutupa kitu ambacho hakina nguvu au mamlaka.

Hawezi kutuambia tufunge kama hakuna kitu cha kufunga, fikra zetu zinapofunguka, tutafahamu kuwa kuna mambo ambayo tunatakiwa kuyafunga na yasitusumbue katika maisha yetu.

Kuna vitu vya kuvifungua ili tuwe na ustawi katika Kanisa na jamii kwa ujumla. Swali hapa ikiwa tumepewa siri hii, kwa nini bado ufahamu wetu umefungwa?

Uwezo na mamlaka tuliyopewa na Yesu Kristo yanatufanya tusihofu kwa sababu yeye ndiye aliyetupa funguo za ufalme wa mbinguni.

Ikiwa tumepewa mamlaka haya, haipendezi kuendelea kukaa katika umaskini, ujinga na maradhi.

Tumeamua kupambana na umaskini, hebu na tutumie rasilimali alizotupa Mungu kuondokana na hali hiyo. Tunaweza kufuta ujinga kwa kuhakikisha tunapata elimu.

Tunaweza kupambana na adui maradhi, kwa kujenga hospitali, kusomesha madaktari, funguo hazitakuwa na maana ikiwa nchi na Kanisa litakosa ustawi, uchumi bora, miundo mbinu bora, umeme wa kutosha, maji safi, usafiri madhubuti na wa uhakika.

Yesu Kristo katukabidhi funguo, katufundisha namna ya kuzitumia, hawezi kutukabidhi, uwezo na mamlaka bila kutufundisha namna ya kuyatumia. Ndiyo maana Rais John Magufuli ameomba Watanzania tumuombee.

Anajua kwamba anaweza kufanya kazi ya kupambana kuinua uchumi wa nchi kwa uwezo wa Mungu kwa sababu, ameshakabidhi mamlaka ya kufunga na kufungua.

Hii ina maana kuwa akifanya kitu chochote katika mapenzi ya Mungu nchi inapata ustawi na Mungu atakuwa upande wake.

Funguo ni mamlaka. Kazi ya funguo ni kufunga na kufungua.

Yesu Kristo ametupa funguo za ufalme wa mbinguni, maana yake ni kwamba ametupa ‘mamlaka’ ya ufalme wa mbinguni.

Ikiwa tumepewa funguo za ufalme wa mbinguni mwaka huu 2019, ni wakati wa kufunguliwa na kufikia mafanikio.

Tumehangaishwa sana, tumeona mwaka uliopita Mungu akitupitisha katika mambo mengi, hatuna budi kumshukuru na sasa anapenda kutupeleka hatua nyingine zaidi.

Tunatakiwa kubadilika kifikra tuache kusumbua watu kwa maneno yasiyo na faida, tufanye kazi kwa mikono yetu na kwa bidii.

Usikatishwe tamaa na watu ambao wanaishi kiujanjaujanja, miaka 57 ya nchi hii imetosha kukupatia picha halisi ya ulivyokuwa unaishi na unakoelekea.

Unayo mamlaka ya kukemea watu wanaotumiwa, kutaka kututoa katika njia kwa sababu Biblia inaandika, “Lolote utakalolifunga duniani, litakuwa limefungwa mbinguni.”

Kila Mtanzania kwa kuitumia funguo hii, maana yake Mungu atausimamia uamuzi wake wa kulifunga jambo ambalo halina tija kwa Taifa.

Tukiamua kulifunga jambo, Mungu atalifunga pia, wewe Mkristo, wewe Mtanzania, amua sasa kwamba tunaweza kuifanya Tanzania kuwa kama nchi za wenzetu zilizoendelea.

Wewe unaweza kufanya, fanya.



Chanzo: mwananchi.co.tz