Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ujumbe wa Dk Bilal katika mashindano ya kuhifadhi Quran

57018 Pic+bilali

Tue, 14 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Makamu wa Rais mstaafu, Dk Mohamed Gharib Bilal amewataka viongozi wa dini nchini  kuhamasisha vijana kusimama katika misingi  imara ya dini ili waishi katika uadilifu,  amani na utulivu.

Ametoa rai hiyo leo Jumapili Mei 12  katika fainali ya mashindano ya Afrika Mashariki ya kuhifadhi Quran tukufu ya yaliyoandaliwa na taasisi ya Al- Manahilul Irfan Islamic Center na kufanyika katika viwanja vya Sabasaba, jijini Dar es Salaam

Amesema katika nyakati hizi za mabadiliko ni muhimu kwa viongozi wa dini kuhamasisha mashindano ya Quran ili kujenga imani kwani imani ikisimama imara hakutakuwa na upotoshaji, uhasama wala mambo  mabaya.

"Mashindano haya ni ishara njema tuzidi kuhamasisha vijana wadogo washiriki kuhifadhi Quran kwa sababu aliyeihifadhi hawezi kuwa mpotoshaji wala kupotosha watu,” amesema Dk Bilal.

Mufti wa Zanzibar, Swalehe Omary amesema mwezi wa Ramadhani ni mwezi mtukufu wa mavuno.

Aliwataka Waislamu kuhakikisha wanahifadhi na kuisoma Quran ili kuishi kwa amani na uadilifu.

Pia Soma

Amebainisha kuwa Quran imeweka wazi batili na haki na inakataza rushwa, ubadhirifu na ikifuatwa watu watakuwa salama katika mioyo yao.

Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum aliyemwakilisha Mufti wa Tanzania, Sheikh  Abubakar Zuberi  aliwataka Waislamu waishi na watembee kwa mujibu wa Quran.

Naye mratibu wa mashindano hayo ya Quran, Sudi Mussa

amesema ni mashindano ya 11 na kwamba wakati wa uandaaji walikumbana na changamoto ya wafadhili kujitoa.

Mussa amesema kwa sasa hawana wafadhili baada ya kujitoa na kuomba wadau mbalimbali na  taasisi kufadhili mashindano hayo kwa sababu yanasaidia kuwafundisha vijana kuacha mambo mabaya na kuwajenga kusimama katika imani.

Katika mashindano hayo washiriki watano walishindana katika kuhifadhi juzuu tano na washindi sita walishindana kuhifadhi juzuu 30.

Mshiriki kutoka Temeke Lailatu Hassan (8) aliibuka mshindi wa kwanza katika kuhifadhi Quran juzuu 5.

Kwa upande wa kuhifadhi juzuu 30, Mtanzania Omary Abdallah aliibuka mshindi kwa alama 99.3, akifuatiwa na mshiriki kutoka Uganda,  Usama Idrisa ambaye alipata alama 99.1 na mshiriki kutoka Kenya, Muslim Haji yeye alipata alama 99.

Chanzo: mwananchi.co.tz